Zama hizo ukitaka kupata taa aina ya koroboi au kibatari, uwe unatoka kijijini au mjini, Mwanza, ni lazima utakwenda kununua katika mtaa huo, ndiko zilikuwa zinatengenezwa kwa wingi na kuuzwa kwa bei tofauti, kulingana na ukubwa wake.
Leo hii, ni kama simulizi kuamini kwamba imebaki historia kuwa machinga waliokuwa wakipambana kuondoka katika eneo hilo baada ya serikali kuagiza machinga kuondolewa katikati ya jiji na kuhakikisha wanapelekwa kwenye maeneo yao waliyotengewa.
Katika miaka yote kihistoria katika mtaa huo wa Makoroboi walikuwa wakipambana na vyombo vya dola, wanapoondolewa,vurugu zilikuwa zikitawala kurushiwa mawe mgambo wa jiji hata askari wengineo na kulazimika kutumika nguvu kubwa ya kuwapiga mabomu ya machozi na magari ya washawasha, ili kuwatawanya waweze kuondoka kwenda kwenye maeneo yao rasmi waliyopewa.
Ni msuguano uliochangia watu wengi kupoteza maisha au kujeruhiwa na kupata ulemavu, wachache waliondoka, lakini baada ya muda mfupi, wanajaa tena eneo hilo. Wapo wanaosifika walikuwa nyuma yao bila ya kujali athari zake.
Mtaa huo, pia ni njia maarufu wanayopita watu mbalimbali wanaotoka nje ya jiji hilo katika mikoa mbalimbali, wale wanaokwenda mjini kila siku hawawezi kumaliza siku nyingi bila ya kupita mtaa huo, ambao ulikuwa umesheheni maduka ya nguo na bidhaa mbalimbali wakiwemo mama lishe.
Machinga hao walikuwa ni vigumu kuwaondoa kutokana na mambo ya kisiasa, lakini serikali imeweza kufanikiwa kupaweka tofauti katika tafsiri mpya.
Wafanyabiashara hao wadogo, walikuwa wamejenga vibanda vyenye gharama kubwa na kuweka mbele ya maduka mengine ya wafanyabiashara wakubwa, kila aina ya bidhaa zilikuwa zikipatikana.
Machinga wengine walitumiwa na wafanyabiashara wenye maduka makubwa kufanya biashara hizo, lengo ni kukwepa kodi za serikali wanazotakiwa kulipa kihalali, hapo ndipo wengi wao wataumbuka na kuonekana biashara zao wanavyoziendesha.
Mimi binafsi naishukuru serikali kuwapeleka katika maeneo yao waliyotengewa, wengi walikuwa wakifanya biashara zao katika maeneo hatarishi, walijenga vibanda juu ya mifereji, mitaro na kusababisha kuziba,kutoa harufu mbaya pamoja na uchafuzi wa mazingira.
Ulikuwa mchango mkubwa kwa jiji la Mwanza hata likashuhudiwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira, leo hii linabadilika kurejea katika usafi ukawa changamoto yenye sura yake. Hivi sasa, jiji limehamia sura mpya hata wananchi wameona kumbe serikali inawapeleka kwenye maeneo sahihi.
Kazi iliyobaki ni watendaji wa serikali kusimamia maeneo ya machinga walikopelekwa, kuhakikisha miundombinu muhimu ipo katika masoko hayo, mifereji, mitaro, barabara, umeme, maji na usafi wa mazingira, ili kuepuka wakati wa mvua magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu yasiibuke.
Tukumbuke, Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye hotuba yake wakati akiingia madarakani kuwa anaona mbali na akawataka watendaji wa serikali kuchapa kazi kwa bidii na maarifa kuwahudumia wananchi.










