Ni kwasababu wanafunzi wa ngazi zozote wanaweza kutumia simu na kompyuta popote walipo ikiwa kuna mtandao, kujifunza na kujiongezea maarifa.
Hili linawezekana bila kujali uko kijijini au kwenye majiji makubwa, bora tu kuwe na umeme na ‘Wi-Fi’ au mtandao wa intanet usiotumia nyaya unaounganisha vifaa vya mawasiliano.
Hali hiyo pia imeleta ushindani kwenye elimu, kutokana na ukweli kwamba, TEHAMA inampa mwanafunzi maarifa zaidi ya kupata taarifa, ujuzi na elimu kupitia vyombo vya mawasiliano, kama simu na kompyuta.
Kutokana na umuhimu huo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeanzisha somo la TEHAMA kwa elimu ya msingi na sekondari ili kuwawezesha Watanzania kujiona kuwa ni sehemu ya dunia ambayo sasa ni kijiji kimoja.
Baadhi ya wadau wa elimu nao wanaendesha kampeni na mafunzo ya kuwahamasisha wasichana kupenda masomo ya sayansi, kuwa wabunifu na kupenda kujifunza TEHAMA.
Pamoja na juhudi hizo, kumekuwapo na changamoto ambazo ni vyema zingefanyiwa kazi ili somo hilo liweze kufundishwa kwa ufasaha na pia lienee katika shule za umma nchini.
Miongoni mwa changamoto hizo, ni baadhi ya walimu kukosa mafunzo ya somo hilo na pia shule nyingine kutokuwa na umeme hali ambayo inaleta ugumu kwa walimu na wanafunzi kufundisha au kujifunza TEHAMA.
Baadhi ya walimu wa shule za vijijini, wanadai kwamba wametengwa, kwa madai kwamba, hawapati mafunzo kuhusu TEHAMA, na hata wakiyapata, hawawezi kuyatumia kwa kuwa shule zao hazina umeme.
Katika mazingira hayo, wanasema, wanalazimika kufundisha wanafunzi kwa nadharia badala ya vitendo, hali ambayo inawafanya wabaki nyuma kwenye eneo hilo.
Wanatamani wanafunzi wa shule za vijijini wajifunze TEHAMA kwa vitendo ili nao wawe na ubora kama walivyo wenzao wanaosoma mijini.
Kimsingi, madai hayo ya walimu yanaweza kuwa na uzito na ingefaa kama yangefanyiwa kazi, ili kuwaongezea uelewa wa somo hilo badala ya kuwachorea kompyuta kwenye ubao.
Kuwachorea kompyuta ubaoni, wanaweza kuelewa, lakini huenda hatua hiyo haiwasaidii mwanafunzi kuelewa kifaa hicho kikamilifu.
Umeme utafanikisha somo hilo kufundishwa kwa vitendo katika shule zote na mafunzo ya walimu wanaoandaliwa kufundisha TEHAMA yakawa na tija.
Hivi karibuni, Wizara ya Nishati ilitangaza kushusha gharama za kuingiza umeme majumbani hadi kufikia Sh. 27,000, hivyo nafasi hiyo ingefaa kutumika kuhakikisha kila shule zinakuwa na umeme.
Kamati na bodi ambazo shule zao hazina nishati hiyo, zingeangalia uwezekano wa kuhakikisha zinaweka mikakati ya kupata umeme, ili kufanikisha somo hilo kwa wanafunzi wote wa mijini na vijijini.
Unafuu wa gharama za umeme ungetumiwa kuhakikisha nishati hiyo inakwenda hadi vijijini, kwani huko nako wapo wanafunzi wanaohitaji kujifunza somo la TEHAMA kwa vitendo.
Ni kweli kama wanavyokaririwa na vyombo vya habari baadhi ya walimu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakisema inawawia vigumu kufundisha mada za TEHAMA kwa kuwa hawajawahi kutumia kompyuta.
Lakini, inaaminisha kwamba, kuwapo kwa umeme katika shule za vijijini, ni hatua ya kwanza, aidha pia suala la kila shule kuwa na kompyuta ni la pili, hivyo ingefaa mikakati kuwapo kwa nishati hiyo kupewa mkazo.
Si vibaya kamati na bodi za shule zikahamasisha wananchi kuangalia uwezekano wa kuchangia fedha za kuvuta umeme na kisha ifuate mikakati ya kuwapo kwa kompyuta kwa kila shule.










