Hili la Mshery, fundisho klabu kutosajili kizamani

05Mar 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hili la Mshery, fundisho klabu kutosajili kizamani

NAKUMBUKA miaka mingi nyuma, mzee mmoja ambaye nina undugu naye, mkazi wa Tabata alimwita kijana wake na kumpa eneo la uwanja nyuma ya nyumba yake na kumtaka ajenge.

Wakati huo eneo hilo lilikuwa bado baadhi ya maeneo ni mapori. Ilikuwa haijachangamka kama ilivyo sasa. Kijana akakataa na kumwambia baba yake hawezi kuchukua eneo hilo hivi hivi bila ya kuandikishiana. Mzee huyo alikasirika na kumuuliza ina maana hamwamini yeye baba yake, anaogopa kuja kumgeuka?

Kijana akamjibu baba yake kuwa dunia ya sasa siyo kama ile ya zamani waliyoishi wao ambapo watu walikuwa na utu, kuheshimiana, pamoja na uaminifu uliopitiliza.

Akamwambia tatizo siyo yeye, ila wadogo zake ambao bado wadogo wakiwa wakubwa na kugundua kuwa alipewa eneo la uwanja bila maandishi, inaweza kumletea matatizo. Kwa shingo upande mzee akakubali kuandikishana na kijana wake.

Miaka ikaenda, mzee akaanza kuugua. Kabla hata hajafa, alishuhudia mgogoro au ugomvi kwa kijana wake mkubwa dhidi ya wadogo zake, wakidai eneo alilojenga nyumba ni la familia, na baba yao alimpa kwa mdomo bila maandishi yoyote.

Kabla ya kufariki, mzee aliwaita wote na akawaonyesha nyaraka zote zinazoonyesha waliandikishiana na hakumpa kwa maneno. Ndipo watoto hao walipoamini na kutulia. Baada ya muda mzee akafariki.

Kisa hiki kifupi nimekitoa hapa kuonyesha imefikia wakati dunia ya sasa hata wanandugu wenyewe hawaaminiani na wanageukana, achilia mbali watu baki.

Miaka ya nyuma walikuwa wakiishi kwa kuaminiana, na walikuwa waaminifu.

Mtu anaweza kumpa mwenzake kitu cha thamani na asimgeuke. Wengi walikuwa wanawashangaa wazungu au watu wa nje kila kitu wanafanya kazi ya kuandikishiana. Kumbe wao walishatoka zamani kwenye maisha yale. Waliyaishi zamani na wakawa wameingia kwenye maisha ya kila mmoja kujitazama yeye maisha ya ubinafsi.

Ndiyo maana kwa sasa kila kitu kinakwenda kwenye maandishi na mikataba. Hata kwa mtu ambaye unamwamini kupita kiasi.

Majuzi kuliibuka taarifa za klabu ya Mtibwa Sugar kulalamika kutolipwa fedha zake za usajili kwa ajili ya aliyekuwa mchezaji wao golikipa, Aboutwalib Mshery. Kupitia kwa msemaji wao, Thobias Kifaru alisema walikuwa hawajapewa malipo yao, licha ya kwamba walisaini kukubali mchezaji huyo aondoke.

Hapa ndipo niliposhangaa sana. Hivi hadi leo karne hii, bado kuna klabu inauza mchezaji kwa mali kauli?

Na sidhani kama Mtibwa Sugar waliweka kipengele wasipolipwa fedha hiyo hadi siku fulani basi mkataba huo utakuwa batili, au watakuwa walikiuka kanuni.

Sifikiri kama waliweka kwa sababu kama ni hivyo, wala wasingekuwa na tabu ya kupiga kelele katika vyombo vya habari.
Kilichotokea tu ni kwamba Mtibwa Suagr iliamua kupiga kelele ili kuonewa huruma, au kuifanya Yanga ione aibu na kulipa fedha hiyo ya usajili.

Kwanza nilishangaa kwa klabu kubwa kama Yanga ambayo ilikuwa na uhitaji zaidi wa mchezaji kutoipa Mtibwa Sugar pesa za kipa huyo, kwani kipa wake Djigui Diara alikuwa amekwenda Cameroon kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2022), lakini mshangao wangu zaidi ni pale Wakatamiwa hao kushindwa kutumia fursa hiyo kupiga pesa ya haraka na badala yake wakamtoa kwa mali kauli, wakati wao wenyewe wanamhitaji.

Dunia ya leo, si kwenye soka, au maisha ya kawaida, hakuna kitu kama hicho, watu kwa sasa hawaaminiani. Hakuna maisha ya kijamaa tena kama yale ya zamani.

Kama hamkuandikishana, mtu anaweza kukuruka hivi hivi huku anakujua, na ushahidi kukawa hakuna.

Kwa hili lililotokea, liwe funzo kwa klabu zote nchini biashara ya wachezaji ndiyo kubwa zaidi kwa klabu zote dunaini. Inashangaza kuona klabu inakubali mchezaji aondoke ikiwa haijalipwa chochote kile. Cha kushangaza ni kwamba hakuna maandishi yoyote yanayowafunga waliomchukua.

Klabu za Ligi Kuu au nyingine zisionyeshe unyonge linapokuja suala ya klabu kubwa kutaka kusajili wachezaji wao wanapokuwa kwenye mikataba kwa kukubali kila wanachoambiwa.

Pigeni pesa, kama watakupa robo, nusu, au nusu na robo, andikishianeni zilizobaki zitalipwa lini na zisipolipwa nini kifanyike. Zikiendelea kufanya biashara 'kishikaji' zitaendelea kuumia au kusubiri huruma ya kelele za waandishi wa habari na wachambuzi.