Mathalani, Idara ya Uhamiaji ilitangaza nafasi za kazi wakajitokeza waombaji zaidi ya 10,000 iliwalazimu kufanyia usaili uwanja wa taifa.
Aidha, Desemba mwaka 2021 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ilitangaza jumla ya watu 22,106 waliitwa kwenye usahili wa nafasi za ofisa uchunguzi na maofisa uchunguzi wasaidizi wakiwania nafasi 350.
Wote walitakiwa kwenda Dodoma kwa ajili ya usaili wa maandishi ambao ulifanyika kwenye vyuo vitatu tofauti, huku vingine vikiwa nje ya mji ambako wahusika wanapaswa kutumia gharana.
Hivi karibuni, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ilitangaza nafasi za ualimu na afya ambazo zinataka watu zaidi ya 12,000.
Tathmini ya maombi iliyotolewa na wizara hiyo ilionyesha kuwa kuna waombaji zaidi ya 83,000 ikiwa ni wastani wa waombaji zaidi ya 16,000 kwa siku, jambo linaloonyesha hali ngumu ya ajira iliyopo nchini kwa sasa.
Kilichotusukuma kuandika tahariri hii leo ni namna wanaoomba nafasi hizi wanaitwa kwenye usaili inakuwa ni ya kuwagharimu sana wao na familia zao, ili hali hawana kazi wala kipato.
Unapowasafirisha waombaji hawa kutoka mikoa mbalimbali ambao wengine wanasafiri zaidi ya saa 12, wanakwenda Dodoma ambako wanatakiwa kupangisha hoteli, lodge au nyumba za kulala wageni kwa siku tatu au nne watakazokuwa hapo ni kuwaumiza.
Mathalani, mtu anayetoka Kasulu, Kigoma au Sumbawaga au eneo jingine la pembezoni kabisa ambaye familia yake imeshamsomesha hadi chuo kikuu sasa inataka kuona akitoa msaada kwa familia, naye anatakiwa asiwe na chini ya shilingi 200,000 kwa ajili ya usaili ambao hana uhakika wa kupata ajira kutokana na ushindani.
Anapotakiwa kusafiri atatakiwa kuwa na nauli, chakula na mahitaji mengine, jambo ambalo ni gumu kwa watu maskini ambao ndiyo wanatafuta kazi ili kujikwamua.
Tunadhani lazima serikali iliangalie hili kwamba mchakato wa usaili ufanyike kwa njia ya mtandao kupunguza idadi ya wanaovuka hatua ya pili ya mchakato huo.
Aidha, kama inawezekana muhimu usaili ukafanyika kwa kanda za nchi ili kuwapunguzia wahusika gharama, hata serikali yenyewe kutumia gharama kubwa kuwaweka maofisa kwenye mchakato huo kwa muda mrefu na kuwagharamia.
Kwa mfano, waombaji kutoka Zanzibar, Pwani na Dar es Salaam na Tanga wanaweza kupangiwa kanda yao. Arusha, Kilimanjaro na Manyara eneo moja pia.
Mikoa ya Kanda ya Ziwa kama Kagera, Shinyanga, Mara, Mwanza, Simiyu na Geita wanaweza pia kuwa na kituo chao.
Hivyo hivyo, mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida inaweza kuwa na kituo kimoja wakati Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa pia inaweza kuwa na kituo kimoja. Kadhalika, mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma inaweza kuwakutanisha pamoja waombaji kutoka maeneo hayo wakati mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Songwe inaweza kuwa na kituo kimoja.
Kwa kutumia utaratibu huu, serikali itawapunguzia mzigo wa gharama, usumbufu na mateso waombaji wa nafasi za ajira ambao wengi ni kutoka familia maskini. Tunawashauri wabunge wetu kuliona hili na kulipigia kelele katika mkutano unaoendelea hususan wakati wa makadirio ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora).
Kuwasafirisha watu zaidi ya 83,000 kwenda Dodoma na wakati huo huo kuna shughuli nyingine zinaendelea kama za mikutano ni kuwatesa kwa kuwa watahangaika kupata mahali pa kulala, kwa kuwa Jiji la Dodoma bado halijaweza kujitosheleza kwa wageni wote kwa wakati mmoja.
Ni muhimu kuangalia jambo hili ili kupunguza usumbufu na kupoteza muda, kwa sasa dunia imepiga hatua kutokana na ukuaji wa teknolojia, umerahisisha utendaji kazi wa kila siku, hata usaili unaweza kufanyika kwa njia ya mtandao katika kuchuja kundi la awali na kubali na wachache wa kusonga mbele.










