Wanafunzi 907,802 wanatarajiwa kujiunga na shule mbalimbali za sekondari nchini mwaka ujao, bila kuwapo awamu ya pili au ya tatu kama ilivyokuwa ikifanyika miaka ya nyuma.
Hatua hiyo ya kutoanza masomo kwa pamoja, ilitokana na uhaba wa madarasa, ambao wanafunzi wengine kusubiri hata miezi miwili ili ujenzi wa madarasa ukamilike kwanza ndipo waripoti shuleni.
Yawezekana madhara ya mtindo wa wanafunzi wa kidato kimoja kutoanza masomo kwa pamoja yasionekane, lakini ninaamini kwamba, wakipishana muda wa kuanza masomo, baadhi yao watashindwa kufanya vizuri.
Ili kuhakikisha kwamba, wanafunzi wote waliochaguliwa kidato cha kwanza mwaka ujao wanaanza masomo kwa pamoja, serikali inasema inajenga madarasa manne katika kila ilipo shule ya sekondari ya umma nchi nzima.
Hiyo ni kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, akisema tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, wanafunzi wataanza masomo pamoja.
Akiwa katika mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma, Ummy anaweka wazi kuhusu utaratibu huo.
Ikumbukwe, mbali na kuanza kidato cha kwanza kwa mafungu, baadhi ya shule ziligeuza majengo ya maabara kuwa madarasa ya muda hali iliyoelezwa kuwa ilisababisha wanafunzi kutojifunza masomo ya sayansi kwa vitendo.
Njia hiyo ilitumika ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaenda shule hata kwa awamu mbili au tatu, sababu kubwa ikiwa ni uhaba wa madarasa unaotokea kila mwaka wa masomo.
Pamoja na serikali kuamua kujenga madarasa manne kwa kila shule, ipo haja kushirikisha wadau wa elimu katika kufanikisha azma hiyo, lakini ujenzi huo uwe ni ajenda ya kudumu na endelevu, uhaba wa madarasa utabaki historia nchini, kwani hautakuwa wa kusubiri kusikia shule fulani ina uhaba ndipo mikakati ya ujenzi ianze.
Kwa mtazamo wangu ni kwamba, uhaba wa madarasa kila mwaka si jambo jema, hivyo ingefaa kila mmoja kwa nafasi yake akashiriki kikamilifu katika ujenzi huo ili hatimaye usiwepo uhaba wa madarasa tena nchini.
Iwapo ujenzi huo utakuwa ni ajenda ya kudumu kwa kushirikisha wadau wote wa elimu, kuanzia wazazi, kero itaisha, kwa kuzingatia kwamba, kila mwaka wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuongezeka.
Kwa mfano, wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2021, walikuwa ni 759,706, lakini kwa wale waliochagulikuwa kujiunga kidato hicho kwa mwaka ujao ni 907,802.
Idadi hiyo ni kubwa kidogo kuliko ya mwaka 2021, hali ambayo ni wazi kwamba, kuna haja ya kujipanga zaidi hasa kwa kufanya ujenzi wa madarasa kuwa ajenda ya kudumu badala ya kusubiri kwanza matokeo.
Serikali imeamua kujenga madarasa manne kwa kila shule, ili kupunguza uhaba huo, lakini kuna haja ya kushirikisha wananchi katika ujenzi huo hasa kwa kuzingatia shule hizo ni zao.
Ninaamini kwamba, wazazi na walezi wakishirikishwa katika ujenzi huo wanaweza kutoa mchango wa hali na mali, kuanzia nguvukazi yao au fedha, kwa kuwa wao ni wadau wakubwa wa elimu.
Kimsingi, kushiriki katika shughuli za maendeleo ni jukumu la kila mmoja, kwa maana hiyo, wana mchango mkubwa katika ujenzi wa madarasa ili kuwapunguzia watoto wao kero za kila mwaka.










