Mafao sawa, kiporo kikokotoo kipashwe moto

15Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mafao sawa, kiporo kikokotoo kipashwe moto

JUZI Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemevu), Prof. Joyce Ndalichako, akieleza baadhi ya mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, madarakani kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), alisema umelipa mafao yenye thamani ....

ya Sh. trilioni 1.15.

Mafao hayo yamelipwa kwa wastaafu na wategemezi 51,079, huku Sh. bilioni 692.38 za pensheni ya kila mwezi, sawa na wastani wa Sh. bilioni 57.7 kila mwezi kwa wastaafu 147,459.

Hii ni habari njema kwa wastaafu na wategemezi ambao kwa mujibu wa sheria ya hifadhi ya jamii wanastahili kulipwa wanapotimiza vigezo vyote muhimu, lakini kumekuwa na ucheleweshaji kwa sababu ambazo mara nyingi hazijawekwa wazi.

Kilio kimekuwapo pia kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa watu kuchelewa kulipwa mafao yao hasa wastaafu na fao la ukosefu wa ajira, jambo ambalo limesababisha wengi kuishi maisha magumu.

Tunapongeza jitihada zilizofanyika kuhakikisha deni la PSSSF linalipwa, kwasasa hatutarajii kusikia kilio cha wastaafu kukosa mafao kwa wakati, kwa kuwa wapo waliosota kwa miaka mitatu bila kupata stahili zao, huku pensheni ya mwezi ikichelewa.

Hivi karibuni, Bunge liliitaka serikali kuweka mikakati madhubuti kulipa madeni kwenye mifuko hiyo, huku wakipongeza kupungua kwa deni la PSSSF, lakini kuitaka mifuko kulipa mafao kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ikiwasilisha taarifa ya mwaka 2020/21 ilibaini kuwapo kwa madeni, na kwamba hadi Juni 30, mwaka 2020 deni la serikali la NSSF lilikuwa kiasi cha Sh. trilioni 1.174 ambalo ni la mwaka 2007 hadi 2021.

Pia, Mfuko wa Taifawa Bima ya Afya (NHIF), unaidai serikali zaidi ya Sh. bilioni 209.70, hali inayopunguza ufanisi wa mfuko husika na kuyharibu mizania ya fedha kinyume na Kanuni za Kimataifa za Uaandaaji wa Hesabu.

Mara kadhaa wabunge wametaka kujua hatua zilizofikiwa kwenye utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018, iliyounganisha mifugo na kupata PSSSF, ambayo ilileta kikokotoo chenye usawa baina ya mifuko husika.

Desemba 28, mwaka 2018, aliyekuwa Rais Hayati John Magufuli, aliagiza mifuko kurudi kwenye utaratibu wa awali wa utoaji mafao yaani NSSF kutumia asilimia 25 kukokotoa mafao na pensheni ya mwezi, huku PSSSF wakitumia asilimia 50 hadi mwaka 2023.

Asilimia 25 maana yake ni mtu anapostaafu akipigiwa hesabu ya jumla ya kiasi anachostahiki kukipata, mafao ya mkupuo ni asilimia 25 na asilimia 75 inayobakia kwenye mfuko ataendelea kulipwa kama pensheni ya mwezi hadi atakapofariki.

Asilimia 50 maana yake mstaafu anapata kiasi hicho kutokana kwenye jumla kuu, huku akipata asilimia 50 nyingine kama pensheni kwa maisha yake yote.

Iliyokuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA), ilisema lengo la kuwa na kikokotoo kipya ni kuleta usawa kwa mifuko yote kwa kuwa watumishi wa umma walikuwa wakilipwa mafao ya mkupuo mengi (asilimia 50) huku wa sekta binafsi wanaohudumiwa na NSSF wakilipwa asilimia 25.

Pia, walisema kwa mfuko kulipa asilimia 50 ulilemewa kiasi cha kushindwa kuwahudumia wanachama wake na jitihada hizo zilifanyika, ili kuokoa kushindwa kujiendesha kabisa.

Pamoja na mafanikio hayo, lakini bado kuna jambo ambalo ni kiporo linalohitaji majadiliano ya wadau kuhakikisha mifuko inalipa mafao kwa wakati na kuendelea kujiendesha.