Bila uwajibikaji madudu ripoti ya CAG hayataisha

13Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Bila uwajibikaji madudu ripoti ya CAG hayataisha

JANA ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilikabidhiwa kwa Bunge ambayo sasa itakuwa wazi kwa umma kusoma na kujua kilichopo ndani.

Katika ukaguzi wake kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), CAG alibaini watu 444 walipimwa kipimo cha damu zaidi ya mara moja, huku wengine wakipimwa zaidi ya mara 30 kwa siku moja.
 
Aidha, wanaume 731 walionekana wamepewa huduma za kujifungua jambo ambalo linatia shaka, na kuzua maswali mengi juu ya matumizi ya fedha za umma.
 
Kwa ujumla ripoti inaonyesha wapi pametoboka serikalini kiasi cha fedha kutoka kwenda kwenye mikono ya watu, badala ya kuhudumia wananchi ambao ndiyo walipa kodi.
 
Kila mwaka ripoti ya CAG inaonyesha upigaji ambao kimsingi unakatisha tamaa walipakodi, kwamba fedha zao hazitunzwi na kutumika kwenye miradi inayotakiwa ambayo italeta tija kwenye maisha yao.
 
Pia, alibaini kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za mikopo haikukamilika kwa wakati, ambayo moja kwa moja inagusa maisha ya watu jambo linaloonyesha inapaswa kufuatiliwa kwa karibu utekelezaji wake.
 
Kwenye halamshauri madudu yameendelea kuonekana ikiwamo uchepushaji wa fedha nyingi kutoka hazina kwenda maeneo hayo kuliko kiasi kilichotakiwa, jambo ambalo linakatisha tamaa kwa kuwa wananchi wanatarajia kupata huduma muhimu.
 
Wakati hali ikiwa hivi walipakodi ndiyo wanatibiwa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma ambazo kila mara wanaambiwa hakuna dawa au vifaa tiba, huku wengine wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
 
Lakini ndiyo wanateseka kuyafikia masoko kutokana na miundombinu duni kwa kuwa hakuna fedha za kujenga barabara ili wasafiri bila kikwazo, lakini ndiyo hao ambao watoto wao wanakosa elimu nzuri kwa kuwa hakuna madawati au vyumba vya madarasa vya kutosha.
 
Pia, ndiyo hao wanaokosa maji wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji huku wanawake na wasichana wakipata madhila ya kubakwa au kufanyiwa vitendo vibaya, lakini hao hao wanasikia fedha zimechotwa na watu fulani.
 
Ni lazima kujenga mifumo ya uwajibikaji kuzuia fedha za umma kupenya kwenye mkondo usio sahihi, kwamba isizoeleke kuwa kuiba ni jambo la kawaida.
 
Ni muhimu watumishi wa umma wakatenda majukumu yao kwa hofu ya Mungu ndani yao kwa kutambua kuwa nafasi walizopewa ni dhamana na ipo siku mbele ya muumba wataulizwa kama walitimiza wajibu wao ipasavyo.
 
Kwa Mtanzania maskini asiye na uhakika wa kesho atakula nini anaposikia fedha zimechotwa kwenye mradi ambao ungebadilisha maisha yake ni kuendelea kumsononesha na kutokuwa na huruma kwa kuwa huenda kuna waliofariki kwa kukosa dawa au huduma muhimu za afya.
 
Leo hii huduma za afya kwenye vituo vya huduma vya serikali siyo za kuridhisha kiasi cha wengi kukimbilia sekta binafsi, lakini ilipaswa kila mmoja kukimbilia huduma za umma kwa kuwa ni nzuri, za uhakika na nafuu kama nchi zilizoendelea.
 
Ukisikiliza wabunge kila mara wanauliza maswali ya lini serikali itafanya hili na hili au kutoa fedha za kutekeleza mradi fulani ambao unategemewa na wananchi fulani, jibu huwa ni kwamba mchakato unaendelea na fedha itakapopatikana utajengwa, lakini wakati huo huo kuna watu wamefuja fedha za umma kwa manufaa yao.
 
Kwa nchi zilizoendelea hawazungumzii tena huduma za afya kama jambo la gharama bali ni bure kuanzia elimu, afya na miundombinu kwa kuwa walitumia fedha zao vizuri kuhakiksiha zinajengwa, lakini ni kashfa na kosa kubwa kwa mtu kukwepa kodi au kuiba fedha au mali ya umma.

Wapo waliowajibishwa ikiwamo kuondolewa madarakani kwa sababu ya kubainika kutumia vibaya mali ya umma, lakini kwa nchi za Afrika inaonekana ni kawaida kwa kuwa upo mtandao wa kulinda ulaji kuendelea, jambo ambalo linapaswa kukemewa ili kuboresha maisha ya watu.