Samatta arudi Kongo kumvaa Katumbi

21Jan 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Samatta arudi Kongo kumvaa Katumbi

STRAIKA hatari wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta, aliondoka nchini jana asubuhi kurejea Lubumbashi ili kumalizana na uongozi wa klabu hiyo ya DR Congo na kupata baraka za kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.

mBWANA SAMATTA

Samatta aliondoka jijini Dar es Salaam jana saa tatu asubuhi akifuatana na mmoja wa viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo inamsaidia kumshawishi mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi amruhusu kuhamia Ubelgiji.
Samatta aliambia Nipashe juzi usiku kuwa anaondoka nchini akiwa tayari ameshafanya uamuzi wa hatma yake.
Samatta alisema atamshawishi Katumbi ili akubali kumpa ruhusa kwenda Ubelgiji na kama hilo litashindikana ataamua kubaki TP Mazembe hadi Aprili mwaka huu mkataba wake utakapomalizika ili aondoke akiwa ni mchezaji huru.
"Ninaondoka, lakini tayari nina mambo mawili kichwani, nina msimamo, nimeshajipanga, " alisema Samatta ambaye alifanya hivyo pia wakati usajili wake wa kuhamia Simba ulipogubikwa na utata.
Alisema ataendelea kuwa mvumilivu na anaamini kuwa kila kitu kinakwenda kwa wakati.
"Mara kadhaa nilipata timu, lakini sikufanikiwa kuondoka, hivyo kama kusubiri nimeshafanya hivyo sana muda uliobaki hautanisumbua kuvumilia kubaki Mazembe," aliongeza.
Uamuzi huo wa Samatta ambaye tayari ameshaingia makubaliano ya awali na Genk, umetokana na Katumbi kuendelea kusisitiza kuwa angependa kuona Mwanasoka Bora wa Afrika 2015 anajiunga na klabu ya Nantes ya Ufaransa na siyo mahali pengine.
Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo alisema jana kuwa angependa mshambuliaji huyo anamaliza mkataba wake na TP Mazembe na kuwa huru kufanya mazungumzo na timu atayoitaka.