Ukomavu wa kisiasa unaweza kumaliza migogoro ya vyama

06Jul 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ukomavu wa kisiasa unaweza kumaliza migogoro ya vyama

NDANI ya vyama vya siasa kumekuwapo na mvutano unaochangiwa na sababu mbalimbali, ikiwamo kutofautiana hoja, mawazo, mitazamo na maoni miongoni mwa wanachama au na viongozi wao.

Mazingira hayo husababisha wengine kuhama vyama, kufukuzwa au kuendelea kubaki huku wakisuguana na kuvifanya visipige hatua mbele kutokana na migogoro.Wapo ambao hukutwa na hatia na kupewa adhabu kama kufukuzwa au kutakiwa kuomba radhi ili maisha yaendelee, lakini badala yake wanabaki kuendeleza migogoro ambayo haina afya kwa taasisi zao.Kwanza migongano au migogoro katika vyama haliepukiki, kwa sababu vinakutanisha watu tofauti na wenye mtazamo inayotofautiana, hivyo jambo la muhimu ni ukomavu wa kisiasa.Ninaamini kukaa na kujadiliana mambo yao na kupata muafaka suala ambalo linaonekana haliendi sawa ni muhimu kwa ustawi wa chama cha siasa.Hivyo, hali ikishafikia kumfuta mtu uanachama, kama ana mapenzi na chama, kinachofuata ni kuomba radhi ili arudishwe kundini ili kuendelea kukitumikia badala ya kukumbatia migogoro inayoweza kusambaratisha chama.Kimsingi, ni wazi kwamba kwenye suala la kuomba radhi, wapo baadhi ambao wamejaliwa busara na hufikia kuomba hata kama hawajafanya kosa, lengo likiwa ni kuepusha malumbano yasiyo na msingi.Hivyo, ni vyena kama wanasiasa wangekuwa na utamaduni huo kwa kutafakari na kisha kuchukua hatua ambazo zitasaidia kuzima migogoro ndani ya vyama vyao ambayo inaweza kusababisha wananchi wasiviamini.Ninaamini kwamba kuomba radhi ni hatua moja na kusamehewa ni jambo muhimu, hasa kwa kutambua kuwa hakuna binadamu aliyekamilika, hivyo kukaa na kumaliza tofauti ni boraChama ni wanachama na bila wanachama hakuna chama, hivyo kuwapo kwa migogoro na kisha kufukuzana, sidhani kama ni jambo jema, na si vizuri wanachama kufurahia pale mwenzao anapofukuzwa.Ndiyo, inawezekana kada akawa amekwenda kinyume na taratibu za chama na kufutiwa uanachama, ni sawa, lakini ingefaa hatua hiyo ikachukuliwa kwa umakini wa hali ya juu, ili kuepusha migogoro.Ni kweli kwamba, migogoro ni sehemu ya maisha ya kila siku ya mwanadamu, kwani hutokea kwa sababu kila mmoja ana mahitaji, na kwa bahati mbaya rasilimali za kutimiza mahitaji hayo hazitoshi.Licha ya kutotosha kwa rasilimali, lakini namna ya kufikia mahitaji hayo hakuingiliani au hakufungamani kati ya mtu na mtu au kundi na kundi. Kutoingiliana ama kutofungamana kwa namna ya kuyafikia mahitaji husababisha kutokea kwa migogoro.Lakini baadhi ya migogoro ni midogo inaweza kusuluhishwa, mingine ni mikubwa kiasi kwamba huacha madhara makubwa yasiyoweza kurekebishwa au huchukua muda mrefu kupona.Wadau wa siasa walishawahi kuelezea kuwa vyanzo vya migogoro ya ndani ya vyama hivyo, ni upendeleo kwa baadhi ya wanachama na kuwatenga wengine, kukosekana kwa mgawanyo sawa wa rasilimali ambapo kiongozi wa chama hupata mgao mkubwa kuliko wengine.Kwamba, kukosekana kwa mgawanyo mzuri wa rasilimali na mamlaka kuegemea upande wa juu tu husababisha tatizo la kiuongozi ambalo huzaa migogoro inayoweza kusambaratisha vyama.Kukosa ajenda za msingi kwa vyama vya siasa ambapo huweza kusababisha kutokea kwa migogoro, hasa panapotokea baadhi ya wanachama kutaka ajenda maalumu ambayo chama itakibeba kama msingi wa kujitofautisha na vyama vingine na kuandaa sera mbadala ya kuiuza kwa umma.Vilevile kuna suala la imani, itikadi, falsafa na uvumilivu dhidi ya mabadiliko, ambapo vinasababisha wale ambao hawataki kubadilika kujikuta wakizua migogoro kati yao na viongozi wao bila sababu za msingi.Lakini pamoja na yote hayo, ukomavu wa kisiasa ni nguzo muhimu ndani ya vyama ambayo viongozi wanaweza kuionyesha na kuitumia kumaliza migogoro katika vyama vyao.