Lengo la ziara hiyo ni kukagua na kusimamia miradi inayotekelezwa na wizara na taasisi zake, kuzungumza na wananchi na kupokea kero, maoni, ushauri na kutoa majawabu na ufumbuzi na ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya nishati.
Aliitaja mikoa atakayofikiwa na huduma hiyo ni Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa, Sogwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Mtwara.
Maeneo yatakayopewa kipaumbele ni upatikanaji na matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, usambazaji wa umeme vijijini na vitongoji, upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Pia uboreshaji wa huduma zinazotolewa na taasisi za wizara, usambazaji wa mafuta salama na ya bei nafuu vijijini.
Tunaamini kupitia ziara hiyo Watanzania wengi wanaoishi maeneo ya vijijini wanakwenda kupata umeme ipasavyo, kuanzia walioomba kuunganishiwa na kulipa na wanaotamani kufikiwa na huduma hiyo.
Tunafahamu juhudi za serikali za kutaka kuwafikishia umeme wananchi wa vijijini kwa wakati kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), lakini baadhi ya makandarasi wamekuwa kikwazo kwa miradi hiyo.
Ili kuondokana na kero ya makandarasi katika kusambaza umeme, ni muhimu nchi ikajipanga vyema kwenye kuendeleza vyanzo vya nishati jadidifu kwa kuwa ndiyo msukumo wa dunia, lakini kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili huduma iwafikie wananchi wengine na kwa haraka.
Wakati tukiendelea na vyanzo vilivyozoeleka ni muhimu kuwekeza na kuwa makini na uwekezaji unaofanywa kwenye vyanzo vya nishati jadidifu ambavyo ni rafiki kwa mazingira ambavyo ni jua, upepo, mawimbi na upepo wa bahari na tungamotaka, ili inapofika ulazima wa kuachana na gesi, mafuta na maji kuwe na maandalizi ya kutosha.
Maji ni chanzo kizuri cha kuzalisha umeme, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi inapotokea ukame vyanzo hukauka na kushindwa kuzalisha nishati hiyo, mara kadhaa Tanzania imepitia mgawo sababu ikiwa ni kukauka kwa mabwawa ya kuzalisha nishati hiyo.
Hivyo, tunaamini kuwa ziara ya Waziri Makamba inakwenda kumaliza kabisa ama kupunguza tatizo la kukatika umeme ovyo nchini.
Watanzania wanaimani na serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, sio vyema kumwangusha kwa kuwapo kwa tatizo la kukatika kwa umeme, ni muhimu kuona uhalisia kwamba umeme haukatiki na kama ikitokea umekatika wananchi waelezwe tatizo.
Tunaamini ziara ya Waziri Makamba inakwenda kuzaa matunda ya kutokomeza tatizo hilo, kwa sababu limekuwapo kila mwaka hasa wakati wa ukame kwa sababu siku 21 si haba.
Kwenye ziara hiyo, imetajwa mikoa mingi ikiwamo Songwe na Mbeya, ni wakati mwafaka kwa Waziri Makamba kwenda kuangalia chanzo cha nishati jadidifu (umeme wa joto ardhi) ambalo lipo kwa wingi mikoa ya Songwe, Mbeya na kwingine.
Majirani zetu Kenya wanazalisha umeme wa joto ardhi kwenye bonde la ufa ambalo limepita pia Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara nchini ambako kuna majimoto ambalo halijatumiwa vyema.
Kwa mujibu wa Wikipedia, inakadiriwa Bonde la Ufa lina uwezo wa kuzalisha megawati 2,000 iligundulika mwaka 1956 eneo la Olkariana uzalishaji ulianza mwaka 1981 zilizalishwa megawati 15 na sasa wanazalisha MW 256 na wanatarajia kufikia 576 ndani ya miaka 20 ijayo.
Jitihada ni kubwa na sasa utafiti umeshafanyika, lakini kasi iongezeke ili nchi iwe na vyanzo tofauti tofauti vya umeme kuondokana na kutegemea umeme wa maji pekee, ambao haijaonyesha mafanikio kwa miaka mingi hasa kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi.









