Wasomi wana nafasi katika jamii?

09Feb 2016
Charles Kayoka
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Wasomi wana nafasi katika jamii?

HIVI karibuni katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Whatsapp! Kulikuwa na video ya uapishwaji wa madiwani katika halmashauri moja ilikuwa ikimuonyesha diwani mmoja akisoma kwa mashaka wakati akiweka kiapo chake.

Ilikuwa ni kichekesho,lakininiliona ni jambo linaloakisi ainisho la uongozi katika jamii na hawa wapiga kura wetu, kiongozi sio lazima uwe na elimu, ukijua kuupiga mdomo vizuri basi, mambo yatakwenda.Na hili liko katika ngazi zote za uongozi katika vyama na serikali. Watu ambao hawana uwezo wa kutosha kielimu na kimaarifa ndio wanaopigiwa upatu kuwa, viongozi kama tulivyoona kwenye video hiyo mtandaoni.Lakini kila siku tunaambiwa, wasomi toeni mchango wenu katika maendeleo. Hivi lipi linalowezesha wasomi kutoa mchango wao katika jamii!Uwezo wa wasomi kutoa mchango huanza na uwezeshwaji. Je, mfumo wa elimu na kujifunza unalenga katika kumfanya msomi kutoa mchango. Msomi anatakiwa kuwa mwenye fikra zilizokomaa na zenye ubunifu na kufikiri kwa uyakinifu.Na hilo halianzi kwa bahati nzuri, bali kwa namna anavyosomeshwa na jinsi mtaala ulivyosukwa.Kama mfumo wa usomi ni ule wa kukariri na kulazimishwa kukubali kile tu kinachoonekana kinafaa kwa mwalimu na sio kwa pande zote. Mfumo wa elimu yetu, kwa sababu mbalimbali, ni mfumo wa kuwashindilia wanafunzi kichwani na sio cha kuwawezesha wanafunzi kuwa wachambuzi, watafiti, wabunifu, na wenye kuuliza maswali.Mwanafunzi wa hivi anapohitimu anakuwa amejengewa uwezo wa kufikiri mwenyewe na kuwa mtatuzi wa matatizo.Na ndipo tujiulize, hawa wanafunzi wanaosomeshwa kwa gharama kubwa na serikali wanapohitimu wanakuwa wamejengewa uwezo huo?Marekani na nchi nyingi za Ulaya pamoja na mambo mengine, elimu yao inasisitizia sana uwezo wa mawasiliano na uwezo wa kutafakari kwa uyakinifu na kuuliza maswali- critical thinking.Tuanzie hapa!Lakini msomi maana yake nini? Msomi ni mtu aliyebobea katika taaluma fulani, na kuwa wakati wote anaitumia elimu yake na ubobezi wake kusaidia wengine, kufanya ugunduzi, kufanya tafiti, kusoma ili kujiongezea maarifa, na kuandika, na kuwa mtu asiyetosheka na lile analolifahamu na huwa hakubaliani na kitu kwa sababu tu kimezungumzwa na mtu mkubwa.Kama mtu amehitimu ngazi ya juu ya elimu halafu hawezi kuonyesha moja ya sifa hizi basi huyo sio msomi.Na utakuwa na wanafunzi au unaowaita wasomi wengi waliohitimu elimu ya juu lakini uwezo wao katika haya niliyoyataja ni mdogo,basi usomi unakuwa jina tu, sio hulka. Mtu anakuwa msomi kwa kuonyesha vitabia vinavyofanana na msomi, kwa maana halisi ya msomi!Lakini msomi aweze kutoa mchango lazima aheshimiwe! Katika nchi za Afrika Ikulu, wizara za serikali, kila idara, kuna wataalamu wengi waliobobea katika fani zao.Na waliajiriwa kwa ajili ya kutoa msaada kwa taifa lao. Lakini uliza kama wanatumika na kama ushauri wao unakubalika.Wanasiasa ndio walioshika mpini na ndio wanaoamua nini kifanyike kwa utashi wa kisiasa, kwa maslahi ya makundi, watu binafsi au chama.Unapoona kuwa raisi au waziri amejitajirisha kuliko kiasi kinachotegemewa ujue nafasi ya wasomi ilitupiliwa mbali.Hawezi kushauri kitu kikaeleweka kwa sababu mwanasiasa huyu aliyejitajirisha kupindukia hawezi kukubali ushauri utakaomzuia kuendelea kuwa tajiri, au kumzuia kuendelea kutawala.Katika mazingira kama haya, msomi ataamua kuwa kimya na yeye kufuata mkondo.Wasomi wanahitaji nyenzo za kuwasaidia kufanya utafiti; wanahitaji kusikilizwa wakitoa maoni yao, na yafanyiwe kazi.Msomi hawezi kujiona wa maana kama anapotoa ushauri wake kitaaluma, wanasiasa wanaona kuwa ni sawa na kelele za mlango hazimzuii mwenye usingizi kulala. Kuwa maslahi ya kisiasa ni muhimu kuliko ya kitaifa.Mchango wa wasomi hautawezaonekana kama hakuna fursa za ajira na kujiajiri na kama fursa hizo zinakwenda kwa upendeleo.Kwa sababu upendeleo huingiza kwenye mfumo watu wa ovyo, na matokeo yake ni wasomi kukosa nafasi ya kujionyesha na kuonyesha uwezo wao. Kama tunataka wasomi wawe wa manufaa basi tuweke mazingira rafiki.