Hata hivyo, mechi hiyo ilikuwa ikitarajiwa kupunguza mbio za Yanga kuelekea kuwania kutwaa ubingwa msimu huu kama Simba ingeshinda, lakini bado matokeo hayo hajahalalisha moja kwa moja vinara hao wa Ligi Kuu Bara kujihakikishia kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya misimu minne.
Licha Yanga kuwa na pointi 55 kileleni, 13 zaidi ya Simba iliyopo nafasi ya pili huku zikiwa zimebaki takriban mechi tisa kabla Ligi hiyo kumalizika msimu huu, kimahesabu bado ligi haijamalizika hadi itafikia ukingoni kwani lolote linaweza kutokea ingawa kwa muonekano ni vigumu.
Yanga imebakiza mechi tisa wakati Simba imebakiza mechi 10 kabla ya ligi hiyo kumalizika, hivyo ili Simba iwe bingwa inahitaji kushinda mechi zake zote zitakazoiwezesha kumaliza na pointi 72 wakati huo ikiombea Yanga kupoteza pointi 11 katika michezo yake tisa iyobaki jambo ambalo ni vigumu, lakini kwenye soka lolote linaweza kutokea.
Pamoja na vita hivyo, vya kuwania ubingwa ambavyo vinaonekana kuwa upande wa Yanga kama itachanga karata zake vema kwa kushinda mechi sita tu kati ya tisa, bado kuna mpambano mkali kwa upande wa kuwania nafasi nne za juu katika ligi hiyo ambayo msimu huu kuna bonasi kubwa kutoka kwa wadhamini wa haki za matangazo ya televisheni, Kampuni ya Azam Media Limited.
Ushindani huo umeongezeka kutokana na Kampuni ya Azam Media Limited kutangaza bonasi kubwa katika mkataba wa udhanimi walioingia na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka nchini Mei mwaka jana wenye thamani ya Sh. bilioni 225.6 kwa kipindi cha miaka 10.
Katika mkataba huo bingwa atapata mbali na zawadi kutoka kwa mdhamini mkuu, Benki ya NBC, Azam Media Ltd itatoa bonasi ya Sh. milioni 500, mshindi wa pili milioni 250, watatu milioni 225, wa nne milioni 200 na zitakwenda zikipungua hadi timu zitakazocheza mechi ya mtoano kuwania kucheza Ligi Kuu msimu ujao, zikilamba milioni 20 kila moja.
Lakini pia juhudi za Simba kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufika hatua ya robo fainali, kumeiongezea Tanzania pointi na kuwa miongoni mwa nchi 12 zitakazoingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa; mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho.
Kwa mantiki hiyo, kuna uwezekano mkubwa timu zitakazomaliza nafasi nne za juu msimu huu zikakata tiketi moja kwa moja kushiriki michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika, jambo ambalo limezidi kuongeza ushindani mkubwa katika ligi hiyo.
Hiyo ni kutokana na msimu huu kuwapo kwa uwezekano mkubwa kwa Simba ama Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka nchini maarufu FA Cup na dhidi ya Azam FC ama Coastal Union, hivyo moja kati ya watani hao wa jadi wakibeba ubingwa, tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika itarudi kwenye timu zilizomaliza nafasi nne za juu Ligi Kuu Bara.
Jambo ambalo linaweza kutokea, lakini pia kama Coastal Union ama Azam FC mojawapo itatwaa Kombe la FA, basi timu tatu zitakazomaliza nafasi ya juu kwenye Ligi Kuu zitakata tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa pamoja na iliyobeba ubingwa huo wa FA.
Kutokana na vita hivyo, kuna haja kwa TFF na TPLB, kuelekeza macho yao kwenye hatua hii ya lala salama Ligi Kuu Bara, kwani kunaweza kuchezeka mchezo mchafu wa rushwa ili kupanga matokeo kuanzia vita vya ubingwa hadi zinazowania kumaliza nafasi ya tatu na ya nne.
Lakini pia ikumbukwe kuna kundi linalopambana kuepuka kwenda kucheza mechi za mchujo na timu mbili kutoka Ligi ya Championship, ili kucheza Ligi Kuu msimu ujao, hivyo nako si salama hasa ukizingatia timu zote ukiondoa Simba na Yanga, zilizobaki nyingi zinapishana pointi moja hadi tatu tu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Hivyo, tunaitaka TFF na TPLB kuongeza umakini na ikiwezekana kuvishiriksiha vyombo vya usalama na zaidi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili kuzuia upangaji wa matokeo ambao utakwenda kusababisha kupatikana wawakilishi wabovu kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, lakini pia ukipora haki ya timu zinazostahili bonasi kubwa kutoka kwa wadhamini na zile zitakazopoteza haki yao ya kuendelea kuwamo Ligi Kuu msimu ujao.