WATAJUTA! Simba wasipotwaa ubingwa msimu huu Intro:

08Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
WATAJUTA! Simba wasipotwaa ubingwa msimu huu Intro:
  • *Azam FC ndiyo timu pekee ambayo hadi sasa imeshinda mechi zote za ugenini (nje ya Dar es Salaam) msimu huu.

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliingia raundi ya 18 mwishoni mwa wiki mabingwa watetezi Yanga wakichuana na JKT Ruvu jijini Dar es Salaam huku Simba wakisafiri hadi mjini Shinyanga kuwakabili Kagera Sugar wanaopambana kujinasua kwenye janga la kuporomoka daraja.

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliingia raundi ya 18 mwishoni mwa wiki mabingwa watetezi Yanga wakichuana na JKT Ruvu jijini Dar es Salaam huku Simba wakisafiri hadi mjini Shinyanga kuwakabili Kagera Sugar wanaopambana kujinasua kwenye janga la kuporomoka daraja.
Duru la pili la ligi hiyo msimu limeonekana kuwa na upinzani mkali kulinganishwa na lile la kwanza ambalo Azam FC na Yanga hazikupoteza
Kabla ya kuanza kwa msimu huu wa VPL Septemba 12, Spotika ilifanya mahojiano na makocha wa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo kujua malengo ya kila timu. Timu tatu - Azam, Simba na Yanga zilisema zinapania ubingwa. Mwadui FC, Mbeya City na Mtibwa walisema wanapigania nafasi tatu za juu.
Na kadri ligi inavyoendelea, vita ya ubingwa inaonekana kuwahusisha zaidi Azam, Simba na Yanga huku Mtibwa na Mwadui FC zikionekana 'kufukuza mwizi' kimyakimya.
Lakini ratiba ya VPL msimu inaonekana kuibeba Simba kufanya vizuri kutokana na kupangiwa mechi chache za ugenini mzunguko wa pili ambao rekodi zinaonyesha huwa ni mgumu kwa timu za Dar es Salaam kwa vile timu za mikoani hupambana kuukwepa mstari wa kuporomoka daraja.
Na ratiba nzuri ya mechi za ugenini mzunguko wa kwanza ndiyo imekuwa ikirahisisha kazi kwa timu kutwaa ubingwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya VPL msimu wa 2013/14, Azam FC ilicheza mechi tatu tu nje ya Dar es Salaam mzunguko wa pili. Mechi hizo ambazo ilishinda zote zilikuwa dhidi ya Mgambo Shooting (Tanga), Ruvu Shooting (Mlandizi, Pwani) na Mbeya City FC (Mbeya).
Katika duru la kwanza la VPL msimu huo, Wanalambalamba walicheza mechi sita nje ya jiji hilo zikiwamo tatu za mwanzoni mwa msimu ilizocheza ugenini mfululizo dhidi ya Mtibwa Sugar mkoani Morogoro Agosti 24, 2013, Rhino Rangers FC mjini Tabora Agosti 28, 2013 na Kagera Sugar FC mjini Bukoba Septemba 14, 2013 (baada ya raundi ya pili msimu huo, ligi ilisimama kwa wiki mbili kupisha mechi za kimataifa za Taifa Stars).
Hata kikosi cha Yanga nacho kilipata bahati hiyo ya kuwa na ratiba nzuri ya duru la pili msimu uliopita. Timu hiyo ya Jangwani ilicheza mechi sita nje ya Dar es Salaam mzunguko wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar (Morogoro), Stand United (Shinyanga), Kagera Sugar (Bukoba, Kagera), Police Moro (Morogoro), Coastal Union (Tanga) na Mbeya City (Mbeya).
