Yanga yaipania Majimaji leo

21Jan 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Yanga yaipania Majimaji leo

LIGI kuu Bara leo inafunga mzunguko wa kwanza, huku mabingwa watetezi, Yanga wakipania kuzoa pointi tatu kutoka kwa vibonde, Majimaji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji wa timu ya Yanga

Mabingwa Yanga wenye nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa leo kutokana na ubora wa kikosi chao kulinganisha na timu hiyo ya Songea, hawatakuwa na mchezaji 'kiraka' Mbuyu Twite na nahodha wao, Nadir Haroub 'Cannavaro' anayeendelea kuwa nje ya uwanja kutokana na kuwa majeruhi.
Wakati Yanga wakisukumizia nyavuni mabao tisa bila kuruhusu kamba zao kutikiswa hata mara moja katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu Bara, wapinzani wao Majimaji wameruhusu mabao 15 kugusa nyavu zao, huku wenyewe wakifunga mabao manne.
Kikosi cha kocha mpya wa Majimaji, Kali Ongala ambaye ni mchezaji wa zaman Yanga, kimefunga mabao tisa tu katika mechi 14 za ligi msimu huu (goli moja pungufu ya idadi ya mabao yote ya Amissi Tambwe wa Yanga), huku timu hiyo iliyorejea tena Ligi Kuu ikifungwa mara 24.
Ingawa Ongala ameanza kwa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Coastal Union Jumamosi iliyopita, timu yake itaingia uwanjani ikiwa na rekodi mbaya ya kufungwa mabao 6-1 na Simba Oktoba 30 (kipigo kikubwa zaidi msimu huu).
Na Yanga ambayo haikucheza soka la kuvutia ikishinda 1-0 dhidi ya Ndanda FC Jumapili, huenda ikakumbana na majaribu ya wachezaji wake wa zamani, beki Lulanga Mapunda na mshambuliaji Danny Mrwanda ikiwa timu hiyo ya Jangwani itaendelea kufanya makosa yaliyoigharimu kwa URA visiwani Zanzibar Januari 10.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, aliambia Nipashe kwa simu jana kuwa wamekiandaa vyema kikosi chao kuhakikisha kinaibuka na ushindi wakati wakimaliza mzunguko wa kwanza.
Wakati Yanga wakipambana kuziacha kwenye mataa Azam na Simba, Mwadui FC itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mwadui.
African Sports inayoshika mkia ikiwa na pointi nane baada ya mechi 14, itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
---------------------------