Mwaka mmoja wa Rais Samia kaliheshimisha soka wanawake

14Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mwaka mmoja wa Rais Samia kaliheshimisha soka wanawake

ILIKUWA ni miezi takriban saba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, pale kikosi cha Timu ya Wanawake Twiga Stars kilipotwaa Kombe la Shirikisho la Soka Ukanda wa Kusini mwa Afrika (COSAFA).

Twiga Stars ilikwenda kama mgeni mwalikwa, kwani Tanzania au Shirikisho la Soka nchini (TFF), halipo kwenye Ukanda wa COSAFA.

Kinadada wa Tanzania walifanya vema kwa kutoa vichapo kwa timu za Namibia, Botswana, Malawi, Afrika Kusini hadi ikatwaa kombe hilo. Ilikuwa ni dalili nzuri ya kuanza kung'aa kwa soka la wanawake nchini ambalo huko mwanzo lilionekana ni kama la kujifurahisha tu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu, Somoe Ng'itu, anasema kuwa awali mpira wa miguu wa kinamama ulionekana kama ni mchezo wa kupoteza muda, na waliocheza walionekana kuwa ni wahuni waliokosa kazi, lakini kwa sasa hali imebadilika kabisa kwani wachezaji wameanza kuheshimika.

Hiyo ndiyo dhana kubwa iliyojengwa na wengi na ilisababisha wazazi na walezi wengi kuwakataza mabinti zao kucheza mchezo huo kwa kuona kuwa hautowasaidia chochote, zaidi ya kuwaharibu tu.

Mwezi huo huo wa Oktoba mwaka jana, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwaita Ikulu, ambapo pamoja na kupata nao chakula, lakini kuwapongeza kwa kazi kubwa walioifanya si kwa kuleta kombe nchini, lakini kuitangaza nchi kwa ujumla.

Rais alilipokea kombe hilo, lakini naye aliagiza mabinti hao kupewa viwanja.

Machi 19, Rais Samia anatimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani. Lakini kwa muda mfupi tu alioingia, ameufanya mpira wa miguu kwa kinamama kuthaminiwa na kuheshimika.

Mzazi yeyote yule ambaye hapo awali alikuwa akimkataza binti yake asicheze soka kwa madai ni mchezo wa kihuni, halafu akaona tukio lile la mabinti za wenzake wakiwa Ikulu pamoja na mheshimiwa Rais, ni lazima atakuwa alijisikia vibaya.

Kama alisikia Rais akitangaza mabinti wake wapatiwe viwanja, atajuta juu ya uamuzi wake alioufanya. Na wale wote ambao walikuwa wanabezwa na wazazi wenzao kwa kuwaacha watoto wao wa kike kujitumbukiza kwenye soka, sasa wao ndiyo wanaanza kutamba.

Kwa kifupi, Rais ameliheshimisha soka la wanawake na kuonekana ni mchezo kama mingine ambayo inaweza kumfanya mtoto wa kike kupata kipato kitakachomwezesha kuishi bila kumtegemea mtu mwingine, kusaidia wazazi wake, kufahamika, lakini kufika nchi mbalimbali na maeneo ambayo hata mzazi hakuota kufika, ikiwamo Ikulu.

Nadhani kwa hali ile na ilivyo sasa mwaka mmoja tu wa uongozi wa Rais Samia, kuna wazazi wameshaanza kubadilisha mitazamo yao, kwani soka la wanawake limekuwa juu kwa sasa, na hata mashabiki wa soka la wanaume nao, wameshaanza kuanza kulifuatilia.

Tuliona mechi kati ya Simba na Yanga kwenye miezi kadhaa nyuma, ikiwa ni ya Ligi Kuu ya Wanawake jinsi mashabiki walivyojitokeza kwa wingi wakishangilia mithili ya timu za wanaume.

Na baadhi ya mechi za Ligi Kuu zimeanza kuonyeshwa laivu, zikivutia watu wengi.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wilfred Kidao, anasema kuwa kipindi kifupi tu cha Rais Samia kuwapo madarakani, Ligi Kuu ya Wanawake si tu imepanda hadhi, lakini imeanza kuwa ya kulipwa, huku wachezaji mbalimbali kutoka nje ya nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ghana, Burundi, Nigeria, wakija nchini kujiunga na klabu mbalimbali kwa sababu imeanza kuwa na maslahi.

Ukiongea na baadhi ya wachezaji wa kike, wanakwambia kuwa tofauti na zamani, kwa sasa soka la kinamama limeanza kuwalipa, kwani wanalipwa posho na mishahara mizuri na wengine wameshaanza kuwajengea wazazi wao nyumba, pia wao wenyewe kuwawezesha kuishi kwa kazi hiyo tu ya soka, tofauti na zamani.