Mbinu hii kukomesha ukatili wa kijinsia ilivyo ya kipekee

08Mar 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mbinu hii kukomesha ukatili wa kijinsia ilivyo ya kipekee

LENGO namba nne la Kimataifa la Maendeleo Endelevu (SDGs), linagusia usawa wa kielimu, likitaka kuwapo kwa fursa sawa kwa makundi yote kuipata haki hiyo.

Kadhalika lengo la tano linahimiza usawa wa kijinsia. Kwa ujumla yanatetea ustawi na hatima njema ya mwanamke.
Wadau mbalimbali kwa kushirikiana na serikali wanajitahidi kutekeleza malengo hayo.

Kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni, jijini Dar es Salaam au Sauti ya Jamii, ni miongoni mwa wadau hao, ambao ili kufikia usawa katika elimu kwa kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia, wanatoa mafunzo na huduma.

Ukeketaji, mimba za utotoni na ndoa za utotoni ni miongoni mwa vitendo ambavyo vinapigwa vita kwa kukamata wanaovisababisha, lakini elimu inatolewa kwa jamii ili kuachana na vitendo hivyo.

Kituo hicho kinatoa elimu ya kupinga vitendo hivyo, katika familia, jamii na hata shuleni maeneo ya Kipunguni, kuokoa mabinti ambapo baadhi yao wamepewa mafunzo ya ufundi bure kwa lengo la kuwawezesha kujitegemea.

Taarifa ya kituo hicho inayotolewa kuhusu mafanikio ya kukabiliana na unyanyasaji huo, wakati Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima, anapotembelea Sauti ya Jamii, inamvutia.

Anaagiza kufanyiwa makala maalumu kwa ajili ya kusambazwa ili kuigwa na wadau wengine wanaofanya kampeni kama hizo.

Ni katika ziara yake hivi karibuni kwenye kata ya Kipunguni akihamasisha watu kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani na kupewa taarifa za maendeleo ya kituo hicho.

Taarifa hiyo iliyosomwa na mwenyekiti wa kituo, Fatma Talib, inaonyesha jinsi ambavyo mafunzo ya ufundi kwa watoto wa kike waliokimbia ukatili na kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia shuleni na majumbani yalivyoleta tija, jambo linalomkuna zaidi Waziri Gwajima.

Mwenyekiti huyo anasema, tangu kianze kutoa mafunzo ya ufundi cherehani bure mwaka 2016, kimesaidia wasichana 360 waliokimbia ukeketaji kutoka nyumbani kwao ambao sasa wanajitegemea.

Mbali na ufundi chereheni mafunzo mengine ni ya saluni na ujasiriamali kwa wanawake walioacha ungariba ambao pia wamepewa mbegu na vitalu ili kulima mboga za majani na kuziuza katika masoko mbalimbali.

Fatma anasema, kituo hicho kiko chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), huku kikisaidiwa na baadhi ya wadau kama Women's Legal Aid Centre (WILAC), Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNIFPA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Women Fund Tanzania (WFT)na Timiza, Binti Makini.

Hatua ya kumnyima elimu mtoto wa kike au wa kiume, ni miongoni mwa vitendo ambavyo huchukuliwa kama ukatili wa kijinsia, ambao kituo hicho kinapambana nao kwa kuelimisha jamii ili ibadilike.

Kimsingi, juhudi zinazofanywa na kituo hicho, ni vyema zikaungwa mkono na wadau wote wanaopenda maendeleo ya mtoto wa kike ili kukomesha vitendo vyote vinavyomkwamisha.

Juhudi hizo zikipewa kipaumbele na jamii, ninaamini kuwa kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu isemayo; 'Kizazi cha Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu inaweza kuzaa matunda.

Kaulimbiu hiyo pia inamalizia kwa kuhamasisha jamii kujitokeza kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu. Lakini binafsi ninataka kukazia zaidi suala la usawa wa kijinsia kwenye elimu.

Usawa katika elimu ni muhimu, lakini usawa huo huanzia nyumbani, kwa lengo la ufikiaji wa elimu kwa wasichana na wanawake, hivyo ni vyema jamii ikashiriki kikamilifu kuhakikisha jinsi zote zinapata elimu kwa usawa.

Wazazi na walezi ni muhimu watambue majukumu wanayowapa watoto wao na maadili wanayowasilisha kwao kwa kuelimisha kuhusu usawa wa kijinsia ikiwamo kuwafahamisha kuwa wote wana haki sawa katika kupata elimu.

Ni vyema wanawake wanapoadhimisha siku hii, waangalie uwezekano wa kuongeza vituo vingi zaidi kama hicho cha Kipunguni, ili elimu ya kukomesha vitendo hivyo usamba kote nchini hasa maeneo ya pembezoni.