Waamuzi wanaweza kumaliza hili bila VAR

26Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Waamuzi wanaweza kumaliza hili bila VAR

KUMEKUWA na kelele nyingi za wadau wa soka kuhusiana na mamuzi ya waamuzi wa mpira wa miguu kwenye Ligi Kuu Tanzania bara na zile za chini.

Wadau wengi wameonesha kwamba, sasa kunahitajika teknolojia ya usaidizi wa waamuzi kwa njia ya video yaani VAR.

Sababu yao kubwa ni kwamba, wanahitaji maamuzi sahihi kutoka kwa waamuzi hao ili mwenye haki ya kushinda asipokonywe.

Kama kuna kitu katika siku za karibuni kimekuwa kikiwaudhi wapenzi wa michezo ni waamuzi, hususan wa soka kutoa maamuzi yenye utata.

Ingawa tunaamini kwamba maamuzi tata yamekuwapo kwenye michezo mingi hata ya ligi za madaraja ya chini, lakini yale yanayofuatiliwa sana na kuzua mjadala ni yanayohusu klabu kubwa na zenye wapenzi wengi za Yanga, Simba na Azam.

Kuamua vibaya ni kunyima haki kwani asiyestahili ananufaika na maamuzi ya hovyo huku mwingine akiumia.

Wachambuzi wa soka wamekuwa wakionesha kwamba matukio ya waamuzi wetu kushindwa kutafsiri vyema sheria za mchezo, hususan wa soka unaopendwa zaidi nchini inavunja moyo na kuua maendeleo ya mchezo huo nchini.

Tunakubaliana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia aliyesema hivi karibuni kwamba, maamuzi tata yamesababisha kuwapo kwa kilio kikubwa cha kutaka matumizi ya usaidizi wa waamuzi kwa njia ya video (VAR).

Ni kweli kabisa kwamba, waamuzi ni wanadamu kwa hiyo wanaweza kufanya makosa kutokana na uanadamu wao.

Lakini kama alivyosema Karia, kwa nini wanashindwa au kukataa kushirikiana katika kuona matukio yanayofanyika uwanjani kwa sababu wanakuwa zaidi ya mmoja. Kwa nini wanamwachia yule wa katikati hata kama wao wameona tofauti.

Karia alihoji kwamba kuna maamuzi mengine yanafanyika ambayo mwamuzi wa kati hakuona.

Anachokisema Karia ni kwamba, endapo waamuzi watakuwa wanashirikiana kuelezana pale mwamuzi wa katikati anaposhindwa kujua ukweli sawasawa wa kilichotokea na kuuliza wenzake kwa undani, itasaidia sana kupunguza maamuzi yanayoacha maswali na kukatisha tamaa.

Na kama alivyosema Karia, VAR ni gharama kubwa na tukiamini anachosema kwamba anakijua vyema, kupata VAR moja ni Sh bilioni 14.5 na ina kamera 33-38 za aina tofauti tofauti na kwamba hata ukiipata siyo mali yako bali inabaki kuwa mali ya aliyetengeneza.

Pamoja na serikali hivi karibuni kuonesha utayari wa kuwa na VAR, lakini kwa mtazamo wetu tunadhani kipaumbele kikubwa kwa sasa kiwe ni kuboresha viwanja kila mkoa na kushuka hadi kila wilaya kabla ya kukimbilia huko.

Tumeshuhudia mechi za ligi kuu zikichezewa katika viwanja ambavyo kwakweli hata kama vimeidhinishwa, bado vinachangia matokeo yasiyotarajiwa hasa kunaponyesha mvua.

Ni kwa mantiki hiyo tunahimiza waamuzi kujitahidi kuwa waadilifu na kutenda haki, lakini kupokea ushauri wa Karia wa kufanya ushirikiano kwenye maamuzi.

Lakini tunadhani bado mamlaka za juu zinapaswa kutoa adhabu kali zaidi kwa mwamuzi anayevurunda na hasa anaposhindwa kutafuta ushauri wa wenzake au anayeonekana dhahiri uwezo wake ni mdogo katika kutafsiri sheria 17 za soka.