Inakuwaje Yanga msimu huu kimataifa?

08Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Inakuwaje Yanga msimu huu kimataifa?

MASHABIKI wa Yanga wana swali moja tu la kujiuliza. Timu yao inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, je kuna matarajio ya kufanya vizuri mwaka huu.

Keshokutwa Jumatano, mabingwa wa Bara watapanda pipa kwenda nchini Mauritus kucheza mechi ya awali ya mchuano hiyo dhidi ya Cercle de Joachim.
Haina rekodi nzuri kwenye michuano ya kimataifa, na hilo ndilo swali la mashabiki wa Yanga.
Hata hivyo, mwenendo mzuri kwenye mechi za nyumbani, kunawapa matumaini kiasi mashabiki.

PLUIJM AFIKIRIA HATUA YA MAKUNDI
Pamoja na kuanza vibaya mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans van der Pluijm aliiambia Spotika kuwa malengo ya awali msimu huu kwenye mashindano hayo ni kucheza hatua a makundi.
Anasema kuwa katika michuano mikubwa kama hiyo timu yake kufuzu kucheza hatua ya makundi ni hatua muhimu na yenye mafanikio zaidi.
"Ili ufike fainali ni lazima upitie hatua ya makundi na kama timu yangu itafika hapo, ni mafanikio makubwa kwetu," alisema Pluijm.
Anachojivunia kocha huyo Mholanzi ni asilimia 80 bora ya usajili wa wachezaji uliofanywa na Yanga msimu huu.
"Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni magumu, klabu nyingi za Afrika Mashariki na Kati zimeonekana kuwa 'vibonde', msimu huu tunataka tuwe tofauti na ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita," alisema Pluijm.
Aliongeza mbali na kukosa mechi za kirafiki na kimataifa, ushindani waliokutana nao kwenye mechi za ligi umesaidia kuijenga timu.

ATAKA USHINDI
Mholanzi huyo alisema atahakikisha wanashinda mechi hiyo ya kwanza ili wajisafishie njia ya kucheza hatua inayofuata.
Alisema anataka kuona safu yake ya ulinzi inafanya kazi kwa kujituma katika mechi zote. Ni wazi kazi hiyo kubwa wanayo mabeki pacha, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kelvin Yondani.
"Kwenye mpira huwezi kucheza mechi zote bila kukutana na mabonde, kufungwa au sare, hivyo vikwazo ni vya kawaida," alisema Pluijm.
Alisema amewaandaa wachezaji wake kutofikiria mechi za mbele badala ya kujipanga kushinda mchezo walionao.
"Kwa mfano sasa, tuna mechi mbili kabla ya kukutana na Simba, lakini jambo la ajabu ni kwamba watu wanaangalia mechi hiyo ya watani na kusahau zilizo jirani."

CANNAVARO, KAMUSOKO WAREJEA
Daktari wa timu hiyo, Nassor Matuzya hadi jana Jumapili, kwenye kikosi hicho hakukuwa na mchezaji majeruhi.
Nahodha Cannavaro yuko fiti na ataongoza wenzake kwenye mechi ya ugenini Jumamosi wiki hii.
Kuhusiana na Thabani Kamusoko ambaye hakucheza mechi iliyopita ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya 'Maafande' wa Prisons, daktari huyo alisemea naye ameshapona maumivu ya kifundo cha mguu.
Kwa upande wa beki Hajji Mgwali ambaye alikuwa anaumwa tumbo, naye maumivu yamekwisha baada ya kumaliza matibabu.

CANNAVARO-TUTAPAMBANA
"Ukishinda mechi ya kwanza, wachezaji hujiamini zaidi na hofu hutopotea. Natumaini tutafanya vizuri na kushinda mchezo huu wa kwanza na kufanya vizuri kwenye mechi zitakazofuata. Wachezaji wanajua kupitia mashindano haya wanapata fursa ya kujitangaza kwenye soko la kimataifa la wachezaji, hivyo hakuna atakayefanya makosa," alisema nahodha Cannavaro.