Alisema miaka ya karibuni kumekuwa na tabia ya watu kujikweza kutaka utukufu kutoka kwa watu wanaowatumikia, huku wakisahau kuwa kazi nzuri inayofanywa na muhusika itamfikisha kwenye utukufu kuliko kulazimisha kutukuzwa.
Aidha, kwa kuanza ameahidi kuwa mfano wa kuwa mtumishi wa watu na siyo kutaka kutukuzwa, huku akiahidi kuwafikia wananchi kwa kufanya ziara.
Tunaunga mkono kauli ya Kinana kuwa kuna wakati dhana ya mtumishi wa umma ilipotea na kuwa na watu wenye kutaka kuabudiwa, kutukuzwa kunyenyekewa kupita kiasi wakati wako kwenye ofisi za umma wanawajibika kuwatumikia walipa kodi.
Wapo watumishi waliotumia vibaya ofisi za umma kujitajirisha na watu wao wa karibu, wengine wakiota majipu kwenye makwapa (kiburi, kujikweza) kutokana na kujikweza mbele ya umma kwa sababu ya nguvu ya fedha na nafasi walizonazo.
Wengi wanasahau cheo ni dhamana na unapoaminiwa unatakiwa kulipa imani, badala yake wananchi ambao ndiyo mabosi wao wanawadharau , huku wakisigina kanuni na sheria zilizopo.
Kanuni za utendaji katika utumishi wa umma za mwaka 2005 zinasema ili utumishi wa umma uwe wenye ufanisi na wa kuheshimika, watumishi wanapaswa kuzifuata kanuni za maadili ya utumishi pamoja na kuwa na tabia na mwenendo unaozingatia kutoa huduma bora, utii wa serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma , kuheshimu sheria na matumizi sahihi ya taarifa.
Kanuni hiyo inasema huduma bora ni kuweka malengo halisi ya kazi, ili kuwawezesha kufikia kiwango cha juu kabisa katika utendaji wao wa kazi.
Pia, inawataka kuwa wabunifu, wavumbuzi na siku zote kujibidiisha kuongeza viwango vya utendaji kwa kujiongezea maarifa na ujuzi.
Aidha, wanatakiwa kutumia misingi ya haki, badala ya upendeleo katika utoaji wa huduma, kuepuka kufanya vitendo viovu au kutamka maneno yanayolenga kuwaaibisha watumishi wa ngazi moja, za chini au wa vyeo vya juu.
Pia, wanatakiwa kuepuka matumizi ya lugha mbaya, matusi, utani na hasira katika utendaji wa kazi, kupeuka mwenendo mbaya ambao utaathiri ufanisi katika utendaji kazi, kufika sehemu ya kazi kwa muda uliopangwa na kuzingatia muda rasmi wa kufanyakazi.
Haya ni machache kati ya mengi ambayo yakifuatwa yatamtambulisha mtumishi sahihi anayelipwa kwa kodi za watanzania, lakini baadhi wametaka kuwa miunguwatu kwa sababu ya vyeo hivyo.
Wapo walioonekana kutumia nafasi zao kuwanyanyasa wananchi wazi kwa kutumia maneno yao, kiasi cha wao kuwa kama waliowaajiri wananchi na siyo wameajiriwa, huku wengine wakijipatia utajiri bila hofu yoyote.
Katika baadhi ya ofisi za umma watumishi hawatimizi wajibu wao ipasavyo huku wakisema serikalini hakuna haja ya kukimbizana na kazi kama sekta binafsi, na hilo hudhihirika zaidi Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wanapofanya ziara kwenye eneo la wananchi huibua kero ambazo zinastahili kutatuliwa na watumishi wa ngazi za chini.
Ni lazima watumishi wawe karibu na wananchi katika kutatua kero zao, kama alivyoona Kinana nasi tumeona kuna tatizo kubwa kwa watumishi wengi ni lazima kufuatilia kwa karibu ili kurejesha nidhamu na uwajibikaji.
Ofisi za umma isiwe ni sehemu ya kutengeneza miungu watu ambao wanatumia kodi za watanzania, bali wawepo kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa kuwa ni wajibu wao kuwajibika kwa mujibu wa maadili ili kupunguza mzigo na lawama kwa viongozi wa ngazi za juu.










