Kuwapo kwa rushwa kuna chimbuko lake ambalo ni mmomonyoko wa maadili ambao huanzia katika ngazi ya familia hadi taifa, hivyo vita dhidi yake si ya serikali tu, bali kukuza maadili kunahitaji wadau wote na jamii kwa ujumla wake.
Tunasema hivyo kwani mmomonyoko huo ndio unaozaa maovu ikiwamo tatizo la rushwa ambalo sasa ni sugu katika maeneo mbalimbali kuanzia shuleni, sehemu za kazi na kwingine.
Kutokana na hali hiyo tunashauri wazazi, walezi na jamii kushiriki kikamilifu katika malezi bora yatakayosaidia watoto kuwa raia wema kuanzia nyumbani, shuleni ili hata wakiwa watu wazima, waendelee na kusimama katika maadili mema.
Pamoja na hilo, tunashauri pia kuwapo kwa mitaala kwa ajili ya somo la maadili, ambalo lingesaidia wanafunzi kuitambua rushwa na madhara yake wangali wadogo, kwani chanzo cha rushwa ni mmomonyoko wa maadili.
Tunaunga mkono juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa za kupambana na rushwa zikiwamo za kuanzisha klabu za wapinga rushwa shuleni ili wanafunzi wapate elimu ya madhara ya tatizo hilo.
Hatua hiyo ni nzuri kwa sababu inawaandaa wanafunzi kupinga rushwa wangali wadogo hata pale wanapokuwa watu wazima wanaendelea kupambana nayo kwa manufaa yao na ya taifa kwa ujumla.
Kwa mfano, wanafunzi wanatakiwa kujua rushwa ni nini, ikiwamo ya ngono, fedha na vitu vingine badala ya kuisikia tu bila kujua maana yake na madhara yake na kujikuta wakijiingiza humo.
Hivyo tunadhani sasa ni wakati mwafaka wa kuwapo kwa mikakati ya kuhakikisha wanafunzi kuanzisha shule za msingi hadi juu wanapata elimu kuhusu rushwa.
Siyo vibaya kuiga kile ambacho kinataka kutekelezwa katika Shule ya Sekondari Kibiti mkoani Pwani kwa kuanzisha midahalo ya wazi kuelimisha kuhusiana na mapambano ya rushwa kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Tunaamini viongozi na watumishi bora wa umma, huandaliwa tangu mwanzo, kwa hiyo suala la kuanzisha somo la maadili shuleni ni la muhimu ili kuchangia kuandaa viongozi watakaoleta mapinduzi chanya ya kiuchumi kwa nchi yetu.
Wanafunzi wakipata elimu kuhusu rushwa na madhara yake, tunaamini kuwa hata watakapokuwa wakubwa wataendelea kuichukia, kutokana na ukweli kwamba inakwamisha maendeleo na inaua uchumi.
Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa utawala bora ni kipaumbele cha kufikia Malengo ya Maendeleo ya Taifa, kwamba utawala bora umekuwa ni jambo muhimu katika kukuza, kuimarisha amani na mengine mengi.
Tunashauri Mkakati wa Taifa wa Dhidi ya Rushwa wa mwaka 2017- 2022 ambapo awamu ya tatu ya mkakati huo ni mwendelezo wa juhudi za serikali za kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa.
Utaratibu wa utoaji wa elimu kuhusu rushwa kutolewa kuanzisha shule za msingi tunauona kama mtazamo mpya unaolenga kuhakikisha rushwa inaondolewa nchini kuanzia sasa na hata baadaye.
Kwa upande mwingine elimu kuhusu rushwa kuanzia ngazi ya shuleni ni uamuzi sahihi kwa kuwa watoto wakipata uelewa mapema kuhusu athari zake, itasaidia kupunguza kama si kumaliza kabisa kasi ya sasa ya matukio ya rushwa ya ngono katika shule na vyuo.
Licha ya kupongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa hususan ya kutoa elimu ya rushwa shuleni, tunazishauri shule zote pamoja na vyuo kutekeleza mpango huo kwa kuwa utasaidia kuongeza uelewa wa watoto na wanafunzi kuhusu rushwa na athari zake kwao hususan ya ngono ambayo imekithiri na kuwaathiri ktika maeneo yao ya masomo.
Matarajio yetu ni kuwa tunaweza kuwa na jamii yenye uelewa mpana kuhusu rushwa, hivyo wengi kuichukia katika jamii na mwishowe janga hilo kupungua kwa kiwango kikubwa katika jamii, hivyo nchi kupaa kimaendeleo katika siku za usoni.










