TPLB ongezeni makali zaidi kwa waamuzi hawa Ligi Kuu

31Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TPLB ongezeni makali zaidi kwa waamuzi hawa Ligi Kuu

MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa 14 utanza wiki hii baada ya mwishoni mwa wiki kupisha mechi za hatua ya 32 ya michuano ya Kombe la FA, ambayo bingwa huiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Mzunguko wa 14, utaanza wakati Yanga ikiendelea kutesa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 10 zaidi ya Mabingwa Watetezi, Simba wenye alama 25 katika nafasi ya pili ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 msimu huu.

Hata hivyo, ligi hiyo ambayo msimu huu imekuwa ngumu zaidi tofauti na misimu mingi iliyopita, inaendelea huku kilio kikubwa kikielekezwa kwa waamuzi kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu kwa kutokujua, mapenzi binafsi kwa baadhi ya klabu au pengine kwa kurubuniwa ama vinginevyo.

Hata hivyo, wiki iliyopita Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Januari 27, mwaka huu kilipitia mwenendo na matukio mbalimbali na kufanya maamuzi kadhaa ambayo pia yaliwakumba baadhi ya waamuzi.

Waliokumbwa na maamuzi hayo ya Kamati ya TPLB, ni Mwamuzi wa Kati, Hance Mabena kutoka Tanga, ambaye ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitatu kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu kwenye tukio la mchezaji wa Yanga, Djuma Shabani kuchezewa rafu kabla ya kulipiza kwa kumpiga kiwiko, mchezaji wa Polisi Tanzania, Yahaya Mbegu.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu raundi ya 13 uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, pia Mwamuzi Msaidizi namba moja, Pascal Joseph kutoka Shinyanga na mwamuzi wa akiba, Jackson Samweli wa Arusha, wameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitano kwa kosa la kushindwa kumsaidia mwamuzi wa kati, Mabena katika kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu kwenye tukio hilo la Djuma.

Kwa ujumla tunaipongeza TPLB kwa kuchukua hatua hizo ambazo tunaamini itakuwa fundisho kwa waamuzi wengine ambao wanafinyanga sheria za soka na kuziacha timu zingine zikilia kwa kupoteza pointi visivyo halali.

Hata hivyo, tunaitaka TPLB iendeleze wimbi hili kwa kutosita kuchukua adhabu kali zaidi, kwani kwa tukio kama alilolifanya Djuma hadi yeye mwenyewe akajutia pamoja na klabu yake, kabla hata ya adhabu hizo ambapo naye amefungiwa mechi tatu na faini ya shilingi milioni moja, ni dhahiri waamuzi wetu wanapaswa kuchukuliwa hatua kali zaidi kwani kwa kufumbia macho matukio kama haya, ipo siku tutashuhudia madhara makubwa zaidi kwa afya za wachezaji ama hata kupoteza maisha uwanjani.

Nipashe hatutaki kuona madhara makubwa zaidi yakitokea, hivyo njia pekee ya kudhibiti matukio kama hayo ni umakini zaidi kwa waamuzi huku wakichezesha kwa haki, lakini TPLB kutosita kuchukua hatua kali kwa wote wanaofinyanga kanuni/sheria za soka.

Tunaamini TPLB ikiongeza umakini na kutosita kuchukua hatua kali kwa waamuzi wanaovurunda ligi yetu itakuwa bora zaidi na ushindani utaongezeka huku akipatikana bingwa aliyestahili atakayeweza kwenda kutoa ushindani wa kweli kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aidha, hatuna budi kuwasihi waamuzi kuongeza umakini na kutosita kutoa kadi nyekundu hata tatu ama zaidi pale inapolazimika kufanya hivyo kutokana na makosa ya wachezaji uwanjani.

Tunatambua mara nyingi wamekuwa wakilazimika kuongozwa na busara zaidi ama mapenzi yao au vinginevyo badala ya kufuata sheria/kanuni zinazoongoza mpira wa miguu duniani, hivyo kusababisha rafu nyingi zinazoweza kuhatarisha afya za wachezaji, katika hilo tunataka haki itendeke si kutenda tu bali pia ionekane ikitendeka kweli.