Kozi za FIFA, UEFA, TFF zilete mabadiliko nchini

05Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kozi za FIFA, UEFA, TFF zilete mabadiliko nchini

KATIKA kuhakikisha mpira wa miguu hapa nchini unakuwa na maendeleo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na mashirikishiko ya kimataifa ambayo ni FIFA, UEFA na CAF, wanaendesha kozi na mafunzo mbalimbali hapa nchini.

Mafunzo na kozi hizo zinazofanyika hapa nchini ni za utawala, uamuzi na ukocha katika ngazi mbalimbali.

Tofauti na miaka ya nyuma, tangu uongozi wa Rais wa TFF, Wallace Karia, tumeshuhudia kozi hizo zikifanyika kwa kuleta wakufunzi wa kimataifa kutoka FIFA, UEFA na CAF ili kuwapa elimu stahiki inayotakiwa wadau wanaohusika katika nafasi hizo.

Lengo la TFF kuratibu mafunzo hayo ni kutaka kuona kila mdau katika eneo lake anafanya majukumu yake kwa weledi na hatimaye kupandisha kiwango cha wachezaji wa soka wa Tanzania.

Msingi mwingine wa mafunzo hayo si tu kuboresha uwezo wa wasimamizi hawa wa shughuli za uendeshaji mpira wa miguu kila siku, lakini ni kutaka kuona kasi ya maendeleo ya wadau hawa muhimu katika sekta hii inaendana na mahitaji halisi ya mchezo huu ambao kwa sasa unaendelea kuchezwa kisasa.

Inafahamika wazi ili kufikia mafanikio ambayo mataifa mengine ya Ulaya yalipo au baadhi ya nchi za Afrika ambazo tayari zimepiga hatua, ni ukweli usiofichika ni lazima TFF kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau kuwekeza kwa makocha pamoja na miundombinu.

Kuwekeza katika makocha, waamuzi na viongozi kutasaidia kufanya kazi za mpira wa mguu kuwa nyepesi kwa sababu kamwe hakutakuwa na sintofahamu ambazo mwisho wa msimu, timu husika huvuna matokeo mabaya na 'zigo' anatupiwa kocha au kiongozi aliyekuwa madarakani.

Ni lazima tutumie vyema mafunzo mbalimbali yanayoendeshwa kwa sababu kwa kupata elimu stahiki ya kazi unayofanya, ni wazi mhusika atajiweka sehemu sahihi na kile anachokifanya badala ya kufundisha au kuchezesha mpira kwa kubahatisha.

Tunawakumbusha wale ambao wamesoma kozi hizo, kuyatumia mafunzo yao kwa vitendo na kuacha kuifungia elimu waliyopata kwenye mikoba yao, kwa kufanya hivyo hawatalisaidia taifa kufikia malengo ya nchi kuwa washindani na si washiriki kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa tunayoshiriki.

Endapo wadau wetu watatumia vyema elimu wanazofundishwa na wakufunzi hao kutoka nje, ninaamini hata bajeti ya fedha ya kuhudumia timu za taifa ambayo inatolewa na Rais wa Jamhuri ya Muundano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan inaonekana imepelekwa eneo sahihi.

Zama za kupata mafanikio kwa kutegemea miujiza zimepita, huu ni wakati wa kuona mwanamichezo, klabu au taifa lililowekeza kikamilifu ndilo linafanya vyema kwenye mashindano wanayoshiriki, na ili kufika huko, kila mdau ambaye anashiriki katika mpira wa miguu hapa nchini anatakiwa kuweka weledi katika kila jambo analolifanya.

Mafanikio ya Ujerumani, Brazil au Hispania, yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa kuanzia kwa wazazi, walezi, serikali, makampuni na taasisi zinazofanya kazi kwenye mataifa hayo kwa sababu waliamini uwekezaji wa kweli ndio utawapeleka kwenye ushindi na si vinginevyo.

Unaweza kusema ni jambo dogo kwa wale wasiopenda kuangalia wapi tulikotoka, lakini TFF inatakiwa kupongezwa kwa hatua ambayo Watanzania tumefikia kwa mwamuzi wetu, Frank Komba, kuwa mmoja wa waamuzi wanaochezesha katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambazo zinamalizika hapo kesho huko nchini Cameroon.

Ukiondoa Komba, huko AFCON yuko Mnyarwanda, Salima Mukansanga, ambaye ameweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kupuliza kipenga kwenye michuano hiyo mikubwa, hali ya kuwa Rwanda haijashiriki fainali hizo kama ilivyo Tanzania.

Kama hili limewezekana kwa kupitia mafunzo mbalimbali yanayotolewa hapa nchini, basi waamuzi, makocha na viongozi wetu huu ni wakati wa kujikita kufanya majukumu yenu kwa weledi, hatimaye jina la Tanzania litang'ara katika michuano ya kimataifa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Hakuna kisichowezekana, kikubwa ni kila mdau kuitendea vyema nafasi anayoipata na hatimaye nuru njema itaonekana na heshima ya Tanzania itarejea huku neno 'Kichwa cha Mwendawazimu' litabakia historia.