Wachezaji Simba sasa wajifunze kunufaika na VAR michuano Caf

11Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wachezaji Simba sasa wajifunze kunufaika na VAR michuano Caf

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limetangaza kuanzia hatua ya robo fainali na kuendea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, teknolojia ya video maalum kwa ajili ya kumsaidia mwamuzi (VAR), itaanza kutumika rasmi.

Hii itakuwa mara ya kwanza katika historia ya soka la nchi hii na Afrika Mashariki, VAR kutumika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini pia kwa Wawakilishi wa Tanzania, Simba kuwa klabu ya kwanza nchini kutumia teknolojia hiyo kwenye mashindano hayo ya Afrika.

Simba kama zilivyo klabu nyingine katika mashindano hayo ya CAF, itaanza kutumia VAR kwenye mechi yake ya kwanza ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho itakapoikaribisha Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili wiki hii.

Simba ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa ngazi ya klabu, itahitaji kushinda kwa idadi kubwa ya mabao kwenye mechi hiyo ili kurahisisha kazi ya kufuzu nusu fainali watakaporudiana ugenini wiki moja baadaye.

Tunaamini hilo linawezekana hasa kutokana na uwezo wa kikosi cha Simba pamoja na benchi lao la ufundi, lakini wakipata nguvu kubwa kutoka kwa mashabiki 60,000 walioruhusiwa kuingia uwanjani, hivyo kilichobaki ni wachezaji kuelekezwa tu namna ya kunufaika na VAR katika mchezo huo.

Hata hivyo, kwa kasi ya mawinga wa Simba, Bernard Morrison na Pape Sakho, ambao mara nyingi hukokota mpira na kulazimisha kuingia nao ndani ya 18, tunaamini VAR inaweza kuwa upande wao kwa kunufaika na penalti endapo wachezaji hao wakielimishwa kucheza na akili ya mwamuzi lakini pia namna ya kugongana kwa faida.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba mara nyingi mwamuzi hulazimika kwenda kuangalia marudio ya tukio husika kwenye VAR endapo tu wachezaji watamfuata kulalamika kutoridhishwa na uamuzi alioutoa kuhusu faulo ama madhambi yoyote watakayotendewa.

Kama wachezaji wa Simba watachukulia 'poa tu' (sawa tu) kwa kila uamuzi ambao mwamuzi anatoa dhidi yao bila kumfuata kulalamika, ni wazi hawatanufaika na VAR, hivyo kuwanufaisha wapinzani wao, Orlando Pirates.

Lakini pia wachezaji wa Simba hawana budi kuwa makini kwa kuepuka kucheza madhambi hususan ndani ya eneo la hatari kwani wapinzani wao nao watakuwa makini wakitaka kunufaika na VAR, ambayo inang'ata pande zote.

Kwa mantiki hiyo, benchi la ufundi linapaswa kuwakumbusha na kuwasisitiza namna ya kunufaika na VAR, kwani tunaamini wachezaji nao wamekuwa wakifuatilia mechi mbalimbali ambazo teknolojia hiyo imekuwa ikitumika, na kuona namna gani wenzao wanafanya ili kumshawishi mwamuzi kwenda kujiridhisha.

Katika hilo pia, ni wakati muafaka kwa wachezaji wa klabu zote nchini kuanza kujifunza mengi kupitia mechi hiyo na nyinginezo, kuhusu namna ya kunufaika na VAR.

Tunasema hivyo, kutokana na ukweli kwamba, ni wazi mafanikio ya VAR katika hatua hii ya robo fainali msimu huu, yanaweza kuchochea CAF kutangaza teknolojia hiyo kuanza kutumika kwenye michuano yake yote kuanzia hatua za awali msimu ujao.

Pamoja na hayo yote, benchi la ufundi la Simba wanapaswa kusoma na kuchanga vema karata zao kwa kuandaa mbinu zitakazowalazimisha wapinzani wao kucheza madhambi zaidi kwenye mechi hiyo na hata ile ya marudiano ugenini.

Lakini pia, Simba haina budi kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo ambao tunaamini utakuwa mgumu kwa kila upande hasa kwa wawakilishi hao wa Tanzania ambao watakuwa na presha kubwa ya kutaka kupata ushindi nyumbani. Kila Kheri Simba katika maandalizi ya mechi hiyo muhimu kwenu.