Kesho Simba, wawakilishi pekee wa Tanzania na Afrika Mashariki waliobakia kwenye mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), itashuka dimbani Benin kuvaana na Asec Mimosas katika mchezo wa Kundi D.
Asec Mimosas ya Ivory Coast inachezea mechi zake Benin kutokana na viwanja vya nchini kwake kuwa kwenye maboresho ya kuelekea fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Simba ambayo inaonekana imeimarika na ina uzoefu wa kushiriki mashindano ya kimataifa sasa imeanza kufanya michakato yake kwa kuzingatia mahitaji ambayo hukutana nayo kwenye michuano hiyo ya CAF.
Ni kama vile unaweza kusema tayari Simba imeanza kujipambanua na klabu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na namna inavyojiendesha licha ya baadhi kutamba zinafanya shughuli zake kwa weledi.
Kwa kawaida dirisha la usajili huanza baada ya kukamilika msimu na dirisha hilo huhusisha timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championsip (zamani Ligi Daraja la Kwanza), First League (Ligi Daraja la Pili) na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, na hufunguliwa rasmi baada ya kutangazwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF).
Wakati sasa hata dirisha dogo la usajili ambalo hutoa nafasi kwa klabu kuongeza nguvu na kuimarisha vikosi vyake kutokana na mapungufu waliyoyabaini katika mechi za mzunguko wa kwanza ikiwa imemalizika, lakini tayari tunasikia Simba imeshakamilisha baadhi ya usajili wa nyota wake wapya wa kimataifa.
Lakini pia wachezaji wengine wa kigeni wakiwa kwenye hatua nzuri za kukamilisha usajili wa kuja nchini kujiunga na Simba kwa ajili ya msimu ujao, bado klabu nyingine zikiwa zimelala au zinaendelea na mikakati ya kuwania ubingwa huku wengine wakipambana kujinasua kushuka daraja.
Hatua ambayo Simba imefikia, inapaswa kuigwa na timu nyingine kwa ajili ya kuimarisha timu zao kwa maslahi ya kuendelea kuifanya Ligi Kuu Tanzania Bara iwe imara, lakini pia kujiweka tayari kukabiliana na ushindani kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Kitendo cha kuanza mchakato wa usajili mapema na kwa kuangalia wachezaji walioko kwenye ligi kitasaidia kupata nyota wenye uwezo na kutawaepusha kusajili wachezaji wa majaribio ambao kwa kiasi fulani huzigharimu timu kwa kuwasubiri viwango vyao kurejea katika ushindani.
Timu zitakazofanya mchakato wa usajili mapema na kwa utulivu, hakika zitajiweka kwenye nafasi ya kufanya vizuri katika msimu ujao na kuacha kugombania mchezaji mmoja kama ilivyozoeleka.
Jambo zuri huigwa, Yanga, Azam, Namungo, DTB inayofanya vizuri katika Ligi ya Championship na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara amkeni sasa kwa kuanza kuufikiria msimu ujao na kuacha kufanya usajili wa zimamoto zikiwa zimesalia siku chake, kuanza mazungumzo ya awali na wachezaji ni uamuzi sahihi kwa sababu utatoa nafasi kwa makocha kuwafuatilia ili kuridhishwa na viwango vyao.
Ingawa bado msimu haujamalizika, lakini kwa kiwango kikubwa kila timu imeshafahamu mahitaji yake halisi kuelekea msimu mpya, ni ukweli usiofichika timu itakayokuwa kwenye nafasi ya kufanya vizuri ni ile itakayokuwa ilifanya usajili bora na ilipata maandalizi sahihi wakati wa Pre Season.
Nipashe inazikumbusha timu zote kubadili mfumo wa utendaji wake kazi kwa kubadilika na kufuata mahitaji halisi ya soka la sasa ambapo usajili wa zimamoto kamwe hautawafikisha kwenye mafanikio.
Kama Simba imeanza, basi timu nyingine hazijachelewa, muda unaruhusu kwa kuanza kusaka wachezaji watakaowasaidia na hatimaye itawapunguzia gharama ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha pale ambapo itaonekana mchezaji huyo amekuwa lulu, lakini itaifanya Tanzania kuwa na wawakilishi imara kwenye michuano ya CAF.










