Matamasha Simba, Yanga yaanzie mikoani kilele Dar

08Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Matamasha Simba, Yanga yaanzie mikoani kilele Dar

WAKATI Klabu ya Yanga iliadhimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi Jumamosi iliyopita, watani wao wa jadi, Simba leo wataadhimisha Tamasha lao maarufu kama Simba Day lililoasisiwa miaka 13 iliyopita chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali.

Jumamosi Yanga iliadhimisha tamasha lao hilo maarufu kama Siku ya Mwananchi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, likiwa ni la nne tangu liasisiwe katika klabu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.

Kwa ujumla tamasha hilo lilifana na si hilo tu bali kila mwaka klabu hizo zimekuwa zikiboresha matamasha yao hayo kwa kuja na vionjo tofauti ambavyo huwa vivutio vikubwa kwa mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi, jambo ambalo kusababisha Uwanja wa Mkapa kufurika.

Pamoja na mambo mengi mazuri na ya kuvutia ambayo hufanyika wiki moja kabla ya kilele cha matamasha hayo, kubwa ambalo Nipashe tumekuwa tukivutiwa nalo ni namna ambavyo klabu hizo hufanya shughuli za kijamii ikiwamo kurudisha kidogo walichokipata msimu mzima kwa kusaidia wasiojiweza na wenye mahitaji maalum.

Hilo hufanyika likiambatana na viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hizo kujitokeza kujitolea damu kwa ajili ya kwenda kusaidia wagonjwa wenye hitaji hilo katika hospitali mbalimbali, kwani zoezi hilo hufanywa na wapenzi wa klabu hizo kote nchini.

Kinachotufurahisha zaidi ni mwitikio mkubwa kwa wanachama na mashabiki wa timu hizo kote nchini, kwani wiki ya matamasha hayo inapotangazwa matawi ya klabu hizo katika mikoa na wilaya mbalimbali hujikusanya na kuanza kufanya shughuli hizo za kijamii kwa kutoa misaada na kuchangia damu, jambo ambalo tunaona ni zaidi ya upendo, hivyo hatuna budi kuwapongeza.

Hata hivyo, tunatamani kuona wigo mpana zaidi kwa klabu hizo kwa sasa kufikiria matamasha hayo kuanzia mikoani na kisha kielele chake kufanyika Dar es Salaam ili kuzifikia jamii kila kona nchini lakini pia wanachama na mashabiki wa timu hizo kufurahia burudani zaidi mubashara.

Tunatambua haitakuwa rahisi kwa klabu hizo kupeleka matamasha hayo kila mkoa hasa kutokana na maandalizi ya msimu mpya kuwa mdogo, hivyo kwa kuanza zinaweza kufanya kwa kanda moja moja mfano mwaka ujao Kanda ya Ziwa, unaofuata Kanda ya Kati, kisha Kanda ya Kaskazini na nyinginezo.

Tunaamini inawezekana kabisa kwa klabu hizo kila moja kufanya matamasha makubwa mawili moja katika kanda moja kabla ya kilele kufanyika Dar es Salaam, jambo ambalo si tu litaziingizia mapato makubwa bali litasaidia pia kuzifikia jamii ambazo zinahitaji nazo kusaidiwa kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa Dar es Salaam.

Ni wazi matamasha hayo yakifanyika klabu hizo zinaweza kuandaa utaratibu mzuri wa kuuza jezi na bidhaa nyingine za klabu kwa wingi, mbali na mapato ambazo zitaingiza kwa mashabiki wao kuhudhuria uwanjani siku hiyo.

Lakini kama ni umuhimu wa kupoteza mvuto siku ya kilele kwa kuwa utambulisho wa wachezaji wapya tayari utakuwa umeonekana kupitia TV, bado zinaweza kufanya jambo kama hilo kwa kuanzia Dar es Salaam na kisha kuchagua kanda mojawapo kwenda kucheza mechi moja kubwa ya kirafiki ambayo itaambatana na burudani zote ili kuwaleta karibu mashabiki wao.

Nipashe tunatamani kuona timu hizo kongwe nchini ambazo zimeteka mashabiki wa soka kila kona, zikiwa chanzo kikubwa cha kivutio cha utalii Tanzania kwa kutumia kila tone la fursa ambalo linaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato lakini pia zikitumika kuutangaza mpira wa Tanzania ndani na nje ya nchi ili kuvutia wawekezaji wakubwa zaidi.

Leo hii tunaona uwekezaji mkubwa katika soka ukiongezeka hadi klabu ndogo kama Singida Big Stars ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu ikiwa na wadhamini kibao jambo ambalo limeifanya kuweza kusajili nyota kibao wa kigeni wakiwamo watano kutoka Brazil.

Tunaamini kupitia Simba na Yanga, ambazo zinajulikana zaidi ndani na nje ya nchi kama ambavyo zinalitangaza soka letu kwa sasa, bado zinaweza kufanya jambo kubwa zaidi kupitia matamasha hayo kwa kuwa chanzo kikubwa cha wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza kwa klabu zetu.