Wakizungumza katika mkutano uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la HakiElimu na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wanataaluma kutoka vyuo vikuu, walijadili na kubaini vikwazo mbalimbali vinavyotia shaka utekelezaji wake. Mjadala huo ulijielekeza kujadili Sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inavyoweza kuwaandaa watoto wa Tanzania kukabiliana na changamoto za karne ya 21. Baadhi ya wanataaluma kutoka vyuo vikuu mbalimbali, wanakubali kwamba, sera hiyo imezidi kuleta mjadala mpana katika kutatua matatizo ya elimu ikiwamo usawa na kuwandaa vijana kuingia katika ushindani wa soko la ajira. Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage anasema pamoja na serikali kutumia sera mpya, bado ubora wa elimu umekuwa ni changamoto ya muda mrefu na kwamba Serikali inatakiwa kuandaa mikakati itakayowezesha upatikanaji wa elimu bora katika ngazi zote. Sera hiyo kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo imeeleza muda wa mwanafunzi kupata elimu utakuwa miaka 14, badala ya 18 ya huko nyuma. Katika mfumo huo, mtoto atasoma mwaka mmoja katika shule ya awali, shule ya msingi miaka sita, sekondari miaka minne na chuo miaka mitatu. Katika sera za awali ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995, 1998 na ile ya elimu ya juu ya mwaka 1999, zilikuwa zikitambua elimu ya awali kuwa ni miaka miwili, msingi miaka saba, sekondari miaka sita na chuo miaka mitatu. Kalage, anasema njia pekee za kufanikisha suala hilo ni kuboresha shule za umma ambazo zinahudumia asilimia 94 ya watoto, kuweka miundombinu mizuri ya majengo, mifumo imara ya usimamizi, maabara na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. "Napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi za kuhakikisha kuwa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inapatikana. Hii ni baada ya kuwapo kilio cha muda mrefu kwa umma na wadau wa elimu kudai kufanyiwa marekebisho kwa sera za elimu za zamani. Hata hivyo, kuna changamoto zilizojitokeza na inahitajika kutatua,” anasema Kalage. Mkurugezi huyo anasema, suala la kuboresha elimu ni kutimia kwa malengo ya sera kuhakikisha kuwa, elimu inayotolewa nchini inakuwa bora na ya viwango vya ushindani. Katika tafiti nyingi anasema kwamba zinakubali kuwa elimu inayotolewa lazima iwe yenye ubora na kushauri zifanyike jitihada za kuboresha mazingira ya ufundishaji na kuwekeza katika ubora wa walimu ambao ndio msingi wa elimu yenyewe. Changamoto kubwa katika utekelezaji wa sera hiyo ni matumizi ya lugha mbili kwa wakati mmoja. Katika shule za msingi na sekondari lugha zinazokubalika ni Kiswahili na Kiingereza, ikielezwa kuwa ni lugha kuu za kufundishia na kujifunzia. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashiru Ally, anasema kikwazo cha lugha kitasababisha kutokea kwa mkanganyiko katika madarasa na kujenga matabaka kwa wanafunzi. Sera hiyo anasema kuwa haijafafanua ni jinsi gani walimu watatumia lugha hizo kwa wakati mmoja, jambo ambalo walimu watakuwa na sitofahamu katika ufundishaji. “Sera inatakiwa kuweka wazi hatua gani Kiswahili kitatumika na wapi itakuwa kwa Kiingereza, kueleza tu kwamba lugha zote zitatumika haitoshi na itajenga mkanganyiko,” anasema Ally. Anasema wakati shule za umma ambazo watoto wanaosoma ni wale wa hali ya chini wakiwa katika mshangao, wenzao wa shule binafsi wataendelea kupata elimu kwa lugha ya Kiingereza, hivyo kuendeleza kujenga madaraja. “Elimu itakuwa ya kubagua wale watoto wa wengi hawatapata elimu bora na kuambulia makombo, huku wenzao wa shule binafsi wakifurahia ubora wa elimu baada ya kutumia lugha moja ya Kiingereza,” anaongeza. Joviter Katabalo, kwa upande wake anasisitiza ili sera hiyo iweze kufanya kazi kama inavyotarajiwa, lazima kuwapo na usawa kati ya wanafunzi wanaosoma shule binafsi na serikali. Anasema shule nyingi za serikali hazina miundombinu ya kisasa inayoweza kuwaandaa wanafunzi kusoma vizuri, tofauti na wenzao wa shule binafsi. “Serikali inatakiwa kujikita katika kujenga na kukarabati majengo yake yalingane na sehemu ya kutolea elimu, itoe ushawishi wa kishindani kwa wanafunzi wenyewe kupenda kusoma na kutoa elimu kwa wazazi waone suala la elimu lipo mikononi mwao badala ya kila kitu kuiachia serikali,” anasema Dk. Katabalo. Prof. Suleman Sumra anakiri kwamba, tangu aingie katika sekta hiyo miaka 50 iliyopita, mfumo wa elimu umeparaganyika hivyo kunatakiwa nguvu kubwa kuufufua. Anasema elimu ya Tanzania haiwezi kutoa vijana watakaoingia katika ushindani wa ajira na wenzao wanchi za Kenya, Uganda na Rwanda. “Kama Rais Dk. John Magufuli, anataka kufufua uchumi wa viwanda lazima tupate vijana wenye ujuzi wa kufanya kazi, hii ni changamoto kubwa kwetu na lazima tutafute suluhisho la haraka,” anasisitiza Prof.Sumra. Washiriki karibu wote waliipongeza serikali kuja na mpango wa elimu bure, kwamba utasaidia kuwawezesha watoto wengi wa wananchi maskini kupata elimu ya msingi watakayoitumia kutafutia fursa mbalimbali. Akizungumza kwa niaba ya Mkurugezi wa Sera na Mipango Chonya Caristus, alisema Serikali imekamilisha mikakati yote ya sera hiyo na wanachosubiri ni maboresho ya mwisho. Sera hiyo anasema kuwa, itatumika vizuri kama mikakati hiyo itapitishwa na kukubaliwa katika ngazi zote ikiwamo wadau wa elimu.
Sera mpya ya elimu inavyokabiliwa na changamoto lukuki
09Feb 2016
Moshi Lusonzo
Dar es Salaam
Nipashe
Sera mpya ya elimu inavyokabiliwa na changamoto lukuki
WAKATI serikali imeanza kutumia rasmi sera mpya ya elimu, wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuelezea utekelezaji wake kwamba utakuwa mgumu baada ya kushindwa kutoa majibu ya kushuka kiwango cha elimu nchini.
Wanafunzi katika mazingira magumu










