TFF iwafikishe mahakamani wapangaji matokeo ya soka

08Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TFF iwafikishe mahakamani wapangaji matokeo ya soka

DONDOO MUHIMU:
Kama kweli TFF imedhamiria kukomesha kadhia ya rushwa na upangaji matokeo ya soka nchini, ninafikiri kuna haja shirikisho hilo kuwafungia maisha na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria wale wote wanaobainika kujihusisha na kadhia hiyo kama ambavyo Kanuni za Ligi toleo la 2015

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) lilitoa onyo kwa viongozi wa klabu, wachezaji, waamuzi na wasimamizi wa michezo ya soka nchini wanaojihusisha na vitendo ya rushwa na upangaji matokeo. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kisha kuchapishwa kwenye mtandao rasmi wa TFF, shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini liliwataka wanachama wak kutojihusisha na upangaji wa matokeo (Match fixing) katika michezo inayoendelea sasa katika ligi za ngazi mbalimbali za nchini. Taarifa hiyo ilifafanua kuwa TFF imejipanga na inasimamia vizuri michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Daraja la Kwanza (FDL), Daraja la Pili (SDL) na Kombe la FA inayoendelea na yoyote atakayebainika kujihusisha na mchezo huo wa upangaji matokeo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake. “Katika michezo yote inayoendelea, TFF ina maofisa wake wanaofuatilia kwa ukaribu michezo hiyo, hivyo endapo kiongozi, mchezaji, msimamizi au mwamuzi atabainika kujihusisha na upangaji wa matokeo, hatua kali zitachukuliwa,” sehemu ya taarifa hiyo ilisomeka. “TFF inawaomba viongozi, wachezaji, wasimamizi wa michezo na waamuzi kutojihusisha na mchezo huo wa upangaji wa matokeo kwani kufanya hivyo ni kukiuka katiba, sheria na kanuni zinaongoza mpira wa miguu nchini. ” Binafsi ninalipongeza shirikisho hilo kwa kuwakumbusha wanachama wake na wadau wa soka nchini juu ya umuhimu wa kutojihusisha na kadhia hiyo ambayo imekuwa ikiligharimu taifa kimaendeleo. Ni jambo la kupongezwa pia kuona shirikisho hilo linatuma maofisa wake kwenye mechi za ligi za ngazi zote kuhakikisha hakuna matokeo yanayoandaliwa nje ya uwanja. Hata hivyo, ninafikiri ipo haja TFF kuanza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria waleo wote wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na upangaji matokeo ya soka nchini kwa manufaa ya taifa. TFF imekuwa ikiwaonya mara kwa mara wanachama wake juu ya rushwa na upangaji matokeo, lakini bado inaonekana haijawa mstari wa mbele kupambana ipasavyo na kadhia hiyo. Wakati iikitoa onyo mwishoni mwa wiki, kuna taarifa zilizofikishwa kwenye meza za shirikisho hilo na mmoja wa marefa wa VPL aliyetishiwa kifo na mmoja wa viongozi wa timu za timu za Ligi Kuu. Si hilo tu, TFF pia imeshindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nsa Job ambaye mwaka juzi alihojiwa na kituo cha redio cha Jiji la Dar es Salaam na kukiri kupewa fedha na mmoja wa timu kubwa ili asiifunge na kuirahisishia kupata matokeo mazuri dhidi ya timu yake. Kama kweli TFF imedhamiria kukomesha kadhia ya rushwa na upangaji matokeo ya soka nchini, ninafikiri kuna haja shirikisho hilo kuwafungia maisha na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria wale wote wanaobainika kujihusisha na kadhia hiyo kama Kanuni za Ligi toleo la 2015 zinavyoelekeza.