Baa nyingi mijini hasa kwenye majiji kunafunguliwa baa kila wakati na wateja wanajaa. Mathalani, jijini Dar es Salaam, zama hizi licha ya watu kudai kuwa maisha ni magumu lakini yaelekea si magumu kwenye pombe. Kila mahali baa zimejaa.
Kinachoshangaza na wengi kujiuliza ni hiki inakuwaje baa zinajaa kiasi hiki hasa mpya ambazo ni kama zimesambaa kila kwenye barabara kuu au zile za mitaani zinazotumiwa na watu wengi.
Madai ni kwamba hao wanaoitwa wateja wengi wanachofuata ni wasichana au mabinti ambao wanadaiwa kuwa hutumiwa kuvuta wateja na hata kukuza mauzo ya vinywaji na vyakula katika baa nyingi za mijini.
Yapo madai kuwa wasichana hao hubadilishwa kila baada ya kipindi fulani inaweza kuwa miezi mitatu au sita ama mmiliki wa baa au meneja anavyopenda.
Baadhi ya mabinti hao wanadai kuwa hunyanyaswa wakati wa kazi na kuna baadhi ya wamiliki hawawalipi mishahara badala yake huwalazimisha kuwa na uhusiano na wateja na kwa kifupi huwataka kujiuza kwa wateja.
Inaonekana kuwa pengine ni mkakati wa baadhi ya wafanyabiashara au mameneja wa baa kuwatumia wasichana hao ili kuuza mauzo zaidi au kama moja ya mbinu ya kukuza biashara zao.
Wasichana hao wa baa huvalishwa mavazi mafupi kuonyesha miili yao lakini hutumikishwa kufanyakazi muda wote na uzuri wao au sura nzuri na maumbile yao ndiyo kinachogeuzwa mtaji kwa wauza pombe.
Lakini jambo jingine ni madai ya wasichana hao kuzungushwa kwenye baa mbalimbali tena huko nako wengi hawana ajira.
Wanadai lengo la kuwazungusha kwa kuwahamisha kutoka kwenye baa mbalimbali zilizoko miji tofauti ili kuwahamasisha wateja ambao wengi ni wanaume kunywa zaidi huku wamiliki wakijinufaisha zaidi.
Sehemu ya kazi wanatakiwa kuwa na urafiki wa karibu na wateja, anasema mmoja wa wasichana wa baa: "Mwajiri wetu anasema kabisa ikiwa hutaki kumbembeleza mteja, unapaswa kutafuta kazi nyingine."
Baadhi ya wasichana wanalazimishwa kuingia kwenye ukahaba katika umri mdogo tena wakiwa ni idadi kubwa ya mabinti halafu kwa wakati mmoja.
Ni vyema taasisi kama za ustawi wa jamii, polisi na askari wa ulinzi shirikishi wakafuatilia suala hilo ili kuujua ukweli ili kuwaokoa wasichana hao na kazi ya kutumia kukuza mauzo ya pombe.
Iwapo kuna Chama cha Wafanyakazi wa Mahotelini, Mashambani na Majumbani (CHODAWU) hili linapaswa kuwa jukumu lake la msingi la kutetea na kufuatilia wanachama wake.
Wasichana hawa wanasema wamiliki wanawanyonya na kuwalazimisha tutakutana na wanaume bila ridhaa yao ni udhalilishaji, lakini ni jambo wasilolipenda.
Inabidi utafiti ufanyike kwa sababu serikali inagharamia elimu inakuwaje wasichana hao wasiwe darasani badala yake wafanye kazi kwenye baa mijini?
Aidha ni wakati wa kuzingatia kuwa maradhi mengi yanaambukizwa kupitia ngono na hiyo ni njia mojawapo ya kuwaambukiza watoto hao wadogo magonjwa.
Baadhi ya maradhi yanaweza kuwa ni pamoja na UKIMWI, homa ya ini inayoambukizwa na virusi vya ‘hypatitis’ lakini pia hata maradhi ya saratani ya shingo ya kizazi yanayoambukizwa na Human papilloma virus (HPV), ambayo wakati mwingine husambaa kwa njia ya kujamiiana na watu wengi.
Licha ya serikali kupiga vita madanguro, vitendo kama hivyo kufanyika kwenye baa ni kama kuzigeuza kuwa nyumba za ukahaba ambazo sheria ya Tanzania haiziruhusu.
Suala la wafanyakazi wa baa kutolipwa mishahara nalo linatakiwa kufanyiwa uchunguzi na mamlaka za serikali kama halmashauri, manispaa na TRA kwa upande mwingine kwa kuwa eneo mojawapo linalotozwa ni kodi ya mshahara (pay as you earn) lakini pia kodi ya zuio ambayo kila malipo yanayofanyika hulipiwa kodi.
Ni vyema kuchukua tahadhari na kuokoa wasichana hawa ambao ni mama wa kizazi cha kesho.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








