Pia imeahidi kufanyia kazi mapitio ya sheria, sera na kanuni za biashara nchini, lengo likiwa ni kutengeneza sekta binafsi imara yenye kuchangia uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Ashatu Kijaju, alisema lengo la serikali ni kujenga mazingira wezeshi kwa kuondoa vikwazo vyote, ikiwamo kodi korofi ambazo zimedhoofisha uwekezaji na kusababisha sekta hiyo kushindwa kufikia malengo tarajiwa.
Kauli ya waziri inakuja wiki chache baada ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Godius Kahyarara, wakati wa uzinduzi wa filamu ya Royal Tour, kuwa alieleza katika majadiliano na wawekezaji mbalimbali walibaini sheria, sera na kanuni nyingi zimepitwa na wakati zinahitaji kubadilishwa.
Alisema nyingi ni za miaka ya 90 ambayo sio mbali na 60 na sasa tupo miaka ya 2022, jambo linaloonyesha kuna mambo hayakuwa yamejumuishwa kwa ajili ya kuwezesha wawekezaji kufanyabiashara nchini kwa kutoa ajira, kuchangia uchumi wa nchi na mtu binafsi.
Hii ni habari njema hasa kwa wakati huu ambao Tanzania inajijenga upya baada ya kupitia kipindi ambacho hakikuwa rafiki kikodi na kisiasa, hali iliyosababisha wengi kufunga biashara au kufungasha virago.
Baada ya kuingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan, aliwataka Uwekezaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufanyakazi ya ziada kuondoa vikwazo vyote, kuacha kuchukua fedha kwenye akaunti za watu, kukamata wafanyabiashara na kufunga biashara.
Hatua zinazochukuliwa sasa ni za kupongezwa kwa kuwa zinakwenda kuistawisha sekta binafsi ambayo duniani kote imekuwa ni kiini cha uchumi kwa kuwa ndiyo walipa kodi wakubwa na walioajiri wengi.
Duniani kote ajira nyingi zipo sekta binafsi, serikali hazifanyi biashara (kutegemea na sheria za nchi husika), inabaki kuwa mwezeshaji kwa kuhakikisha sera, sheria na kanuni ni zenye kukuza uchumi, ndicho kilichoonekana kwa sasa kwamba serikali imeliona tatizo kwa upande wao wanalirekebisha.
Kwa mujibu wa sheria zetu Rais ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Biashara Tanzania, ambalo hukutana kila mwaka kujadili mambo mbalimbali ya kukuza biashara na uchumi wa nchi.
Wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, alitumia muda mwingi kujenga sekta binafsi imara na mara zote alisisitiza kuwa ndiyo injini ya uchumi wa nchi, alihakikisha inakuwa na Watanzania wengi walio ajiriwa.
Tunaipongeza Serikali ya Rais Samia kwa kuona hili na sasa inainyanyua sekta hii ili kufikia lengo la ajira milioni nane miaka mitatu ijayo, maana yake nchi inakwenda kupata kodi za biashara, kampuni, taasisi na watu binafsi.
Lazima serikali itimize wajibu wake wa kujenga mazingira wezeshi sekta binafsi ikifanikiwa katika hilo itaongeza makusanyo ya kodi, ajira na kustawi kwa uchumi.
Pamoja na yote mazuri tunakumbusha serikali kuweka jicho lake wazi kila sekunde kuhakikisha uwekezaji unaofanyika nchini unanufaisha Watanzania.
Mathalani, uwekezaji kwenye maliasili muhimu kwa nchi yetu, kuzijua siasa za dunia (Geo Politics), ambazo wakati mwingine huziumiza nchi maskini, lazima watendaji serikalini wawe mbele ya wawekezaji wowote kwa maslahi mapama ya nchi.
Lazima tuwe na uwekezaji wenye uwajibikaji, tuone vyombo vya wafanyabiashara kama Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), vinasimama imara kutetea maslahi ya nchi pasipo kutanguliza maslahi binafsi.









