Diaspora waondolewe vikwazo kuwekeza nchini

29Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Diaspora waondolewe vikwazo kuwekeza nchini

HIVI karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, alikutana na Watanzania wanaoishi Marekani na kutoa ujumbe ambao unawagusa wote wanaoishi nje ya nchi na waliokosa haki mbalimbali, lakini sasa kilio chao kimesikika isipokuwa uraia pacha.

Haya yanakuja baada ya taarifa ya serikali ya Oktoba mwaka jana, ambayo ilisema inakamilisha mchakato wa kupitia maoni ya diaspora, kuhusu kupewa hadhi maalum itakayowawezesha kushiriki masuala mbalimbali ya maendeleo nchini.

Rais Samia alisema Watanzania hao watapata hadhi maalum ambayo itahusisha haki nyingine za msingi ikiwamo haki ya kupata ardhi, mirathi na kuwa na mstari wao katika kiwanja cha ndege.

Alisema Sera ya Diaspora itakapokamilika itasambazwa nchi zote ili waboreshe kwa kadri wanavyotaka, lakini aliwapa tahadhari kuwa sio kila watakachopendekeza kitakubalika.

Aidha, alisema serikali inatengeneza mtandao wa kidijitali kwa ajili ya kuwasajili Watanzania waishio nje ya nchi ili kutatua tatizo la kutojulikana idadi yao ubalozini, huku akieleza kuwa wanatambua mchango wao kwenye maendeleo ya nchi.

Tunaipongeza serikali kwa hatua hii kwa kuwa inakwenda kusaidia nchi kwa kuwa tunaamini Watanzania hao wanakuwa na fedha au wanaona fursa ambazo wanaweza kuziendeleza nchini mwao ambazo zitasaidia nchi kupata mapato, kuajiri wengine na kukuza maendeleo.

Ombi kubwa la diaspora ni kupata uraia pacha ambalo liliibuka wakati wa Bunge Maalum la Katiba ikiwa ni hoja kutoka kwa Watanzania hao na ipo kwenye Rasimu ya Katiba ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, iliyotengenezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.

Taarifa ya mwaka jana ya serikali ilieleza kuwa Watanzania waishio nje ya nchi ni zaidi ya milioni mbili ambao walisaini waraka maalum wapate haki ya kupiga kura kwa kuwa walizaliwa nchini hivyo wanapaswa kuwa na haki hiyo, lakini imekosa nguvu baada ya kupata uraia wa nchi nyingine ambako walikwenda kimasomo au kutafuta maisha.

Tunaamini kila Mtanzania anayeishi nje ya nchi atatumia vyema nafasi hiyo kuboresha sera hiyo ili kusiwe na atakayeachwa nyuma na kuwa na malalamiko kuwa kilichopitishwa hakikuwa jumuishi.

Baada ya kukamilika kwa sera hiyo Watanzania hao watatumia vyema nafasi ya hadhi maalum kuwekeza nyumbani kwa manufaa yao ya sasa na baadaye, huku wakitoa ajira kwa wenzao.

Tunaamini zipo fursa nyingi za kuleta nchini, lakini walishindwa kutokana na kukosekana utaratibu maalum hasa wa umiliki wa uwekezaji watakaoufanya, sera hiyo itakapokamilika itasaidia kuleta mabadiliko makubwa kwa manufaa ya pande zote.

Lakini ni muhimu kwa serikali kuangalia upya suala la uraia pacha, kujifunza kwa nchi nyingine ambazo zimeruhusu suala hilo, faida wanazopata na hasara, kwa kuwa mtu anapokuwa na uhakika wa uraia maana yake anawekeza kwa moyo wote.

Pia, ni muhimu kuendelea kuhamasisha Watanzania walioko nje kuona umuhimu wa kuwekeza nchini kwa kuwaondolea vikwazo vinavyosababisha washindwe kurudi nyumbani kuwekeza kwenye viwanda, biashara na kampuni kwa kuhamisha maarifa kutoka nchi zilizoendelea na kuyaleta nchini kwa faida ya watu wake.

Tunaamini huenda wapo Watanzania wanaoishi nje hawajui wanaweza kuwekeza au kuna vikwazo vimeondolewa ili wanapopata fursa wailete nchini kwa manufaa yao, familia zao na taifa kwa ujumla.

Wapo walioenda kwenye nchi hizo kwa masomo na kuamua kubaki huko, walioenda kwenye mikutano na makongamano, lakini wapo waliozaliwa huko kwa kuwa wazazi walikuwa masomoni, lakini wao wana asili ya Tanzania, kwa kuzaliwa huko kwa mujibu wa sheria zetu sio raia, wanapaswa kufuata taratibu za kuomba kupata uraia.