Mijadala ya kuinua soka ifanyiwe kazi, tusifungiane

09May 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mijadala ya kuinua soka ifanyiwe kazi, tusifungiane

SOKA letu linahitaji uwanja huru na mpana zaidi katika kujadili maendeleo yake na vikwanzo vinavyochangia kushindwa kusonga mbele kwa kasi zaidi kutoka hapa tulipo na kufikia nchi zilizopiga hatua Afrika kama vile Morocco, Misri, Algeria, Tunisia, Afrika Kusini na nyinginezo nyingi zilizopo juu yetu

Kubaki kusema tu kwamba ligi yetu ni miongoni mwa ligi 10 bora barani Afrika, hakutasaidia kitu hasa kutokana na ukweli kwamba bado klabu zetu hazifanyi vizuri kwenye michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF.

Hii ni kutokana na misimu miwili mfululizo ambayo tumeingiza timu nne kwenye michuano hiyo ya CAF; mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika, bado tumekuwa tukibaki na timu moja tu, Simba ambayo imekuwa ikiishia robo fainali.

Takwimu ndizo zinazoweza kuwafanya Watanzania kila mmoja kutembea kifua mbele kwamba ligi yetu ni bora, kwa kumulika namna klabu zetu zinavyofanya vizuri kwenye michuano hiyo ya Afrika na si vinginevyo.

Na kwa kuanika vigezo na takwimu kama hizo, ni wazi kutaongeza ari ya wachezaji kupambana kuweza kufika mbali kwenye michuano hiyo ya Afrika ambayo inaongoza kwa utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani humu.

Tumelazimika kulimulika hilo kutokana na woga mkubwa kwa wenye uwezo wa kulisemea, wakiogopa kwamba wanaweza kufungiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa kale kawoga kwa 'mwanafamilia wa soka' kulikosoa soka letu.

Tumeona mwishoni mwa wiki namna ambavyo hoja nzuri iliyotolewa na Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally ambaye yeye kama mdau wa soka, alidai kuwa timu zinazocheza Ligi Kuu msimu huu zimekuwa dhaifu kwa sababu nyingi zinapigania kuepuka kushuka daraja.

Lakini kutokana na itikadi za Watanzania kubebwa na Usimba na Uyanga, upande wa pili wamekuwa wakigeuza maneno kwa kueleza kwamba alisema "ligi yetu" ni dhaifu, jambo ambalo kwetu sisi tunaona hata kama Ahmed angekuwa amesema hivyo bado si dhambi kwa hoja alizozitoa.

Kinachoonekana ni baadhi kujitokeza kupindua maneno, wakitaka kuona TFF ikimchukulia Ahmed hatua, kitu ambacho sisi tunaona kwa shirikisho hilo kuthubutu kufanya hivyo, kutazidi kuwafanya wadau wa soka wenye nia njema ya kutoa hoja zao za msingi katika kulijenga soka letu kufunga midomo yao.

Kwa kuwafunga mdomo wadau wa soka wenye weledi mkubwa, ni wazi Tanzania itaendelea kuchechemea hapo ilipo kwa miaka mingi zaidi kwani mpira wetu unahitaji uwazi na ushirikishwaji wa maoni kwa kila mwenye nia njema nao.

Hoja aliyoitoa Ahmed akielezea kwamba timu nyingi ni dhaifu hasa akitolea mfano kuwa kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu, ukitoa Simba na Yanga, zilizobaki zote zinapigania kuepuka kushuka daraja na si ubingwa, ni jambo la kutazamwa na kufanyiwa kazi na si kutaka kumfanya kuonekana msaliti.

Tunahitaji kuona akipingwa kwa takwimu, na si baadhi ya wadau wa soka kumlisha maneno wakieleza kwamba alisema ligi ni dhaifu na kwa kufanya hivyo eti anawakatisha tamaa wadhamini ambao wamewekeza kiasi kikubwa cha fedha.

Tunaamini mdhamini yeyote anahitaji kuweka fedha kwenye ushindani mkubwa ili kupata 'walaji' wa bidhaa anayoitangaza, hivyo hoja ya Ahmed hata kama angesema ligi yetu ni dhaifu, bado ingepaswa pia kuchukuliwa kama changamoto kuanzia kwa klabu shiriki, viongozi, TFF na Bodi ya Ligi, TPLB.

Nipashe tukiwa kama wadau namba moja wa michezo nchini, pia tunatamani kuona wakati kama huu zaidi ya timu sita zikiwa zina nafasi sawa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu jambo ambalo lingezidi kuhamasisha wawekezaji kujitokeza kuwekeza na si kama ilivyo sasa timu 14 zikipambana kuepuka kushuka daraja. Hivyo tuache woga na TFF ipokee maoni na kuyafanyia kazi ili msimu ujao kuwe na ushindani mkubwa wa ubingwa na si wa kuepuka kushuka daraja.