Hongera Yanga, timu zijipange kusajili vizuri

04Jul 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongera Yanga, timu zijipange kusajili vizuri

ULIKUWA ni msimu wa kukumbukwa kwa wanachama na mashabiki wa Yanga. Wametwaa kila kitu. Ngao ya Jamii, Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la FA.

Kitu pekee walichopokonywa ni Kombe la Mapinduzi, ambalo lilichukuliwa na watani zao wa jadi Simba. Nao wamewanyang'anya mataji matatu, hayo niliyoyaweka mwanzo.

Kitu ambacho kilichowasaidia zaidi Yanga msimu huu ni usajili bora walioufanya kabla ya msimu kuanza. Walikuwa wakisajili huku baadhi ya watu wakiwadhihaki. Hawakujali, ligi ilipoanza ndipo mbivu na mbichi zilipojulikana.

Ikageuka kuwa moja ya timu tishio, licha ya makosa ya hapa na pale ya waamuzi, lakini ilikuwa ni timu ngumu sana na ambayo timu nyingi zilikuwa hazipendi kukutana nayo.

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule, ambaye timu yao haikufungwa mechi yoyote na Yanga msimu huu, badala yake kutoa sare mara mbili, alisema msingi mkubwa au nguvu ya Yanga ilikuwa ni kwenye kiungo.

Alisema Yanga ilizishinda timu nyingi msimu huu kwenye nafasi ya kiungo, hivyo yeye alikuwa anatengeneza mpango mkakati kwa wachezaji wake kutowapa nafasi viungo wa timu hiyo kuwa huru na mpira na kuamua wafanye wanavyotaka.

Ndiyo maana Yanga msimu huu haikupata ushindi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa timu mbili tu, Simba na Mbeya City kwa kupata sare mbili, lakini zilizobaki, ama imeshinda zote mbili, au mechi moja imepata pointi tatu na nyingine sare.

Msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara umemalizika rasmi kwa kushuhudia ligi ya aina yake. Ligi ilikuwa ngumu, lakini yenye maelezo.

Pamoja na ugumu wake haikuwa ngumu juu, yaani kwenye timu za kusaka ubingwa.

Yanga haikuwa na timu iliyoipa changamoto huko juu, badala yake ilionekana dhahiri kuwa inakwenda kutwaa ubingwa kirahisi.

Cha ajabu Simba ambayo msimu huu imepoteza mechi nyingi na haikuwa bora, nayo ni kama ilikuwa imejimilikisha nafasi ya pili mapema. Ilifikia wakati rekodi zilionyesha hata ikifungwa mechi zote zilizobaki, basi itamaliza ya pili tu.

Kwa ligi ambayo timu zingekuwa zinashindana kwenda juu, Simba msimu huu ilistahili kuwa wa tano wa sita.

Azam ndiyo kabisa ilikuwa haivutii. Siyo Azam ile tunayoijua. Ilifanana na timu zingine kama Mbeya Kwanza, Dodoma Jiji, Coastal na nyinginezo.

Msimu huu ligi ilionekana ngumu kwa sababu nyingi zilifanana uwezo, ukiondoa Yanga na Simba.

Ndiyo maana pilikapilika ilikuwa huku chini, timu zikisaka nafasi ya tatu na ya nne, pamoja na kubaki Ligi Kuu kuliko kusaka ubingwa.

Tunakwenda msimu mwingine wa 2022/23, ambayo kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), utaanza Agosti 17, mwaka huu.

Ni wakati sasa wa timu zote zilizo kwenye Ligi Kuu kufanya usajili wa maana ili kupambana kuusaka ubingwa zaidi na si kupigania kushuka daraja. Timu nyingi zilisaka ubingwa ndipo ligi itanoga zaidi.

Tayari Azam imeonekana haitaki mzaha, imeanza kushusha vifaa, ikileta Waivory Coast wawili, Tape Adinho na Kipre Junior, pamoja na Mnigeria, Issa Ndala.

Inaonekana tayari imeshajua ilipokosea, hivyo imeanza mapema kujipanga. Timu nyingine ni Simba. Nayo inakwenda kucheza Ligi ya Mabingwa. Ni timu inayotegemewa zaidi kwenye kuibeba Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa sababu imeshakuwa na uzoefu. Pia inahitaji mechi moja tu kuingia makundi tofauti na zingine.

Kwa jinsi ilivyo ni kwamba inahitaji marekebisho mkubwa zaidi kuliko timu zingine zote zinazokwenda kucheza michuano ya kimataifa.

Kuna timu zilizobaki Ligi Kuu na zile zilizopanda daraja. Zinatakiwa zitafute wachezaji bora na si bora wachezaji. Zitafute wachezaji watakaoziwezesha timu hizo kuleta ushindani mkubwa na wa kweli, si kusajili wachezaji wa bei rahisi, au waliocheza soka muda mrefu Ligi Kuu, lakini viwango vya kawaida.

Msimu ujao tunataka ligi yenye ushindani wa timu angalau tano kupambana kuusaka ubingwa.

Na hauwezi kutokea kama timu zisipofanya usajili makini na wachezaji wenye uwezo, kiu ya mafanikio, viwango na wapambanaji.