Watanzania tujenge utamaduni kusoma vitabu tuongeze maarifa

13Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watanzania tujenge utamaduni kusoma vitabu tuongeze maarifa

JANA Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilizindua machapisho manne ya vitabu vinavyotoa miongozo kwa waandishi wa habari namna ya kupata na kutoa taarifa kwa usahihi.

Ingawa kazi kubwa ya Baraza hilo ni kutoa miongozo kwa vyombo vya habari, lakini wananchi pia wanapaswa kutambua haki zao za kupata taarifa zikiwa sahihi na zinazozingatia usawa na weledi kwa kujisomea machapisho mbalimbali yanayoelimisha ili kujiongezea maarifa.

Vitabu vinavyochapishwa na Baraza hilo lengo lake ni kuvikumbusha vyombo vya habari jukumu la kuhabarisha umma kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi bila upendeleo au kumuumiza mtu mwingine.

Kazi ya kuchapisha vitabu hivyo inahusisha mambo mengi, ikiwamo wataalamu, muda na fedha ili kuwapa taarifa muhimu wananchi wa kutambua haki zao za kimsingi.

Baraza la Habari hufanya pia kazi ya upatanishi na usuluhishi inapotokea wadau na wananchi kuandikwa kwenye vyombo vya habari bila kupewa nafasi ya kujieleza na habari hiyo kuwa ya upande mmoja.

Kama wananchi hawatasoma vitabu vinavyozungumzia haki na sheria zinazowalinda, maana yake haki zao zitapotea bure na sifa yao kuharibika.

Wakati vitabu hivyo vikizinduliwa wadau walikumbushwa umuhimu wa pande zote za watoa taarifa, wapelekaji na wapokeaji kufahamu mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa kabla habari haijamfikia msomaji ili isimwathiri mtu yeyote.

Vitabu vilivyozinduliwa ni pamoja na kinachozungumzia jinsi ya kuripoti habari za watoto, ambacho kinakumbusha waandishi kuzingatia weledi na maadili ya uandishi kwa kuandika bila kumwathiri mtoto kwenye maisha yake ya baadaaye.

Kitabu kingine kinazungumzia mwongozo wa kupata na kutoa taarifa kwa waandishi wa habari na maofisa habari, ambacho kinakumbusha wajibu wa maofisa habari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari na kutoa taarifa kwa wakati wanapotakiwa kufanya hivyo ili umma uweze kupata haki ya kupata taarifa.

MCT pia imetoa chapisho linalozungumzia hali ya vyombo vya habari katika kipindi cha mwaka 2020 -2021 na sheria zinazonyima uhuru wa habari na chapisho lingine linahusu mafunzo ya uandishi wa jinsia kwenye vyombo vya habari.

Vitabu hivyo ni mwongozo mzuri utakaoviwezesha vyombo vya habari kuripoti habari zake kwa usahihi bila kuumiza upande wowote.

Wakati vitabu hivyo vikizinduliwa, Rais wa Baraza la Habari Tanzania, Jaji Juxon Mlay, aliwakumbusha waandishi wa habari na jamii kuvisoma vitabu badala ya kuvichukua na kuvifungia kwenye makabati huku wakiacha madini yaliyomo kwenye vitabu hivyo yakipotea bure.

Vitabu hivyo ni msaada tosha vitakavyowaongoza waandishi na wahariri kufanyakazi zao kwa ufanisi na kwa weledi.

 

Pia aliikumbusha jamii kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu ili kupata maarifa na kutambua wajibu wao wanapoona hawajatendewa haki katika kupashwa habari.

Katika ulimwengu huu uliotawaliwa na habari za mitandao ya kijamii, wananchi wengi wamepoteza ari ya kusoma vitabu na kuishia kusoma habari za mitandao ambazo sio zote zenye ukweli kama ilivyo kwenye machapisho ambayo huandika habari za kina.

MCT pia imeshauriwa kusambaza machapisho hayo kwenye vyuo, maktaba, vyumba vya habari, ili watu wengi zaidi waweze kuelimika kupitia madini yaliyomo kwenye machapisho hayo.