Timu zienzi majina yetu

11Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Timu zienzi majina yetu

MPIRA wa miguu ni mchezo maarufu, si Tanzania pekee bali dunia nzima. Umaarufu wa Ligi Kuu ya England (EPL) umevuka mipaka ya nchi hiyo, ambao ni faida kwa klabu kubwa za England.

Ukizungumzia mechi za televisheni, ni zile za EPL ndizo zinazoongoza nchini kwa mashabiki kufurika katika maeneo mbalimbali kila mechi zinapochezwa, tena nyingine hushuhudiwa usiku mkubwa.

Klabu kubwa za England zimekuwa zikitumia vizuri wingi huo washabiki hasa katika bara za Asia kwa kufanya ziara za maandalizi ya msimu mpya.

Ziara hizo mbali ya kuwa sehemu ya maandalizi ya timu, lakini hutumika kwa kuuza vifaa mbalimbali vya timu kama jezi.

Kutengeneza wigo wa washabiki si kitu kidogo wala cha mzaha. Ukifuatilia historia ya klabu nyingine za England na sehemu nyingine duniani utabaini kuwa zimetumia muda mrefu kutengeneza washabiki kutokana na ukweli kuwa kuna klabu nyingi huko kwao.

Nyingi ya klabu hizo zimeasisiwa karibu au zaidi ya karne moja iliyopita, na sasa zimekuwa taasisi kubwa, tena si tu katika kucheza mpira wa miguu, bali heshima ambayo zimejijengea.

Hapa Tanzania tuna klabu kongwe na zenye wafuasi wengi za Simba na Yanga. Klabu hizi za Dar es Salaam zimeanzishwa zaidi ya miaka 80 iliyopita. Kimsingi klabu hizi ni za aina yake, kwani zina hazina ya washabiki.

Wakati klabu nyingine zinafikiria na kujipanga kwa ajili ya kutengeneza wigo wa washabiki, zenyewe zina wafuasi wa kutosha. Wafuasi ni zaidi ya washabiki, kwani hao wameshaamini katika Yanga na Simba. Huwezi kuwabadili kutoka kushabikia timu hizo.

Hawa iwe ni wafuasi, washabiki au wanachama tu wao hawazitazami klabu zao katika mwelekeo mwingine zaidi ya ushindi. Kwao maendeleo katika klabu ni ushindi tu, iwe kiwango cha mchezo unaochezwa ni mbovu lakini kinatoa matokeo wao hilo si tatizo.

Hii ndiyo changamoto kwa klabu zetu hizi mbili na nyingine. Kimsingi kama Simba na Yanga zimejitengenezea zaidi wafuasi kutokana na sababu za kihistoria tu.

Tunasema historia kwa sababu sasa hivi ukikutana na mfuasi wa Yanga au Simba mwenye umri wa miaka 50 hawezi kukupa sababu yenye mantiki ni kwa nini alifikia kuipenda klabu anayoishabikia.

Kama hali ni hivyo kwa hao ambao wameishi duniani kwa nusu karne itakuwaje kwa vijana wenye miaka 20 au 30? Hao ndiyo kamwe hawawezi kukueleza kinagaubaga ni kwa vipi waliangukia kushabikia Simba au Yanga.

Mafanikio ambayo klabu za England kama Arsenal, Liverpool na Manchester United zimepata uwanjani na kujikusanyia washabiki sehemu mbalimbali duniani haikuwa kazi ya miaka kumi tu.

Au klabu kama Barcelona na Real Madrid za Hispania, na AC Milan au Inter Milan za Italia washabiki wake hawakuumbwa kutoka hewani.

Ni klabu ambazo mizizi yake vilevile ndiyo msingi wa washabiki, ingawa zina washabiki hadi nchini Tanzania.

Lakini leo ukifuatilia kwa karibu utabaini kuwa si washabiki tu, bali Tanzania kuna timu zinaitwa Manchester United, Arsenal, Liverpool, Barcelona, West Ham, Real Madrid, Real Zaragoza, AC Milan, Inter Milan, Panama na nyingine, na zinacheza ligi zetu.

Kimsingi ili timu iweze kucheza ligi yoyote rasmi- ile inayotambuliwa na chama cha mpira wa miguu cha wilaya, chama cha mpira wa miguu cha mkoa au Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni lazima iwe imesajiliwa.

Hapa hatuzungumzii mashindano ya Kombe la Mbuzi, Kombe la Mbunge na mengine ya aina hiyo. Tunazungumzia ligi ya mpira wa miguu ambayo inachezwa kwa mujibu wa kanuni zilizoandaliwa na wasimamizi.

Umaarufu wa klabu hizo za nje umewapumbaza watu wengi wanaoanzisha klabu nchini. Ndiyo maana ni rahisi kwao kwenda kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo katika maeneo yao na kusajili klabu inaitwa Manchester United. Msajili naye kwa makusudi au kutojua akaisajili hivyo hivyo.

Ni vizuri wasajili wetu na hata waanzilishi wa Manchester United ya Tanzania wakafahamu kwa nini hiyo ya England imeitwa Manchester United, ile ya Hispania inaitwa Barcelona au ile ya Italia inaitwa AC Milan.

Jambo la kwanza ambalo tunatakiwa kufahamu ni kuwa majina kama Manchester, Barcelona, Madrid, Milan, Tottenham, Blackburn ni miji au vitongoji katika nchi hizo za Uingereza, Hispania na Italia.

Ajax Amsterdam ni klabu ya nchini Uholanzi. Lakini leo inaweza ikawepo Ajax Dar es Salaam kama tu kutakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Ajax Amsterdam.

Hivyo, klabu hizo mara tu zilipoanzishwa zilianza kuwa na washabiki katika maeneo yao kwa sababu majina tu yanawakilisha miji husika. Mbeya City au Musoma Shooting zina uhalali wa kujitengenezea washabiki katika miji hiyo kwa sababu hiyo niliyoitaja hapo juu.

Hapa kwetu tuna timu ambazo hazioni tabu kucheza mashindano zikiwa zimevaa jezi za Chelsea, Manchester City au Barcelona. Ni ulevi tu wa kutojua au kutaka kujua kwa nini Chelsea imefika hapo ilipofika.

Umefika wakati kwa Ofisi ya Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini wakati wa kusajili klabu kuangalia zaidi ya malengo na madhumuni katika katiba za klabu zinazoomba kusajiliwa. Maana ya majina ya klabu husika nayo iangaliwe.