Pamoja na jitihada hizo, bado lengo la serikali ni kuwa na asilimia 70 ya Watanzania waliochanjwa halijafikiwa tangu uzinduzi wa kampeni ya chanjo iliyofanyika mwishoni mwa Julai mwaka jana.
Inaelezwa walau hatua ambayo Tanzania imefikia sasa inatoa moyo, ingawa bado elimu zaidi inatakiwa kuendelea kutolewa kwa raia wajue umuhimu wa chanjo na hata wajitokeze kwa wingi kuchanjwa.
Ni suala hilo la elimu na uhamasishaji wa chanjo, vimemsukuma Katibu Mkuu Msaidizi na Mratibu Mkuu wa Kimataifa wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) , Ted Chaiban, kuja nchini na juzi alikuwa katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam kuhamasisha chanjo.
Hapo akapongeza jinsi nchi inavyopambana na ugonjwa huo, hasa kutoka kiwango cha asilimia sita hadi kufikia asilimia 12.4 ya waliochanjwa.
Ninadhani pongezi hizo zingefaa kuwa chachu kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO-19, kwani hali inaonyesha kuwa watu bado wanasuasua.
Kwanini ziwe chachu? Ni kwa sababu Watanzania wako nyuma kufikia ile asilimia 70 iliyokusudiwa na serikali, pia ugonjwa huo hatari unaendelea kuenea katika maeneo mbalimbali duniani.
Hivyo, suala la kuendelea kuchukua tahadhari na kupata huduma ya chanjo ni jambo la msingi, ambalo kila Mtanzania anatakiwa kuchukulia kwa uzito zaidi, ili kuhakikisha afya yake inakuwa salama.
Kama nilivyoeleza kuwa lengo la serikali ni kuwa na asilimia 70 ya Watanzania waliochanja, ili kuwa na walau na kinga sahihi. Naamini kutofikia asilimia hiyo kumemfanya mgeni huyo kutoka WHO kuja kusaidia hamasa na amana kubwa kwetu sote.
Ikumbukwe, chanjo ilizinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa Julai mwaka jana na sasa tunaelekea kutimiza mwaka mmoja tangu huduma hiyo ianze kutolewa nchini.
Hapo kuna haja ya asilimia 12.4 ya waliochanjwa. Nadhani ipo haja kwa kila Mtanzania kutafakari na kisha kuchukua hatua zitakazomwezesha kujikinga na UVIKO-19, hasa kwa kuachana na elimu potofu.
Tangu ugonjwa huo nchini, kumekuwapo elimu nyingi zinazohusu afya zinazotolewa, hata na watu wasio na utaalamu wa afya, hali ambayo inawezekana wamechangia kukwamisha chanjo.
Lakini, yapo maeneo yaliyopiga hatua katika utoaji chanjo, mfano hai ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke (DMO) Dk. Irene Haule, anayesema amefanikiwa kuvuka kiwango cha utoaji huduma ya chanjo elekezi, kutoka watu 3,500 hadi kufikia idadi ya wapata huduma 7,000 kwa siku.
Sababu kubwa ya kuvuka lengo, inaelezwa inatokana na mikakati waliojiwekea ikiwamo ya utoaji elimu kwa jamii, ambayo kwa sasa wana mabanda matano ndani ya viwanja vya Sabasaba.
Utaratibu mwingine, ni kwamba wanatoa huduma nyumba kwa nyumba na kwenye vituo walivyotengwa na huduma nyingine, huku chanjo ya UVIKO-19 ikipewa kipaumbele kuhakikisha wananchi wanakuwa salama kupitia kinga hiyo.
Mikakati ya utoaji huduma ya chanjo ya UVIKO-19 kwa njia kama elimu, imesaidia kuongeza idadi ya wanaopata huduma hiyo, ikiwa ni jitihada za kiserikali kuwalinda wananchi wake dhidi ya magonjwa.
Hatua zinazofanywa na Temeke nazisifu ni nzuri na ninaamini zikiigwa na maeneo mengine ya Dar es Salaam na hata nchi nzima kwa ujumla, lengo la serikali la kutaka asilimia 70 kupata huduma hiyo zitawezekana.
Jambo la kwanza ni kutambua kuwa ugonjwa huo upo, kisha kuchukuliwa hatua zinazoelekezwa na wataalamu wa afya na kuweka pembeni elimu ya mitaani, ambayo kimsingi inapotosha.
Iwapo kila mmoja wetu atajua na kutekeleza wajibu wake dhidi ya UVIKO-19, ni wazi asilimia ya waliochanjwa inaweza kuongezeka hadi kufikia lengo au kulivuka na hivyo kujiweka katika mazingira salama zaidi.