Kila mmoja atimize wajibu kuifanikisha sensa Agosti

05May 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kila mmoja atimize wajibu kuifanikisha sensa Agosti

MAANDALIZI ya Sensa ya Watu na Makazi itakayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu, yamefikia zaidi ya asilimia 81, na inakisiwa kwamba hadi kufikia Juni yatakuwa yamefikia asilimia 100.

Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi wakati akizungumza kwenye sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jijini Dodoma.

Majaliwa anawataka wafanyakazi kuwa mabalozi wa kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika Sensa ya Watu na Makazi lengo likiwa ni kuhakikisha kila Mtanzania anahesabiwa utakapofika wakati mwafaka.

Mwaka huu Taifa letu litakuwa linatekeleza shughuli hii kubwa na muhimu kwa maendeleo yake na wananchi kwa ujumla. Tunasema hivi kutokana na umuhimu wa sensa kwa maendeleo ya nchi.

Kwa sasa wimbo unaoimbwa na viongozi wa serikali na hata wa madhehebu ya dini ni kuhimiza Watanzania, ili wajiandae kwa wingi kuhesabiwa, kutokana na ukweli kwamba sensa ina umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa maendeleo ya taifa.

Wakati wa maadhimisho ya Pasaka mwezi uliopita tuliwaona na kuwasikia viongozi wa Kikristo katika mahubiri yao kwenye ibada wakitoa msisitizo kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika sensa ili wahesabiwe, hivyo kuiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo.

Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zubeir, juzi wakati wa swala ya Idd aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kujitokeza kushiriki katika sensa hiyo, kwa kuwa hilo ni jambo la wote na wasifuate kauli au yanayosemwa katika Uislamu hakuna sensa.

Anahimiza Waislam na Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki suala hilo kwa kuwa ni haki kwa Waislamu na Watanzania kushiriki na kukubali kuhesabiwa kwa manufaa ya Taifa.

Tunaamini sensa ni ya muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa na watu kwa kuwa inasaidia serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025.

Kimsingi, kuna masuala ya huduma za kijamii kuanzia kwenye afya, elimu na mengine muhimu ambayo serikali hainabudi kuyapata kupitia sensa, hivyo tunadhani ni vyema watu kuhesabiwa ili takwimu sahihi zipatikane.

Bila kuwapo kwa takwimu sahihi, serikali inaweza kupata ugumu katika kupanga mipango yake itakayowezesha Watanzania kujiletea maendeleo, hivyo tunashauri kila Mtanzania ajiandae kuhesabiwa.

Lakini pamoja na hayo, tunashauri wale ambao watapewa jukumu la kuhesabu Watanzania, wafike kwa wakati kwenye maeneo husika, wawe na vitendea kazi vinavyotakiwa ili kupata takwimu kwa usahihi.

Hilo likifanyika, tunaamini kwamba, hakutakuwa na visingizio kutoka kwa wanaohesabiwa kwenda kwa makarani, kwamba  hawakufika kwa wakati na kusababisha waondoke kwenye makazi yao kwenda kwenye shughuli zao.

Wito wetu ni kwamba, makarani wafike kwa wakati wakiwa na vifaa vilivyokamilika, lakini siku hiyo watu wabaki nyumbani wahesabiwe kwanza ndipo waende katika shughuli zao na  watoe taarifa sahihi kwa makarabi.

Tunasisitiza kutoa taarifa sahihi, kwa sababu kumekuwapo na elimu potofu kuwa sensa inalenga kutambua watu waliopata chanjo ya UVIKO-19 na pia kuna dodosa linalohusiana na dini huku wapotoshaji pia wakidai kuwa serikali inawahesabu watu ili kuwadai kodi.

Hayo yalishatolewa ufafanuzi na serikali, lakini bado wale ambao hawajaelewa, tunawashauri wawe tayari kuhesabiwa na kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia serikali kupanga shughuli za maendeleo kwa wananchi wake.

Ikumbukwe kuwa, katika sensa kuna taarifa za msingi za kuwezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote.  

Kwa maana hiyo, kila upande utimize wajibu wake inavyotakiwa kuanzia wanaohesabu watu, wale wanaohesabiwa ili kile ambacho serikali imekusudia kukifanya kupitia sensa hiyo, kifanikiwe.

Tunaamini pia kuwa serikali kwa upande wake itahakikisha kwamba maandalizi hayo yatakuwa yamekamilika kwa asilimia 100 kabla ya kufanyika kwa sensa hiyo, ikiwamo kufanyika kwa sensa ya majaribio.