Mkurugenzi wa bendi hiyo Killer Boy amesema leo kuwa Waluguru Original imeingiza wanamuziki watatu katika mashindano hayo ambayo pia yatakuwa ni ya kusaka bendi bora ya mwaka.
"Bendi yetu atashiriki rapa Greyson Semsekwa, mwimbaji, Amina Remmy ili kuwania tuzo ya mwimbaji bora wa kike, utunzi bora, yupo Kinde Makengele ambaye pia anawania tuzo ya mpiga solo bora," amesema Killer Boy.
Killer amesema, itakuwa ni mara ya kwanza kwa bvendi yake kutoa burudani katika jiji la Mwanza kwa kushirikiana na bendi ya Super Kamanyola ya jijini humo, na kwamba watatumia nafasi hiyo kutambulisha albamu yao.
"Bendi yetu ina albamu iitwayo 'Kikao cha Wahenga', ikiwa na nyimbo kama 'Morogoro Yetu, Mwanzo wa Mapenzi, Cha Kupewa, Ngalile Mwanangu Ndole, Supu na Nataka Nilewe', tunazitambulisha Mwanza" amesema.
Amesema, kushiriki mashindano hayo ni nafasi ya pekee ya bendi hiyo kuonyesha makali yake ili kujipatia mashabiki wengi zaidi nje ya mkoa wa Morogoro ambako imeshajipatia umaarufu mkubwa.
"Tukitoka Mwanza tutajipanga kuandaa wimbo wa kuhamasisha chanjo ya corona, ili Watanzania wengi zaidi wajitokeze kupata huduma hiyo kama ambavyo serikali imekuwa ikihimiza," amesema.










