Sababu kubwa inayotawala hapo ni tamaa ya kujipatia mali. Hilo limetamkwa na Diwani wa Viti Maalum wa Kata ya Garula, Pascalina Shitundu, akiwatuhumu wanawake wenzake kwenye kijiji cha Ilasilo.
Diwani huyo ‘akawapasha’ wanawake wenzake kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Shirika la Maendeleo la ADP, linalohusika na masuala ya chakula cha familia.
Mwanasiasa huyo ‘akawapasha’ kinamama wenzake, akiwapa ‘vipande’ vyao kwamba wanakiuka haki za msingi wa watoto, kwa kuchochea waelekee kwenye ndoa za utotoni na huo unahesabika ni ukatili wa kijinsia.
"Ninasikitika kwamba wanawake wenzangu ndiyo mnawahamasisha watoto wasifanye vizuri kwenye mtihani ili muwaozeshe. Sasa unamuozesha mtoto mdogo ili akafanye nini kwenye ndoa? Nawaombeni wanawake wenzangu tuwasaidie watoto wetu," akasema diwani huyo.
Ni kweli, hilo analolisema halipo Songwe peke yake, ila limetawanyika katika maeneo mengi sana na hasa vijijini. Kwa mtazamo na uzoefu wangu, ni afadhali mjini ambako kuna mwamko na watu wana hofu ya mkono wa sheria, kwa sababu vyombo vya serikali na dola vipo karibu na vinaangaza.
Mara zote vyombo hivyo vinaponusa uovu, basi havifumbii macho. Tatizo vijijini bado kuna baadhi ya utamaduni mbaya unaoendelea kutekelezwa hadi sasa na ndiyo maana, hata ikitokea hali kama hiyo uongozi wa kijiji unafumbia macho, kwa sababu baadhi yao wanaamini kwenye hilo.
Huwa najiuliza, hivi kweli watu hao wanakuwa wanawaza nini? Kwa kifupi mimi hapa nawaingiza na wanaume kwenye sakata hili pia.
Kwanza, wao ndiyo wanaokwenda kuwaoa mabinti ambao ni wanafunzi. Pia, waume za hao wanawake nao wanahusika, kwani kwa mujibu wa utamaduni wetu Waafrika kwa sehemu kubwa, ni kwamba wanaume ndiyo waamuzi wa mwisho katika yanayotuhusu.
Kama baba huyo hataki mtoto asiolewe ni kweli haolewi na kama anataka asome atasoma. Ni kweli diwani ‘amewachana’ wanawake wenzake, lakini hapo kwa asilimia kubwa wanaume nao wanahusika, kwa sababu inaonekana wanabariki matendo ya wake zao.
Huo utamaduni nadhani sasa umepitwa na wakati. Zamani wazazi walikuwa wanajitahidi tu kusomesha wanaume na kuwaacha mabinti nyumbani. Madai ni kwamba, mwanaume ndiyo anatakiwa asome ili ajitegemee, apate kazi na awe na familia yake aweze kuihudumia.
Lakini, dhana ikabaki mwanamke yeye ni mtu wa kuolewa hata kama hajasoma, atamtegemea mume kwenye maisha yake, akimtunza na kumjali kwa shida na raha.
Kwa sasa hilo lipo, lakini likibeba mageuzi makubwa na sura mpya. Wanawake wanaolewa kwa sababu ni jambo la heshima na utaratibhu wa maisha, ikiwa ni mahitaji ya kibinadamu, pia kiimani.
Siku hizi wanawake nao wanatunza hata wanaume.
Kwa miaka ya karibuni, kuna mageuzi dunia nzima kuhusu wanawake na wanaume.
Wanawake wamesoma, wamejiendeleza, wamekuwa wafanyabiashara wakubwa na akili kubwa kwenye uongozi pengine hata kuwapiku wanaume.
Kinamama hao, hata katika mfano wa uongozi kitaifa sasa wameshika usukani, hata kurudi kwa walioko shule ngazi ya msingi hadi vyuoni, wanaongoza kwenye matokeo ya ufaulu.
Huo unafaa kuwa mwongozo kwetu sote na hasa wazazi kuondokana na imani za kutosomesha wanawake, kwani wameonekana wanaelimika vizuri zaidi na hata kuzaliwa viongozi bora.
Inasikitisha kuona mzazi analazimisha binti asijibu mtihani wake vizuri kwa kuogopa atafaulu kwa hiyo ataendelea kusoma, badala ya kuolewa.
Wazazi wasiwe na tamaa ya mali za mapema. Mali ambazo wanapewa mara moja na kumalizika, huku binti akiendelea na mateso kwa mume.
Rai yangu ni kwamba wasomesheni watoto wa kike, ili wakipata maisha yao wawasaidie moja kwa moja, bila ya kupigia magoti wanaume ambao nao, baadhi yao wanadumu na fimbo hiyo kuwachapa wao.
Uchunguzi wangu mdogo tu kwenye jamii, nimegundua pia watoto wa kike ndiyo wanaowasaidia zaidi wazazi wao wanapoelimika au kuwa na kipato chao kuliko wa kiume.
Sina maana watoto wa kiume wasisomeshwe, la hasha, lakini ukweli ni kwamba wanaume wanapokuwa na pesa, husaidia au hutoa zaidi upande wa mke, yaani ukweni kuliko kwao kwa wazazi wake.
Lakini, wanawake msaada wao hupelekwa zaidi kwa wazazi wake. Hilo ni somo dogo nawapa wazazi kuwa kumsomesha mtoto wa kike ni kama vile umejiwekea akiba isiyooza.
Wazazi waache mabinti zao wasome, waje kuwa watu wakubwa kwenye nyanja mbalimbali, au wafanyabiashara, badala ya kuwaoza wakiwa hawana lolote badala yake wanakwenda kunyanyasika, kupigwa na kudhihakiwa, huku wao wakiwa hawana msaada wowote wakiogopa kudaiwa mahari waliyokula ambayo hawawezi tena kuilipa.