Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na wakufunzi kutoka katika shirikisho la mchezo huo Afrika (CAF) na FIFA, hivi karibuni limemaliza semina za waamuzi kwa ajili ya kuchezesha ligi hiyo kwa weledi.
Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inadhaminiwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ndio inayotoa wawakilishi wa Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika, pamoja na michuano ya Kombe la FA.
Na sasa kwa msimu wa pili mfululizo, Tanzania Bara inawakilishwa na timu nne katika mashindano hayo yanayoandaliwa na kusimamiwa na CAF, hiyo imetokana na hatua nzuri iliyofikiwa na Simba kwenye michuano hiyo.
Waamuzi ambao wanakumbushwa kufuata weledi si wale wa Ligi Kuu Tanzania Bara pekee, hata wale wanaochezesha Kombe la FA kuanzia hatua ya awali, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake Nchini.
Na kwa upande wa visiwani, Ligi Kuu Zanzibar na Kombe la ZFF ndio hutoa timu zinazoshiriki mashindano ya CAF, kila mwaka.
Ili ligi ipate bingwa wa nchi anayestahili au aliyetokana na ubora wa kikosi chake, ni lazima waamuzi wanaopewa dhamana wachezeshe mechi zote kwa kufuata sheria za mchezo huo unaopendwa zaidi duniani na si vinginevyo.
Waamuzi watakapopindisha sheria za mchezo huo, ni wazi timu zitakazotwaa ubingwa zitakuwa zisizostahili, lakini pia nchi itapeleka timu dhaifu kwenye mashindano ya kimataifa na matokeo yake wawakilishi hao watatupwa nje ya michuano hiyo mapema.
Umefika wakati waamuzi kuongeza umakini na weledi katika kutekeleza majukumu yao na kwa kufanya hivyo, itapunguza malalamiko na lawama mbalimbali kutoka kwa timu, wachezaji, viongozi na wadau wa michezo hapa nchini.
Mbali na kumaliza kero hiyo ambayo wakati mwingine inatafsiriwa inalenga kuzinufaisha baadhi ya timu, pia itawajengea sifa waamuzi kwa kupandishwa daraja na hatimaye kupangiwa mechi za kimataifa kama ambavyo kwa sasa mwamuzi msaidizi, Frank Komba anavyopata uteuzi wa michezo mbalimbali ya CAF.
Kuchezesha kwa haki kutawafanya wachezaji waendelee kujituma na kutokata tamaa hata pale wanapofungwa kwa sababu wanafahamu mchezo wa soka una matokeo ya aina tatu.
Haipendezi na haijengi katika dunia ya sasa ya utandawazi ambapo michezo yote 240 ya Ligi Kuu Tanzania Bara huonyeshwa mubashara, kama waamuzi watachezesha vibaya na hatimaye kupelekea kuvunjika kwa mechi au kutokea kwa vurugu.
Waamuzi wanapokuwa chanzo cha kutokea kwa matukio yasiyokuwa ya kimichezo au ya utovu wa nidhamu yanapunguza heshima ya maofisa hao, lakini pia huwanyima haki wale waliostahili kupata ushindi katika mechi husika.
Tunaamini semina ambazo TFF imewaandalia waamuzi zitazaa matunda na msimu mpya wadau watashuhudia burudani na si mauzauza ambayo yamewahi kutokea katika miaka ya nyuma.
Klabu zimesajili wachezaji wenye viwango vya juu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo wanahitaji kuona haki inatendeka lakini pia tunasaidia kuwaimarisha na wanapoitwa kwenye timu za Taifa, wanakuwa imara na tayari kushindana na si kutegemea kufunga mabao kwa njia za ujanja ujanja.
Kila la kheri timu zote zinazotarajia kuchuana katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League, Ligi Kuu ya Wanawake Nchini, Kombe la FA, Ligi Kuu Zanzibar , Ligi Kuu ya Wanawake Zanzibar na mashindano ya Kombe la ZFF.