Tutengeneze umeme bila kuuzima kwanza

03Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tutengeneze umeme bila kuuzima kwanza

SEHEMU kubwa ya Tanzania kwa sasa inakumbana na athari za kukatika kwa umeme kutokana na mgawo uliotangazwa na serikali, ambao utachukua siku 10.

Katika utekelezaji huo, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Jumatatu lilitoa ratiba ya mgawo wa umeme kuanzia juzi hadi Februari 10, mwaka huu, ambapo mikoa 19 ya shirika hilo imetajwa, huku nishati hiyo ikikosekana kwa saa 16 kwa siku kuanzia saa 02 asubuhi hadi saa 06 usiku.

Hata hivyo, wakati wakazi wa maeneo ya mikoa ya TANESCO ambayo itaathirika ni Dar es Salaam (Temeke, Kinondoni na Ilala), Kilimanjaro na wilaya zake, Arusha, Mara, Mbeya, Manyara, Njombe, Morogoro, Mwanza, Singida, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Tanga, Tabora, Dodoma, Songwe, Iringa na Geita, mgawo huo, maeneo nyeti kama ya Jeshi na hospitali hayataguswa.

Mikoa ya TANESCO ambayo haitaathirika kwa mgawo ni Bukoba, Katavi, Kigoma, Lindi, Mtwara, Pemba Kaskazini na Kusini, Rukwa, Simiyu, Zanzibar, Unguja Kaskazini na Magharibi.

Lengo la kufanyia matengenezo miundombinu ya umeme ni zuri na linakubaliwa na kila mmoja, kwa kuwa ni kuiboresha, hivyo kuongeza ubora wa huduma kwa watumiaji wa nishati hiyo.

Jumatatu ikiwa siku moja kabla ya mgawo huo kuanza juzi ambao unachukua saa 16 kwa siku kwa mujibu wa ratiba ya shirika, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande, alitembelea kituo cha kupozea umeme cha Kunduchi mkoani Dar es Salaam na kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala la kukatika kwa umeme katika maeneo yaliyoorodhesha, akisema kwamba hakuna eneo umeme utakatika kwa siku tatu mfululizo.

Alisema wanaendelea na maboresho na kwamba wamejipanga kujua matatizo, majawabu yake na kuwa na mipango ya kuitatua. Alieleza kuwa Tanzania nzima wanajua kila mahali tatizo ni nini, majawabu ni nini na tarehe ya kuyatatua ni lini, hivyo kwa sasa wapo kazini kutekeleza.

Kwamba katika zoezi la kuongeza mitambo ya uzalishaji wa umeme, kutakuwa na uhitaji wa gesi zaidi, akifafanua kuwa hilo linalazimu maboresho kufanyika katika visima vya gesi.

Kwa mujibu wa Chande, wakati maboresho hayo yanafanyika, watatumia siku 10 kufanya uboreshaji wa miundombinu ya umeme, huku akieleza kuwa hilo litasababisha umeme kukatwa kwa baadhi ya maeneo na siyo nchi nzima kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakisema.

Pamoja na mgawo kukusudia kufanyia marekebisho miundombinu, tunaona kuwa utaathiri kwa kiwango kikubwa watumiaji hususani watu waliojiajiri kwenye sekta binafsi ambao hujishughulisha na kuuza vinywaji baridi, kushona nguo, kuchomelea vyuma na nyingine ambazo hutegemea umeme.

Tunaishauri TANESCO kutafuta majawabu kuhusiana na lipi lifanyike ili nchi yetu iondokane na adha ya kukatikakatika kwa nishati hiyo au mgawo kila uchao. Moja ya ufumbuzi wa tatizo hili ni kuanza kutumia teknolojia ya kufanya matengenezo ya umeme bila kuzima umeme.

Teknolojia hii imeshaanza kutumika katika nchi kadhaa barani Afriuka, na jambo la kujivunia ni kwamba Tanzania ina mtaalamu mzawa Mcdonald Liveline Technology LTD 123 Tanzania, ambaye katika miaka ya nyuma aliwahi kufanyakazi na TANESCO.

Mtaalamu huyo amekuwa akitoa mafunzo na kufanyakazi katika nchi kadhaa za Afrika kama Ghana, Zambia, Botswana na nyingine za kufanya matengenezo ya umeme kama kuhamisha nguzo, kukata miti bila kuzima umeme, hatua inayosababishia umeme watumiaji na taifa kwa ujumla. Kwa nini tusiwaamini, kuwathamini na kuwatumia wataalamu wetu kama huyo badala ya kutumiwa na kuzinufaisha nchi zingine?

Tunaamini kwa kuwa serikali yetu ni sikivu, viongozi wakuu wa TANESCO na Wizara ya Nishati chini ya Waziri January Makamba, watauchukua ushauri wetu na kuufanyia kazi, ili kuwaondolea Watanzania kadhia ya kukatikakatika umeme na kuwaathiri.