Hili la nyavu haramu Victoria wengi tumo, sasa tujitathmini

10Mar 2022
Anthony Gervas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hili la nyavu haramu Victoria wengi tumo, sasa tujitathmini

SEKTA ya uvuvi ni muhimu katika ustawi wa jamii, lakini ni ‘pasua kichwa’ kwa serikali, kutokana na kuwapo uvuvi haramu unaofanyika kila mara, kwa kutumia zana zilizozuiliwa na sheria.

Katika kurunzi langu leo namulika swali kwanini uvuvi haramu unaendelea kuwapo, wakati serikali inazipiga marufuku zana zile kutumika.

Najiuliza hilo litakoma lini? Ni kwa sababu kila mara utasikia, wamekamatwa watu kadhaa nyavu zile zimechomwa moto. Ni hali inayozidi kudumu na hatujui kitendawili hicho kitatenguliwa lini.

Binafsi nauliza shida hiyo itakomeshwa lini na serikali? Au kitendawili hicho kitatenguliwa lini, kimsingi unasababisha kuharibu mazalia ya samaki na kuua walio wadogo chini.

Swali la kujiuliza inakuwaje wavuvi haramu wanaendelea kusikika kila kukicha wakati wahusika wanatajwa walewale, watendaji wanaowajibika moja kwa moja kudhibiti hali hiyo iwe katika maeneo ya mialo au ziwani wanabaki kuwa wale wale? Ina maana waharibifu hawajulikani?

Kama wanajulikana, ninadadisi ina maana hakuna namna ya wahusika ama kukamatwa au kuchukuliwa hatua na kama wana maduka yanayohusiana na kashfa hizo, haifiki hatua hata ikibidi leseni za biashara hizo husika hazichukuliwi?

Wavuvi nao kama adhabu wanazopewa hazitoshi kuwarekebisha, nadhani hatua zaidi zinafaa inapobidi kwa mujibu wa mazingira yaliyoko au yanayotumika na wakati husika.

Nitoe mfano wa mahali niliko katika mkoa wa Mwanza na hata mingineyo inayozungukwa na Ziwa Victoria, utasikia kila mara maofisa wa serikali wamekamata wavuvi haramu, wakawanyang’anya nyavu hizo zikiwamo makokoro na kisha zinachomwa moto, lakini baada ya miezi kadhaa mambo ni yale yale kama vile hakujatokea kitu.

Ukiwafuatilia wananchi na wavuvi hao wanadai baadhi ya watendaji wa vijiji, kata na hata wilaya wasiokuwa waaminifu wanakuwa sehemu ya kujihusisha kwa namna mmoja au nyingine hata wakaruhusu mianya kufanyika, simulizi ya uvuvi haramu kuwa endelevu.

Nyavu zile hutumika nyakati za usiku tu kuvulia samaki, lakini maofisa uvuvi au watendaji unapoongea nao kama mwandishi wa habari utasikia wanasema umepungua kiasi kikubwa, wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha doria zao zinafanyika kuwasaka wahalifu wa aina hiyo.

Lakini, cha ajabu zikipita siku chache wavuvi wale wale wanaendelea kuvua wakitumia zana zilezile, hivi wanakuwa wanamdanganya nani maneno yao matamu? Kwanza samaki hawakui.

Nitoe mfano hai aina ya sangara. Pili, niseme wanaua mayai ya samaki wengi kutokana na kuharibu mazalia yao. Binafsi watendaji na wahusika wengine mnaosimamia na kudhibiti hayo acheni, nawasihi mfumbue macho.

Inafaa kuona mnachoma nyavu za mfano na moto wa kampeni uwashwe hasa na haifai hata kidogo kinyume na hapo. Kama kuna nyavu zimefichwa na wahusika, ili baadaye waendelee kuzitumia, kwa namna yoyote ile haitakuwa haki kwa umma.

Huwa tunasikia na kuona sana kutoka kwa mamlaka zetu, tukisikia ''oooh samaki wamepungua sana ziwani, hivyo tufunge ziwa miezi kadhaa ili samaki wazaliane kwanza!” Kumbe chanzo ni makokolo, nyavu za buibui, timba na nyinginezo ambazo ni haramu kutumika.

Wahusika jamani, sisi wananchi tunafuatilia kubaini kitu gani kinaendelea. Dhambi hiyo itawatafuna siku moja, mayai ya samaki yanavuliwa na zana ya kumbakumba ambayo ni kokolo. Enyi ikiwa ni kweli mnajihusisha na dhambi hiyo, watendaji wa vijiji, kata, wilaya na wengine zote kwa nafasi tijitathmini.

Nyavu zinazoruhusiwa kuvulia zinatajwa kuwa za ukubwa wa nchi tano hadi sita, lakini wavuvi hao wenye zana haramu wanasemekana wana mbinu nyingi za kuficha nyavu hizo ikiwamo kuchimbia chini ya mchanga au ardhi ili wasitiwe nguvuni.

Tunapaswa kila mmoja wetu wananchi kufuatilia na kuchukua hatua tukishirikiana na serikali kuondoa changamoto, ikibidi iwekwe adhabu kali ya kifungo kwa wale wanaopuuza sheria na kusababisha kubakia kama kitendawili kisichoteguka kwa serikali siku zote.