Waziri Ummy aliyasema hayo, aliposhiriki mbio za marathon zilizoandaliwa na Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu kwa watoto 200 wenye tatizo la kichwa kikubwa.
Alisema tatizo hilo linatokana na ukosefu wa madini ya ‘Folic Acid’, tatizo linaloweza kuzuilika, ikiwa wanawake walio tayari kuzaa wakitumia dawa hizo.
Taasisi mbalimbali za afya, ikiwamo Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) inaelekeza mama mtarajiwa kutumia vidonge hivyo miezi mitatu kabla ya kubeba ujauzito na wiki 12 za mwanzo za ujauzito huo.
Kituo hicho kinaeleza ulazima huo unatokana na vidonge hivyo kusaidia kuzuia kasoro kubwa katika ukuwaji wa mtoto anapokuwa tumboni mpaka kuzaliwa.
Kwa mantiki hiyo, kama kinamama watarajiwa wasipotumia vidonge hivyo ndani ya kipindi muhimu kinachoelekezwa na wataalamu wa afya ndipo kunasababishwa kuzaliwa watoto wenye matatizo hayo.
Hivyo basi, ili wazazi watarajiwa waweze kufuata maagizo hayo kwa umakini kuna haja ya wao kupanga uzazi kwa maana ya lini anatarajiwa kubeba ujauzito ili aweze kufuata utaratibu muhimu ikiwamo kumeza vidonge hivyo miezi mitatu kabla ya kupata ujauzito.
Ni wakati muafaka kwa wamama watarajiwa kuachana na dhana ya kubeba ujauzito kwa mazoea badala yake wakae na wenza wao na kuamua ni wakati gani wabebe ujauzito ili kufuata vizuri maelekezo ya wataalamu ya kumeza vidonge hivyo.
Daktari Bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Dk. Laurent Mchome, alisema kuwa taasisi hiyo inapokea watoto 700 hadi 1,200 wenye tatizo la vichwa vikubwa kwa mwezi na sababu kuu ikiwa ni lishe duni kwa wajawazito.
Dk. Laurent aliongeza kuwa kati ya watoto 100 wanauzaliwa, watoto watatu hadi wawili wana uwezekano wa kuzaliwa na mgongo wazi au kichwa maji.
Ukweli ni kwamba Tanzania tukiamua tunapunguza au kumaliza kabisa idadi hiyo inawezekana kwa kuwa mhusika mkuu ni mbeba mimba mwanamke akisaidiwa na mwenza wake hivyo watu hawa ni kiungo muhimu katika hatima ya mtoto anayezaliwa.
Lakini kuna hili kundi la pili la wanawake ambao hawapendi kutumia vidonge hivyo kwa sababu mbalimbali ikiwamo kuwa vinaharufu na ladha mbaya mdomoni. Dhana ambayo kama wanawake wasipoachana nayo itaongeza idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo.
Kama mwanamke, unaweza kuvumilia heka heka za mimba kama vile kichefuchefu, kuumwa kichwa, kutosikia hamu ya kula, kiungulia na kutapika kwa muda wa miezi tisa, hivi unashindwa nini kuvumilia harufu ya muda mfupi ya vidonge ambavyo vinakwenda kuokoa maisha ya mtoto wako?
Serikali inafanya juhudi kubwa kuzuia watoto wenye tatizo hilo kuzaliwa nchini, kwa kuboresha huduma ya uzazi hususani kabla, wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua ni jukumu letu kushirikiana nayo kwa kufuata miongozo yao na kutii maagizo yao ikiwamo hili la kutumia vidonge.
Wataalamu wa Afya na wadau wa uzazi salama wasichoke kuelimisha jamii kuhusu tatizo hili na namna linavyoweza kuzuilika ili kuiongezea nguvu serikali katika kufikia malengo ya utekelezaji wake na kuondoa kizazi tegemezi cha baadaye.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








