Aidha, aliwataka kuhimiza wafanyabiashara kulipa kodi, ili kuongeza mapato ya serikali badala ya kudai maendeleo katika maeneo yao, kwa kuwa wana nafasi kubwa kuhakikisha wanasimamia na kuhimiza ulipaji kodi.
Alisema kuwa serikali haina muujiza wa kupata mapato bila kukusanya kodi kutoka kwa wananchi, na kwamba wabunge wana nafasi kubwa katika jambo hilo.
Pia, alisema wabunge wanaolalamika kwenye maeneo yao kuna wafanyabiashara wenye maduka makubwa na madogo wanaopaswa kuhamasishwa kulipa kodi ili fedha ipatikane.
Alichokisema Rais Samia ndicho kinaonekana siyo kwa wabunge tu bali hata viongozi wa serikali, kasumba ambayo imekuwa kawaida kwa wananchi kiasi cha kuamini kuwa matatizo yao yatatatuliwa na serikali pekee.
Ndiyo maana Rais anavyofanya ziara kwenye eneo fulani atapokelewa na mabango yenye orodha ya matatizo ya wananchi, mbunge naye akipewa nafasi kuzungumza jukwani ataorodhesha mengi anayotaka serikali iyafanyie kazi, akija mkuu wa wilaya, mkoa na wengine wataweka orodha kila mmoja akiomba fedha kutoka kapu kuu.
Kutokana na fikra hizo imepelekea kwamba wananchi wanashindwa kutatua changamoto za maeneo yao zinazoweza kutatuliwa kwa kuwa wanaisubiri serikali iwafanyie kwa kuwa wameaminishwa kuwa ndiyo wenye wajibu huo.
Mara kadhaa wabunge wamekuwa wakilalamika au wakati mwingine kuieleza serikali bila kutoa ushauri wa nini kifanyike, jambo ambalo linakuwa siyo msaada bali mtu kapaza sauti tu.
Ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake, kwamba wananchi wote tulipe kodi kwa usahihi na kuhamasisha wananchi kufanyakazi za kutatua changamoto za maeneo yao bila kusubiri serikali pekee.
Tunaona ni muhimu viongozi wakawajenga wananchi katika kufanya kazi za kijamii na siyo kusubiri kufanyiwa, enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wananchi walifanyakazi za kuchimba barabara, kujenga shule kwa kutoa nguvu kazi kuondoa dhana ya mali ya umma.
Zipo barabara zimejengwa kwa nguvu ya wananchi kutokana na viongozi kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha na kushiriki kwa vitendo kufanya kazi hizo, kwamba hawatasubiri kiongozi aje ndiyo waorodheshe matatizo.
Tunajua yapo maendeleo ambayo lazima yagharamiwe na serikali, lakini sasa tunapaswa kuhimiza moyo wa kujitolea, kwamba kusiwe na kukatisha tamaa kwamba kuna wanaopata fedha wakati wengine wanavuja jasho.
Awamu ya kwanza ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wananchi walikuwa wanaibua vipaumbele kwenye eneo lao, kisha inafadhiliwa kwa asilimia 80 huku nguvu kazi ikitolewa na wananchi kwa kufyatua tofali, kuchimba msingi, kuchimba barabara na nyingine.
Kwa mazingira yetu bado hatujafikia hatua ya serikali kufadhili kila mradi kutokana na fedha zilizoko, bali wadau wa maendeleo wa ndani na nje wanashiriki ambao ili kuwatambua ni lazima kuwahamasisha kuchangia shughuli za maendeleo.
Kwenye kila eneo kuna viongozi wa kuchaguliwa kuanzia mwenyekiti wa kitongoji/mtaa, kijiji, Diwani, Mbunge na Rais, wote hawa wanawakilisha wananchi katika kuendesha serikali.
Ikiwa kama mwenyekiti wa mtaa atapeleka malalamiko kwa aliyejuu yake, naye akayasogeza mbele maana yake ni kutengeneza mlolongo wa malalamiko bila kuona suluhisho.