Mikoa inayosuasua chanjo ya UVIKO-19 iige inayofanya vizuri

01Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mikoa inayosuasua chanjo ya UVIKO-19 iige inayofanya vizuri

MWANZA ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo inatajwa kufanya vizuri katika chanjo ya UVIKO-19, ambapo Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. Ruta Thomas, anataja sababu za mafanikio hayo.

Kwa mujibu wa Dk. Thomas, ushirikishaji wa wadau wote wakiwamo wahudumu wa afya kuanzia ngazi ya jamii na viongozi wa serikali za mitaa, kwa ajili ya uhamasishaji wa chanjo hiyo ni miongoni mwa siri ya mafanikio.

Vilevile, katika jitihada hizo za kufanikisha chanjo, anasema kuna kamati ya amani ya mkoa, ambayo iko chini ya viongozi kutoka madhehebu mbalimbali, inayohimiza amani na upendo, lakini inasaidia kuhamasisha watu kuchanja.

Pamoja na hayo, anasema, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amekuwa akipokea taarifa za kila siku kutoka kila halmashauri ili kujua ni wapi kuna changamoto inayoweza kukwamisha chanjo, ili hatua zichukuliwe haraka.

Mbali na Mwanza mikoa mingine inayotajwa kufanya vizuri katika chanjo, ni Kagera, Mara, Dodoma na Ruvuma, inaonyesha kuwa bado kuna haja ya kuongeza jitihada zaidi ili kufanikisha chanjo hiyo.

Nchi ina mikoa zaidi ya 20, lakini inayotajwa kufanya vizuri ni mitano tu, kwa hali kama hiyo, tunadhani iko haja kwa mikoa ambayo iko nyuma kwenda kujifunza mbinu zilizotumiwa na mikoa ambayo iko juu kwenye chanjo.

Tunashauri hivyo, kwa sababu katika maisha ya kawaida, mbinu za kufanikisha jambo huwa zinatofautiana, hivyo kwenye suala la chanjo inawezekana baadhi ya mikoa ikawa kimbinu zaidi.

Lakini tunadhani kuna haja ya kukumbusha Watanzania kuwa nchi yao si kisiwa kisichofikika, bali ina mwingiliano wa watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo kuchukua tahadhari ni jambo muhimu.

Hata Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anakiri kuwa mwitikio wa kuchanja bado ni mdogo nchini, ingawa matarajio ni kufikia asilimia 60 hadi mwishoni mwa mwaka huu, lakini waliochanja hadi sasa wakiwa ni watu 1,922,019.

Idadi hiyo inatajwa na Waziri Ummy kuwa ni sawa na asilimia 3.3 ya wale waliochanjwa, tangu chanjo zilipoanza kutolewa katikati ya mwaka jana ambazo ni aina ya Moderna, Johnson &Johnson, Pfizer na Synopham.

Njia ambayo tunadhani inaweza kusaidia kufanya vizuri kwenye chanjo ni viongozi wa mikoa ambayo bado iko nyuma kwenda kujifunza kwa wenzao ambao wanatajwa kuwa juu kuhusu mbinu na mikakati waliyoibuni na kuitumia kufikia mafanikio hayo.

Tunajua kuwa chanjo ni hiari, lakini jambo la muhimu la kutambua ni kwamba, Tanzania si kisiwa ambacho hakifikiki, hivyo tunaona kuna umuhimu kwa kila Mtanzania kupata chanjo ili kuwa salama zaidi.

Hivyo, mikoa hiyo inayotajwa kufanya vizuri kwenye chanjo, ingekuwa ni fursa kwa ile ambayo iko nyuma kujifunza mbinu na kwenda kuzitumia, ili wananchi wahamasike na kujitokeza kuchanjwa.

Kwa kufanya hivyo, tunaamini kwamba Watanzania wengi zaidi wanaweza kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu chanjo na kujitokeza kuipata, ili hatimaye lengo lililokusudiwa na serikali kuchanja asilimia 60 liweze kutimia.

Ni miezi sita sasa tangu chanjo ilipozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, lakini idadi ya waliochanjwa bado ni ndogo, hivyo tunaona kuna haja ya kuwakumbusha viongozi kwa mikoa ambayo inaendelea kusuasua katika chanjo, wachukue hatua zitakazowezesha watu wengi kuchanjwa.