Simba, Yanga wapeni raha mashabiki wenu

30Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga wapeni raha mashabiki wenu

WATANI wa jadi, Simba na Yanga wanatarajia kukutana katika mechi ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi ya kwanza msimu huu wa 2021/2022 ambayo ilifanyika Desemba 11, mwaka jana kwenye uwanja huo huo, vigogo hao walitoka sare ya bila kufungana.

Hata hivyo, Yanga itaingia uwanjani ikiwa ndio vinara wa ligi hiyo yenye kushirikisha timu 16 lakini ikiwa na rekodi ya kutopoteza mchezo hata mmoja tangu kuanza kwa msimu huu, wakati Simba wao ndio mabingwa watetezi wa misimu minne mfululizo.

Wekundu wa Msimbazi pia wataikabili Yanga ikiwa bado na joto la mashindano ya kimataifa, ingawa imeondolewa kwenye hatua ya robo fainali na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa penalti kufuatia matokeo ya jumla kufungana bao 1-1.

Mechi hiyo ambayo inatarajia kuendelea kutoa sura ya mbio za ubingwa, ni mchezo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki mbalimbali wa soka barani Afrika, na hiyo ni kutokana na ukongwe wa klabu hizo zote za Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Endapo Yanga itapata ushindi katika mchezo wa leo, itakuwa imeendelea kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati Simba itarejesha matumaini ya kulibakisha taji inalolishikilia lakini pia itasaidia kupunguza machungu ya kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa heshima ya mchezo wenyewe, wachezaji wanatarajiwa kujituma na kuonyesha ubora wao katika kuhakikisha wanapata ushindi na kufikia malengo waliyojiwekea msimu huu.

Kila mchezaji anatakiwa afahamu mechi hiyo inatarajiwa kuangaliwa na wadau mbalimbali wa mpira wa miguu, hivyo kuonyesha kiwango bora na nidhamu, kutasaidia kuwatangaza na hatimaye kupata ofa zitakazoboresha maisha yao.

Hatutarajii kuona nidhamu mbaya kabla na baada ya mchezo kumalizika kwa sababu kupitia mechi hiyo, wachezaji chipukizi wanajifunza vitu mbalimbali na endapo vitendo vya hovyo vitachukua nafasi, huenda ikaharibu ukubwa wa dabi hiyo kwa nyota wanaochipukia.

Tunazo kumbukumbu kuna baadhi ya wachezaji waliopata mafanikio baada ya kumalizika kwa mechi ya dabi kutokana na ubora waliouonyesha kwa klabu zao kuwapata mikataba mipya yenye maslahi zaidi lakini pia wapo nyota 'waliopotea' baada ya kumalizika kwa mitanange hiyo ya watani wa jadi.

Soka la sasa ni la kiufundi, wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi hakikisheni mnawaandaa wachezaji wenu kufanya yale yanayostahili katika kuhakikisha wanapata ushindi, lakini pia waheshimu waamuzi ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mechi hiyo.

Waamuzi pia wanatakiwa kufanya kazi yao kwa umakini na weledi kwa sababu kupendelea upande mmoja kunaweza kusababisha mechi kuharibika au kuamsha hasira kwa timu iliyoonewa, kutafsiri vyema sheria 17 za soka ndio kutasaidia kila timu kuvuna ilichokipanda.

Ikumbukwe waamuzi wanaposhindwa kumudu mchezo, hupunguza pia raha ya aliyeshinda kushangilia ushindi wake.

Bila kusahau mashabiki watakaojitokeza uwanjani kushuhudia mchezo huo wanatakiwa wafahamu mipaka na nafasi yao.

Kila shabiki anatakiwa ahakikishe anashangilia kwa nidhamu na bila kuharibu miundombinu iliyowekwa kwenye uwanja huo unaomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kutumia maneno makali kwa wachezaji, waamuzi au mashabiki wenyewe kwa wenyewe ni mambo yasitotakiwa kuonekana kwenye mchezo huo ambao huvutia wadau wa soka kutoka mataifa ya jirani.

Simba na Yanga, mbali na kusaka pointi, tumieni mechi hiyo kwa kuipa heshima na hadhi inayostahili Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imeweza kupanda viwango na kushika nafasi za juu barani Afrika.