Wabunge hao walikuwa wakichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2022/23, ambayo kila aliyesimama alipaza sauti ya barabara yake kutojengwa au imekwama au ilikuwa ni ahadi ya mkuu wa nchi na imesahaulika.
Wabunge hao ni Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay ambaye aliomba kupiga sarakasi na kabla hajaruhusiwa na Spika Dk. Tulia Ackson, akawa ameshatekeleza alichokidhamiria.
Mwaka jana wakati wa bajeti hiyo hiyo tena aliongea kuhusu ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Mbulu Haydom, alimuomba Spika amruhusu aruke sarakasi kutoka alipokuwa amekaa kushoto mwa Spika hadi mbele, lakini alimsihi asifanye hivyo, alitii na kutoa mchango wake huku akitishia kushika Shilingi ya mshahara wa waziri ili bajeti isipite.
Mbunge mwingine ni Jerry Silaa wa Jimbo la Ukonga, alilia kwa uchungu kwa kuwa mkandarasi aliyepewa ujenzi wa mwendokasi ndiye aliyeboronga eneo jingine, jambo linaloumiza sana.
Kimsingi wabunge hawa hawajafanya hivi labda kutafuta sifa kwa umma au mamlaka, wametafuta namna yao ya kufikisha hisia zao ili kutaka uwajibikaji, huenda na wengine walio na ahadi za tangu enzi za Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, wangetamani kufanya jambo.
Ukifuatilia vikao vya Bunge wakati wa maswali na majibu mengi yamejikita kwenye afya, maji, barabara na elimu, hulalamika kwamba wameachwa nyuma kwenye ujenzi wa miundombinu muhimu.
Kutokana na kilio cha wabunge, Spika mara kadhaa ameitaka serikali kuja na mkakati wa kutatua kero hizo, kwamba waangalie mgawanyo wa bajeti hizo na hasa ahadi za viongozi ambazo ni za muda mrefu, huku akieleza kuna barabara lazima mbunge asimame kuuliza swali la nyongeza au achangie mjadala.
Kimsingi jitihada zimefanyika za kuunganisha mikoa, sasa imebaki kuunganisha wilaya na wilaya, pia kufika kwenye mitaa.
Ni lazima wanaoandaa bajeti kuangalia malalamiko ya wabunge, kwa kuwa keki ya taifa inapaswa kumfikia kila Mtanzania, isiwe kuna eneo fulani limetengewa fedha nyingi, lakini inapoibuka hoja ya mkandarasi kujenga chini ya kiwango isiachwe ikapotea hewani bali ifanyiwe kazi ili kuepuka hasara.
Mathalani, wananchi tunajiuliza barabara ya Mwenge Tegeta ya njia nne haina miaka 10 tangu imejengwa ila imekuwa ikifumuliwa na kuwekewa tabaka jipya la lami, yote hiyo ni fedha, lakini swali linakuwa ni kwanini inatengenezwa kwa viwango vya muda mfupi?
Uandaaji wa bajeti huanzia kwenye Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC), ambayo Diwani wa kata husika ndiye mwenyekiti, baadaye Baraza la Madiwani ambalo huongozwa na Mwenyekiti wa halmashauri, baadaye Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na kwenda Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na baadaye wizara.
Maana yake bajeti ni shirikishi na humo vipaumbele huchujwa kulingana na umuhimu wake kwa taifa, na kama kuna barabara imetoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) na kuwa chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ili kuwezesha utekelezaji.
Barabara nyingi zinazolalamikiwa ni zilizopo chini ya TANROADS, maana yake lazima kuja na mkakati wa kuhakikisha zinakamilika, kwa kuwa mbunge ana haki ya kufanya 'kituko' ndani ya muhimili wa kutumga sheria kwa kuwa ahadi yake ni ya miaka mingi, anaona fedha zimetengwa ghafla zimeenda kulipa madeni.










