Kwanza maana ya ‘Dawa ya moto ni moto” nikieleza kutokubaliana na usemi huo. Pili, kutoridhishwa na maneno anayotamkiwa mgonjwa wakati anapoagwa kuambiwa “haya ugua pole.” Tatu sikubaliani na watu wanaposherehekea Mwaka Mpya kusema “Nashukuru/tunashukuru kuuona Mwaka Mpya.” Nikauliza Mwaka Mpya huonekanaje? Una umbo gani, ukubwa gani na rangi yake ikoje? Mpaka nilipokuwa naandika makala haya, hakuna aliyenijibu. Labda wanaendelea kufanya utafiti. Kuhusu usemi “Dawa ya moto ni moto”, mwalimu na rafiki yangu, Mohamed Sharif wa Tanga anajibu: “Misemo ya methali inapoondoshwa mahali mwake hupoteza maana. Kama nimeelewa, itakuwa wahubiri msamaha ndipo ulipoona ‘dawa ya moto ni moto, akuchomae mchome,’ si mafunzo mema. 'Msamaha’ kuna vigezo na masharti vya kuzingatiwa, vinginevyo itakuwa ni kuacha, ambako kutaendeleza dhulma na ufisadi kama msemo: “kuliko na sheria hakuna dhulma.’ Hayo ndio maoni yangu juu ya ‘dawa ya moto ni moto.’ Ulivyochokoza, ni maoni yako; nimeyaheshimu.” Mohamed Sharif hakuishia hapo kwani ananisihi nimruhusu kutumia nukuu ifuatayo: “Wala jicho lako lisiwe na huruma: uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu (Kum.19:21).” Anaendelea: “Kwa vile ni maoni yako lazima yaheshimiwe. Kwa upande wangu kwa hii nukuu ya: “Kisasi ni changu mimi, na kulipa, wakati itakapoteleza miguu yao; maana siku ya msiba wao imekaribia, na mambo yatakayowapata yatafanya haraka ( Kum. 32:35),” haki itakuwa haikutendeka kama hazitajwi Kut. 21:23-25: “Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, kutekeleza kwa kutekeleza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko.” Anaendelea kunukuu: “Na atakayempiga mnyama hata akafa atalipa : uhai kwa uhai. Na mtu akimtia mwenziwe kilema, vilevile kama alivyofanya naye atafanyiwa vivyo: jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vilevile kama alivyomtia mtu kilema, naye atafanyiwa vivyo. Na mtu amwuwaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa (Law. 24:18-21).” Anamalizia kwa nukuu ifuatayo: “Wala jicho lako lisiwe na huruma: uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu (Kum. 19:21).” Hata hivyo napenda kumfahamisha Mohamed Sharif aliye mwalimu na rafiki yangu kuwa nukuu zake zapatikana kwenye Agano la Kale. Katika Agano Jipya kuhusu Yesu na Sheria, twasoma hivi: “Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza (Mt. 5:17).” Mwingine aliyesoma makala ninayoirejelea kuhusu ‘haya ugua pole’ alijibu hivi: “Mzee Maro salaam! Mimi ni Simon Mhina wa The Guardian. Natoa maoni yangu kuhusu suala la ‘ugua pole.’ Neno hili ni sahihi. Mwenye kulitoa anamaanisha kuwa mgonjwa apate wepesi katika kukabiliana na maumivu. “Sio kumtakia balaa la kuendelea kuugua. Mfano nikukute umevunjika mguu. Ni wazi huwezi pona siku hiyo. Utaugua muda mrefu. Hivyo kinachotakiwa hapo ni Mungu akupe wepesi katika kukabiliana na ugonjwa. Nadhani hii ndio maana waliyolenga wasemao ‘ugua pole.’” Katika gazeti la Februari 2, 2016 niliandika makala niliyoipa kichwa “Waandishi vinara wa kupotosha Kiswahili.” Aya ya kwanza niliandika: “Kila uchao (siku baada ya keshokutwa; mtondo) hukosi kusoma magazetini, hasa ya michezo, maneno mapya yanayozushwa na kukuzwa na waandishi.” Mohamed Sharif hakubaliani na maana ya “kila uchao” kama nilivyolitolea ufafanuzi kwa kunukuu Kamusi la Kiswahili Fasaha (Baraza la Kiswahili la Zanzibar) ukurasa wa 413. Yeye anajibu hivi: “Wanasema 1. Jua lachwa na mipango haijakamilika.” 2. “Wakumbuka shuka kumekucha.” Hivyo ‘kwachwa’ na ‘kucha’ kila siku. Dhahiri ya ‘kila uchao’ ni kila siku na si baada ya ‘kesho kutwa.’ Katika gazeti la siku hiyo nilieleza masikitiko yangu kuhusu waandishi wanaotumia maneno ya Kiingereza kwenye magazeti ya Kiswahili nikisema ni ulimbukeni. Mohamed Sharif anajibu: “Kuchanganya Kiswahili na Kiingereza wasanii wa Bongo muvi wanasema ‘Kiswahili hakina mvuto’ ndio maana pia hutoa majina kwa Kiingereza!” Ni yale yale ya ‘mkataa kwao ni mtumwa.’ Methali: Chako ni chako, cha mwenzio si chako. marobarnabas@yahoo.com 0715/0784 33 40 96
Uchokozi umeleta majibu
09Feb 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Uchokozi umeleta majibu
TOLEO la gazeti hili Januari 26, 2016 niliandika makala niliyoipa kichwa “Nawachokoza magwiji wa Kiswahili” nikiuliza maswali matatu.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