Ikiwa ni ratiba kama waliyopewa Azam FC msimu wa 2013/14, Yanga inayonolewa na Mdachi Hans van der Pluijm, ilipangiwa ratiba yenye mechi tatu za nje ya jiji hilo mzunguko wa pili msimu uliopita walizoshinda 3-0 dhidi ya Prisons (Mbeya) na 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting (Tanga) kabla ya kupoteza 1-0 dhidi ya Ndanda FC (Mtwara).
Msimu huu bahati ya ratiba nzuria mechi za ugenini imeangukia Msimbazi. Simba ambayo kwa sasa inanolewa na kocha mkuu wa muda Jackson Mayanja ilicheza mechi saba duru la kwanza ambazo ilishinda nne dhidi ya African Sports, Mgambo (zote Tanga), Mbeya City (Mbeya) na Ndanda FC (Mtwara).
Timu hiyo ilipoteza 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons (Mbeya), ikatoka sare mbili za 1-1 dhidi ya Toto Africans (Mwanza) na Mwadui FC (Shinyanga).
Wakati Simba ikikusanya pointi 15 katika mechi saba za nje ya Dar es Salaam duru la kwanza msimu huu, Yanga walicheza mechi tano nje ya jiji hilo na kukusanya pointi 11 wakishinda 2-0 dhidi ya Mtibwa (Morogoro), 2-0 dhidi ya Kagera Sugar (Tabora) na 1-0 dhidi ya African Sports (Tanga) huku wakilazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya Mwadui FC(Shinyanga) suluhu dhidi ya Mgambo JKT jijini Tanga.
Kama ilivyo kawaida ya mzunguko wa pili kuwa mgumu kwa timu za Dar es Salaam (isipokuwa Azam) zinapokuwa mikoani, Yanga imelianza duru la pili kwa kuambulia pointi moja katika mechi mbili ugenini ikichapwa 2-0 dhidi ya Coastal Union jijini Tanga kabla ya sare ya 2-2 dhidi ya Prisons mjini Mbeya.
Timu hiyo ya kocha mkuu Mdachi Hans van der Pluijm bado ina mtihani mgumu kutetea ubingwa wake msimu huu kwani ina mechi nyingine tano za nje ya Dar es Salaam duru la pili dhidi ya Ndanda FC (Mtwara), Majimaji FC (Ruvuma), Stand United (Shinyanga), Mbeya City (Mbeya) na Toto Africans (Mwanza).
Azam FC wana rekodi nzuri ya mechi za mikoani msimu huu wakiwa wameshinda mechi zote sita walizocheza nje ya Uwanja wa Taifa -- 2-0 dhidi ya Stand (Shinyanga), 1-0 dhidi ya Mwadui (Shinyanga), 0-1 dhidi ya Ndanda (0-1), 4-2 dhidi ya JKT Ruvu (Uwanja wa Karume, Dar), 2-1 dhidi ya Majimaji FC (Songea) na 2-1 dhidi ya Mgambo (Tanga).
Kwa mantiki hiyo, kikosi cha Mwingereza Stewart Hall kina mechi saba za nje ya Dar es Salaam duru hili la pili dhidi ya Tanzania Prisons (Mbeya), Coastal Union (Tanga), Mbeya City (Mbeya), Mtibwa Sugar (Manungu, Morogoro), Toto Africans (Mwanza), Kagera Sugar (Shinyanga) na African Sports (Tanga).
Huu ni msimu wa nne bila taji la Ligi Kuu Msimbazi. Ninafikiri timu hiyo ina kila sababu ya kuutumia mwanya huu wa ratiba ngumu kwa wapinzani wake katika mbio za ubingwa, Azam FC na Yanga.
Ninaamini utakuwa mtihani mgumu kwa mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara kumaliza ukame wa mataji ya Ligi Kuu katika misimu ijayo ikiwa watashindwa kuitumia fursa hiyo msimu huu.

AZAM, SIMBA, YANGA NJE YA DAR
MECHI ZIJAZO ZA AZAM
Prisons vs Azam
Coastal vs Azam
M/City vs Azam
Azam vs Mtibwa
Toto vs Azam
Kagera vs Azam
A/Sports vs Azam

SIMBA DURU LA PILI
Kagera vs Simba
Stand vs Simba
Coastal vs Simba
Majimaji vs Simba
Mtibwa vs Simba

YANGA DURU LA PILI
Coastal 2-0 Yanga
Prisons 2-2 Yanga
Ndanda vs Yanga
Majimaji vs Yanga
Stand vs Yanga
M/City vs Yanga
Toto vs Yanga
----------------