Jicho, maombi yetu kwa Simba kulinda nafasi 4 michuano CAF

22Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Jicho, maombi yetu kwa Simba kulinda nafasi 4 michuano CAF

PAMOJA na kuingiza timu nne msimu huu kwenye michuano ya kimataifa ngazi ya klabu inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF); mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho, hatimaye Tanzania imebaki na mwakilishi mmoja tu, Simba katika mashindano hayo yanayoongoza kwa ...

utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Hiyo ni baada ya Azam FC na Biashara United zilizokuwa zikiiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho baada ya Yanga kuwa ya kwanza kuaga katika Ligi ya Mabingwa kwa kutolewa raundi ya awali na Rivers United ya Nigeria.

Pengine Biashara United ingeweza kuwa mashindanoni kutokana na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya iliyoupata katika mchezo wa awali Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini ilishindwa kwenda kwenye mechi ya marudiano ugenini kutokana na changamoto ya vibali vya kutumia anga ya Sudan, Sudan Kusini na Libya, hivyo CAF ikaiondoa kuwapa Walibya hao nafasi ya kusonga mbele.

Hivyo kuifanya Tanzania kubaki na timu moja, Simba ambayo nayo ilitolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia Kombe la Shirikisho ambapo sasa itacheza mechi moja nyumbani na ugenini dhidi ya Red Arrows ya Zambia na kama ikipata matokeo ya jumla itatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Kwa maana hiyo, matarajio pekee kwa Tanzania katika kutetea kuingiza tena timu nne msimu ujao kwenye michuano hiyo ya CAF, ipo mikononi mwa Simba.

Kibarua cha kwanza cha Simba katika kusaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi, kitakuwa Jumapili wiki hii itakapoikaribisha Red Arrows katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana nchini Zambia Desemba 5, mwaka huu.

Kikubwa kwa sasa ni Simba kujiandaa vema kuelekea mchezo huo ili kuhakikisha inapata ushindi wa kishindo nyumbani kabla ya kwenda kumaliza kazi ugenini, huku ikitambua Watanzania wote wapo nyuma yao wakitaka kuona inapigania kulinda nafasi hizo nne.

Ikumbukwe hadi sasa tayari Libya imefikisha pointi za kuingiza timu nne kwenye michuano ya CAF msimu ujao, hivyo kama Simba ikishindwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kufanya vizuri kwenye michuano hiyo, ni wazi Tanzania itarudi kwenye timu mbili; moja Kombe la Shirikisho na nyingine Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao.

Hivyo, huu ni wakati ambao Watanzania wanapaswa kuwa kitu kimoja kwa kuanza kuiombea Simba katika maandalizi yake hadi siku itakapocheza mechi hizo mbili nyumbani na ugenini kwa kila mmoja kutambua kwamba inalipigania taifa katika kutetea nafasi hizo nne.

Huu si wakati wakutanguliza mbele itikadi zetu za 'kiklabu', lakini ni kipindi ambacho mashabiki wote wa soka wanapaswa kuweka kando tofauti zao na kuwa kitu kimoja katika kuiombea na kuitakia mema Simba isonge mbele kwenye michuano hiyo.

Nipashe tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, tunatambua wazi ili kuwa na matarajio makubwa ya timu zetu kufanya vizuri hatuna budi kupigania kuingiza klabu nne kwenye michuano hiyo inayoongoza kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Tunaamini kwa yeyote asiyeipa Simba sapoti katika michuano hiyo kwa sasa, ni sawa na kutokukubali Tanzania kupata nafasi nne katika michuano hiyo msimu ujao jambo ambalo halina tofauti na kuihujumu nchi kisoka.

Lakini, pamoja na maandalizi makubwa ambayo tunaamini Simba inayafanya kuelekea mchezo huo, mashabiki na Watanzania kwa ujumla hatuna budi kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili ili kuipa sapoti wakati ikicheza dhidi ya Red Arrows.