Timu hizo zitarudiana wikendi ijayo na mshindi wa jumla atafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za U-17 zitakazofanyika baadaye mwaka huu huko India.
Serengeti Girls ni moja kati ya timu sita zilizofika hatua ya mwisho ya kusaka wawakilishi watatu kutoka Afrika watakaofuzu fainali hizo, timu nyingine zilizofika hatua hiyo ni Ethiopia ambayo yenyewe itacheza dhidi ya Nigeria wakati Ghana watapambana na Waarabu wa Morocco.
Hadi kufikia hatua hii, inaonyesha Serengeti Girls wamepambana vyema kusaka tiketi hiyo, hivyo wanastahili kuungwa mkono ili kufikia malengo na ndoto za Watanzania ambazo zimedumu kwa muda mrefu.
Licha ya kutokuwa na wadhamini, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepambana kuhakikisha Serengeti Girls inafanya mazoezi kwa mujibu wa programu zake zilizoandaliwa na Kocha Mkuu, Bakari Shime, wachezaji wanapata vifaa na chakula kwa wakati.
Ingawa timu hiyo ilisafiri jana, lakini bado inahitaji kupata huduma muhimu ili wachezaji wake waishi maisha yanayofanana na kazi ya kulitumikia taifa wanayoifanya.
Tunapenda kuwakumbusha wadau kujitokeza sasa kuwasaidia Serengeti Girls ili kurahisisha maandalizi yao na hatimaye kupata nafasi ambayo wanaililia kwa muda mrefu ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Wachezaji wanapopata maandalizi sahihi sasa, yatasaidia kufuzu lakini pia yatawafanya waende katika fainali hizo (endapo wataifunga Cameroon), wakiwa imara kila idara na si kusindikiza mataifa mengine.
Kesho watakuwa na dakika 90 za ugenini, halafu watarejea nyumbani kumalizia dakika kama hizo zilizobakia. Ni mechi ngumu lakini katika mchezo wa soka hakuna kisichowezekana.
Nipashe inawaomba wadau wa michezo nchini na Watanzania wote kuiombea dua njema timu hii ili itimize ndoto zake lakini pia impe heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.
Kufanya vizuri kwa timu hiyo kutaweka rekodi nyingine kwa nchi kwa sababu ikiwa chini ya Rais ambaye ni mwanamke, itakuwa pia imefuzu tiketi ya kushiriki fainali hizo zinazohusika soka la wanawake duniani.
Ushirikiano na umoja wa kweli unahitajika zaidi wakati huu ambapo Tanzania na TFF iliyoko chini ya Rais, Wallace Karia imepiga hatua, hivyo kama kuna tofauti zozote au mgawanyiko, usipewe nafasi kipindi hiki ambacho Serengeti Girls imekaribia kukata tiketi hiyo adimu na inayosubiriwa kwa muda mrefu.
Wote tunafahamu mpira wa miguu wa wanawake umebadilika na huu ni muda sahihi kwa makampuni na taasisi zenye uwezo kuisaidia timu hii ili ifanye vyema majukumu yake na hatimaye kutulika kiu cha Watanzania ambao hawajawahi kuona Tanzania inashiriki fainali zozote za dunia.
Tunaamini benchi la ufundi limefanya kazi yake vyema na wachezaji watakaopata nafasi ya kucheza mechi ya kesho na ile ya marudiano watajituma na hatimaye kuvuna matokeo chanya.
Nipashe inawakumbusha wachezaji wa Serengeti Girls kufahamu hatua ambayo wamefikia ni kubwa lakini wanatakiwa kuendelea kujituma kwa sababu kwa kufanya hivyo wanaweza kujifungulia milango kwa kuwavutia mawakala kuwasajili na hapo ikawa mwanzo wa kubadilisha maisha yao ya kisoka.
Mungu ibariki Serengeti Girls, Mungu ibariki Tanzania.










