Tunampongeza sana Dk. Tulia kwa kuchaguliwa kuongoza moja ya mihimili mitatu inayounda dola na tunamtakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu hayo mapya.
Hakuna anayeweza kuhoji au kutilia shaka uwezo na weledi, uadilifu wala uzoefu alionao Spika huyo mpya. Hizo ndizo sababu zilizomfanya apitishwe katika ngazi zote za uteuzi, kuanzia Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kamati ya Wabunge wa CCM kisha kuchaguliwa na Bunge zina jana.
Hili linadhihirishwa na Dk. Tulia kupitishwa na Kamati Kuu ya CCM pekee licha ya wanachama zaidi ya 70 kujitokeza kuomba kugombea nafasi hiyo, wengi wakiwa watu wazito na wenye uzoefu wa kutosha.
Kilichodhihirisha zaidi kuwa Spika huyo mwanamke anakubaliwa na wabunge, ni kutokana na jana kumchagua kwa kura zote dhidi ya washindani wake wanane kutoka vyama vya upinzani baada ya kunadi hoja zao mbele ya wabunge.
Mbunge mkongwe kutoka Jimbo la Isimanu, kuliko wote, Willium Lukuvi aliyesimamia uchaguzi huo alimtangaza Dk. Tulia kuwa mshindi kwa kupata kura zote 376 zilizopigwa na wabunge.
Pamoja na pongezi zetu kwake, tunaona kwamba Tulia ana kibarua kikubwa mbele yake kuhakikisha analisimamia Bunge, ambalo mhimili linaundwa na wawakilishi wa wananchi. Majukumu ya Bunge ni kutunga sheria, kufuta sheria zisizofaa pamoja na kuifuatilia na kuisimamia serikali katika utendaji wa shughuli zake za kila siku, zikiwamo wa maendeleo.
Chini ya Dk. Tulia tunatarajia kwamba Bunge halitasita kuhoji ‘madudu’ ambayo litabaini yamefanywa na watendaji wa serikali ngazi zote (Serikali Kuu) na (Serikali za Mitaa) hususani matumizi ya fedha za walipakodi zinazotumika katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hatutarajii Bunge kuacha majukumu yake ya msingi ikiwamo kuihoji serikali badala yake kuwa mtetezi na msemaji wake. Kufanya hivyo ni kukiuka maana ya dhana ya mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili yote mitatu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama).
Kilichotia faraja ni hotuba yake fupi baada ya kuchaguliwa alipoeleza nafasi ya Bunge ambalo ni sauti ya wananchi kwamba mhimili huo ni daraja kati ya serikali na wananchi, na kwamba atatumia nguvu zake kuliongoza kwa umakini ili liwe daraja madhubuti kati ya wananchi na serikali na ataliongoza kuishauri serikali ili kutimiza wajibu wake.
Alisema Bunge litauliza maswali na kuhoji serikali kwa hekima na busara, na kuongeza kuwa watafanya hivyo kwa nia thabiti ili wananchi wapate maendeleo.
Katika miaka ya karibuni, zilianza kuibuka hisia na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kwamba Bunge limeanza kusahau majukumu yake, hivyo kutojisimamia kama mhimili kamili. Kwa kauli ya Tulia tunatarajia kuona maboresho makubwa katika mhimili huo.
Tusingefurahia kushuhudia minyukano isiyo ya lazima iliyokuwa ikionekana kati ya kiti cha Spika na wabunge wa upinzani na wakati mwingine wabunge wa chama tawala na upinzani.
Lingine tunalomwomba Spika Tulia alifanye ni kurejesha Bunge kuonyeshwa mubashara ili wananchi wasikie yanayojadiliwa na wawakilishi wao katika kuwaletea maendeleo kwenye majimbo yao na taifa kwa ujumla. Hii ndio maana ya kuliita Bunge kuwa ni sauti ya wananchi.










